
BEKI wa kimataifa wa Tanzania, Julietha Singano anazidi kuwakosha mashabiki wa FC Juarez inayoshiriki Ligi ya Wanawake nchini Mexico baada ya juzi kuingia kwenye kikosi bora cha wiki.
Huu ni msimu wa tatu mfululizo kwa beki huyo wa timu ya taifa ‘Twiga Stars’ kuichezea timu hiyo akifanikiwa kuingia kwenye kikosi cha kwanza moja kwa moja mbele ya nyota kibao kutoka mataifa ya Ulaya.
Chapisho lililowekwa kwenye mtandao wa kijamii wa timu hiyo liliwekwa picha ya Singano na kuandikwa, “Kwa kutuongoza hadi ushindi na kuacha kila kitu uwanjani mlinzi wetu alichaguliwa kuwa sehemu ya timu bora ya mechi mzunguko wa 16.”
Singano anakuwa mchezaji pekee kutoka kwenye timu ya Juarez kuingia katika kikosi bora cha raundi hiyo, kiufupi mbali na kuisaidia timu hiyo anaonyesha kiwango binafsi na nidhamu ya ukabaji.
Ndiye beki wa kati tegemeo kwenye kikosi hicho na ndani ya misimu mitatu aliyoitumikia Juarez amecheza jumla ya mechi 76.