Jukwaa la Wahariri Tanzania latema nyongo, lamshukia Waziri Silaa

Dar es Salaam. Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limeeleza kusikitishwa na mwenendo wa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa kutohudhuria matukio muhimu ya kihabari anayoalikwa kuwa mgeni rasmi.

Miongoni mwa matukio hayo ni la Mkutano Mkuu wa TEF uliofanyika jijini Dar es Salaam leo Alhamisi, lakini alitumwa mwakilishi.

Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile amesema jukwaa linasikitishwa kusuasua kuhudhuria matukio ya kihabari, likiwamo la Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari (EJAT) zilizotolewa Septemba 28, 2024.

Balile amesema hayo katika mkutano huo wenye kaulimbiu isemayo, “Weledi kwa Uhimilivu wa Vyombo vya Habari,” ambao Waziri Silaa alimtuma Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nicholaus Mkapa.

“Hajaonekana katika matukio mengine ya Jumuiya wa Maofisa Uhusiano (PRST) jijini Arusha. Tukasikia aliitwa Mbeya hakwenda na mkutano wa nane wa wahariri unaoendelea, tunakuomba Naibu Katibu Mkuu kumfikishia salamu za kusikitishwa kwetu,” amesema Balile.

Pia, amesema mwenendo huo haufurahishi na ameomba kukaa na tasnia ya vyombo vya habari kuweza kufahamu yaliyomo, ikiwamo tabia.

Huku wahariri wakashangilia, Balile amesema, Waziri Silaa anapaswa kutambua tasnia ya habari ni sehemu ya wadau wake muhimu anaopaswa kushirikiana nao kwa ukaribu.

Hata hivyo, TEF imemshukuru Waziri huyo kwa kuteua bodi ya ithibati inayokwenda kuleta utekelezaji wa sheria ya huduma za habari, hatua aliyoichukua baada ya kuingia madarakani.

Mbali na masikitiko hayo, Balile amesema zipo taasisi na mashirika yasiyotoa ushirikiano ipasavyo katika vyombo vya habari, jambo linalokwamisha mchakato wa maendeleo.

Amesema ushirikiano unapotolewa pale vyombo vinapohitaji taarifa unasaidia, lakini ikiwa kinyume na hapo inakwamisha mchakato wa kuujulisha umma habari muhimu.

“Bado wapo wachache ambao hawataki kutoa taarifa hata ukiwaendea, naomba Naibu Katibu Mkuu utusaidie uwafikishie salamu,” amesema Balile.

Pia, amesema hata hatua ya Msajili wa Hazina kutaka mashirika na taasisi za umma kukutana na vyombo vya habari kuulizana maswali umesaidia kuongeza uaminifu kati yao, ingawa wapo hao baadhi wasiotoa ushirikiano.

Akizitaja changamoto nyingine zinazowakabili, alitaja sheria ya mwaka 2016 ya Huduma za Habari iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2023, akisema kuna mambo yanapaswa kurekebishwa.

“Changamoto nyingine ni sheria inayomzuia mwekezaji kutoka nje ya nchi kumiliki zaidi ya asilimia 49 ya hisa katika kampuni ya habari, kwani suala hilo linafifisha uchumi wa vyombo vya habari nchini,” amesema Balile.

Pia, amesema hata mamlaka aliyopewa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo ni makubwa, ikiwamo kuwa mlalamikaji, mwendesha mashitaka na msimamizi wa utekelezaji wa hukumu.

Pia, ameipongeza Serikali kwa usimamizi bora uliosababisha Tanzania kupanda katika uhuru wa vyombo vya habari duniani hadi kufikia 97 kutoka nafasi ya 143 katika uhuru wa vyombo vya habari duniani.

“Suala hili halijaja bure, bali linatokana na uamuzi na usimamizi thabiti na maelekezo mahususi ya Rais Samia Suluhu Hassan uliopunguza maonyo na kukoromeana koromeana,” amesema.

Hata hivyo, akizungumza kwa niaba ya Waziri Silaa kwenye mkutano huo, Mkapa ambaye ni Naibu Katibu Mkuu aliahidi kufikisha salamu za TEF, akisema kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wake ameshindwa kuhudhuria mkutano huo.

Gazeti la Mwananchi lilimtafuta Waziri Silaa kwa simu ya mkononi, lakini simu yake iliita bila kupokewa.

Akijibu changamoto nyingine zilizowasilishwa na TEF, Mkapa amesema suala la umiliki wa wawekezaji wa kigeni ni la kisera na mchakato umeanza, huku akiahidi kuwashirikisha.

Mkapa amesema wanaendelea kupitia sera ili kuweka mfumo mzuri katika sekta ya habari. “Tutaendelea kuwashirikisha katika michakato pia, wizara inaendelea kufanyia kazi ripoti ya hali ya uchumi wa vyombo vya habari nchini,” amesema Mkapa.

Mkapa ametoa rai katika kipindi muhimu cha kuelekea uchaguzi, vyombo vya habari kuzingatia mambo muhimu ya weledi katika uandishi.

Baada ya ufunguzi na mada mbalimbali kutolewa, suala hilo liliibuka tena kwa mmoja wa wahariri kutoa hoja akitaka maelezo ya Mwenyekiti wa TEF, Balile juu ya Waziri Silaa hoja hiyo ijadiliwe kwa kina.

Licha ya wahariri wengi kuiunga mkono, lakini haikujadiliwa kwa maelezo kwamba wampe muda Waziri Silaa salamu zimfikie kupitia kwa Mkapa aliyemwakilisha, kisha itajadiliwa siku zijazo za mkutano huo utakaomalizika Jumamosi, Novemba 9, 2024.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo alisema jambo la kuzingatia kwa vyombo vya habari ni ukweli na haki ili kuilinda amani.

“Amani inakuja pale tunaporipoti kwa haki na usawa, tunaposhika kalamu zetu, tuzingatie maadili katika kazi zetu za uandishi wa habari,” amesema Mpogolo.