Jukumu la Serikali, wananchi kudhibiti utapeli

Watanzania wengi wamekuwa wakilalamikia kutapeliwa fedha zao na watu au taasisi zinazodai kuwatajirisha haraka kupitia miradi au mifumo ya upatu.

Tatizo hili limeonekana kuongezeka, hasa kutokana na tamaa ya watu kupata fedha kwa muda mfupi, hali inayosababisha wengine kushindwa hata kuchunguza kwa kina masharti na uhalali wa mikataba wanayojiunga nayo.

Kilio cha hivi karibuni kinatoka kwa baadhi ya wanachama wa Tanzania Community Empowerment Association (Tancea), ambao wanasema wamepoteza mamilioni ya fedha walizokuwa wakichangishwa na taasisi hiyo tangu mwaka 2021.

Wanachama hawa walivutiwa na ahadi za kupewa mabanda ya kuku, vifaranga 1,000, vyakula na dawa za mifugo, lakini matarajio hayo hayajatimizwa, na matokeo yake wengi wanajiona wamedanganywa.

Upo umuhimu kwa Watanzania kuacha tamaa ya utajiri wa haraka, badala yake wajifunze na kuchunguza taarifa za kampuni au mradi kabla ya kujiunga nao.

Tunasema ni jukumu la kila mtu kufahamu kuwa, katika ulimwengu wa biashara, hakuna njia rahisi ya kujipatia fedha.
Mtu anapaswa kujiuliza na kuchunguza iwapo kampuni au taasisi inayomwalika ni halali na kama inakidhi viwango vya uadilifu. Pia, ni vema wakatafuta ushauri wa kisheria kutoka kwa watu wanaowaamini kabla ya kujiingiza katika miradi au upatu.

Serikali pia iwe na mfumo thabiti wa ufuatiliaji na usimamizi wa kampuni hizi za upatu na miradi inayojinasibu kutajirisha haraka.
Jambo la kusikitisha ni kwamba mara nyingi Watanzania wanaamini kuwa kampuni inapoanzishwa na kusajiliwa, na ikijitangaza hadharani kupitia vyombo vya habari, basi ni halali.

Ukweli ni kwamba, baadhi ya kampuni hizi hupata usajili wa awali, lakini zinaendelea kwa njia zisizofuata sheria au kanuni za biashara. Serikali inahitaji kuimarisha mifumo ya udhibiti ili kampuni zote ziwe wazi na taarifa zao iwe rahisi kupatikana kwa umma.

Viongozi wa Serikali pia wana jukumu la kujiweka mbali na taasisi ambazo hawajazifanyia uchunguzi wa kina.
Kumekuwa na matukio ambapo viongozi wa Serikali, kama mawaziri, wakuu wa mikoa, na wakuu wa wilaya, wanatumika kuzindua au kushiriki hafla za kampuni hizi za upatu.

Inapotokea kiongozi wa Serikali anahusishwa na mradi wa upatu, wananchi hujenga imani kuwa kampuni hiyo ni salama na inayoaminika. Hii si sawa, na Serikali inapaswa kutoa miongozo madhubuti kwa viongozi kuhusu kushiriki katika matukio ya kampuni au miradi ya aina hii.

Pia, ni muhimu kwa Serikali kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mbinu za utapeli zinazotumiwa na kampuni hizi. Watu wanahitaji kujua ishara za miradi ya upatu na jinsi ya kujiuliza maswali ya msingi kabla ya kujiunga na miradi hiyo. Kwa maana hiyo, Serikali inaweza kuanzisha programu za kuelimisha wananchi kupitia vyombo vya habari. Tunaamini vita dhidi ya utapeli katika miradi ya upatu vinahitaji ushirikiano kati ya wananchi na Serikali.

Serikali inapaswa kutoa ulinzi kwa wananchi kwa kuweka mfumo wa uwazi na ufuatiliaji, wakati wananchi wanapaswa kuwa waangalifu na kutoingia kwa haraka kwenye miradi inayodai kuleta utajiri wa haraka.