Juhudi za Marekani za kuhalalisha jinai za Israel na kuendelea kuitumia silaha za mauaji ya umati

Vedant Patel, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, ametoa matamshi ambayo yanaonyesha kuwa Marekani haiko tayari kwa vyo vyote vile kumuwajibisha mshirika wake wa jinai za kivita, yaani utawala haramu wa Israel, na kuwa inatosheka tu kwa kutoa madai matupu yasiyo na maana kuhusiana na suala zima la haki za binadamu.

Katika hali ambayo Marekani ilikuwa imeupa utawala wa Kizayuni wa Israel muda wa mwezi mmoja ili uboreshe hali ya kibinadamu na kuruhusu kupelekwa misaada ya kibinadamu huko Gaza, lakini Patel amedai kuwa tathmini ya Marekani haionyeshi ishara yoyote kuwa utawala huo wa kibaguzi umekiuka sheria za Marekani. Katika barua aliyoiandika Anthony Blinken, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani kwa utawala wa Israel mwezi mmoja uliopita, alitoa wito wa kuruhusiwa kila siku lori 350 za misaada ya kibinadamu ziingie Gaza lakini kwa mujibu wa UNRWA, jambo hilo halijatekelezwa bali katika baadhi ya siku kiasi cha misaada ya kibinadamu kwa ukanda huo kimefikia chini ya lori 10.

Kuhusiana na hilo, tovuti ya habari ya Axios imeandika kwamba Washington haina nia ya kuuadhibu utawala wa Kizayuni licha ya hali hiyo mbaya ya kibinadamu huko Gaza. Vyanzo viwili vya habari ambavyo havikutaka kutajwa majina vimeiambia Axios kwamba hatimaye Blinken amepinga kutopelekwa silaha huko Israel kutokana na hali mbaya ya kibinadamu. Uamuzi huu umechukuliwa na serikali ya Marekani, ikiwa ni mshirika mkuu wa Israel na mtoaji mkubwa zaidi wa silaha na misaada mingine ya kijeshi kwa utawala huo, licha ya tamko la mashirika ya kimataifa ya kibinadamu kwamba Israel imekiuka matakwa ya Washington ya kupelekwa misaada zaidi ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza. Wajuzi wa mambo wanasema kwamba barua hiyo ya Blinken mwezi mmoja uliopita ilikuwa ya kipropaganda tu iliyokusudia kuwashawishi wapiga kura wa Marekani wampigie kura mgombea wa chama tawala cha Wademocrat. Mwishowe, Kamala Harris, Makamu wa Rais Biden na mgombea wa Chama cha Democratic, alishindwa na Trump katika majimbo yote 7 muhimu ya uchaguzi. Kutoungwa mkono Harris na Waislamu wa jimbo la Michigan ni mojawapo ya sababu za kushindwa kwake katika jimbo hilo.

Jinai za Israel dhidi ya Wapalestina kwa ushirikiano wa Marekani

Licha ya uungaji mkono mkubwa wa kisiasa na kijeshi wa Marekani kwa utawala wa Kizayuni na licha ya utawala huo kukataa kukubali matakwa ya jamii ya kimataifa, likiwemo ombi la Marekani la kusimamishwa vita vya Gaza au angalau kuruhusu misaada ya kibinadamu iwafikie watu wa Gaza, hasa kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, lakini utawala wa Biden na maafisa wakuu wa serikali ya Washington wametosheka tu kwa kutoa maonyo matupu yasiyo na maana kwa Tel Aviv. Wameamua kutotumia mashinikizo ya kisiasa na kifedha kuilazimisha Israel isitishe vita huko Gaza au kwa uchache iruhusu misaada ya kibinadamu iwafikie watu wa kaskazini mwa ukanda huo ambao wamezingirwa na jeshi la Israel kwa miezi kadhaa sasa.

Hii ni katika hali ambayo Umoja wa Mataifa umetangaza rasmi kuwa misaada haijawafikia watu wa Gaza kwa zaidi ya wiki mbili sasa. Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa ilitangaza Jumatatu kwamba mashambulizi ya anga ya siku 10 ya utawala wa Kizayuni kaskazini mwa Gaza, ambayo yamepelekea makumi ya maelfu ya watu katika eneo hilo kusalia bila chakula wala maji, ni ya kutisha sana. Imeendelea kusema kuwa kutokana na kuongezeka mapigano Mashariki ya Kati, inaonekana kwamba jeshi la Israel linapanga kulitenga kabisa eneo la kaskazini mwa Gaza na ukanda huo mzima na kuendeleza hujuma zake za kijeshi bila kujali kabisa maisha na usalama wa raia wa Palestina.

Uungaji mkono wa kijeshi na silaha wa Marekani kwa utawala wa Kizayuni pamoja na madai ya kutokiukwa sheria za Marekani na utawala wa Israel kuhusu misaada ya kibinadamu yanaendelea huku malalamiko na maandamano makubwa ya wananchi hususan wanafunzi na wafanyakazi wa taasisi muhimu za serikali kuu ya shirikisho kama vile Wizara ya Mambo ya Nje na Usalama wa Ndani, pamoja na wasomi na wanafikra yakiendelea kufanyika kulalamikia siasa za upandeleo za serikali ya Biden kwa Israel. Pamoja na hayo lakini serikali hiyo imefumbia macho malalamiko hayo yote na kueendelea kuupatia utawala huo unaochinja watoto na wanawake bila huruma, misaada ya kila aina ya kijeshi na kifedha na kuunga mkono kisiasa katika taasisi na majukwaa muhimu ya kimataifa.