
Joto la kusaka ubunge katika uchaguzi mkuu ujao kwenye majimbo yaliyopo Mbeya na Songwe limezidi kupanda, baada ya baadhi ya makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kutajwa kuwania nafasi hizo, jambo linalowaweka matumbo joto wabunge wanaohitaji kutetea nafasi zao.
Katika Mkoa wa Songwe wenye majimbo sita ya uchaguzi, majimbo ya Tunduma na Mbozi yamebainika kuwa na mnyukano mkali baada ya kujitokeza makada walio tayari kukabiliana na wabunge watakaotetea nafasi zao.
Mkoani Mbeya, majimbo ya Rungwe na Mbeya Mjini, pia, yanatajwa kukabiliwa na ushindani mkali, huku ikitarajiwa kwamba kama litaanzishwa jimbo jipya la Uyole, basi litapunguza ushindani katika jimbo la Mbeya Mjini.
Kukubalika kwao na uzoefu ndani ya chama hicho baada ya kushika nafasi kadhaa, ni sifa zinazotajwa kuwabeba makada hao na kujiona wanaweza na watosha kuingia kwenye kinyang’anyiro cha kura za maoni na kuibuka washindi.
Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira ameonya kuhusu matumizi ya fedha kwenye uchaguzi, huku akieleza kwamba hakuna mwenye hakimiliki ya ubunge au udiwani, bali wananchi ndio watafanya uamuzi muda ukifika.
Ushindani jimbo la Tunduma
Katika jimbo la Tunduma linalowakilishwa na David Silinde ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi, hali si shwari, anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Ndele Mwaselela, ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kutoka Mkoa wa Mbeya.
Itakumbukwa kwamba kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, kwenye mchakato wa kura za maoni, Silinde hakushinda, alipata kura 118 wakati Aden Mwakyonde aliibuka mshindi kwa kura 250, lakini hakuteuliwa na kamati kuu. Hata hivyo, baadaye kamati kuu ya chama hicho ilimteua Silinde, ambaye alihamia CCM kutoka Chadema akiwa mbunge wa Momba, kupeperusha bendera ya chama hicho katika jimbo la Tunduma.
Licha ya kushika nafasi nyingi ndani ya chama hicho, Mwaselela anatajwa kuwa kimbilio na msaada wa shida za wananchi, hasa pale wanapokuwa na uhitaji, uwezo wake wa kuwasemea kwenye changamoto mbalimbali kwa viongozi wakuu wa kitaifa, jambo linalompa nafasi.
Mfano mzuri ni kwenye mkutano wa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira, uliofanyika wiki iliyopita mkoani Songwe, akikagua utekelezaji wa ilani ya chama hicho, Mwaselela aliibua changamoto na kushangiliwa na wananchi wakati wote.
Kada mmoja wa CCM ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema upepo haujakaa vizuri upande wa Silinde kutokana na nguvu ya mpinzani wake na anashauri kama anahitaji nafasi hiyo, basi akagombee jimbo la Momba, alikokuwa.
“Kwa kweli katika jimbo hili, nafasi yake ni finyu sana, upepo hauko upande wake. Namshauri akitaka kugombea aende Momba alikokuwa, huko atakuwa na ngome kubwa kuliko hapa Tunduma,” anasema kada huyo.
Mkazi wa Tunduma, Frank Mambosasa anasema mbunge wao amekuwa mbali na wananchi, kila wanapomhitaji jimboni hawampati kwa wakati, hivyo wakipata mtu makini wako tayari kufanya mabadiliko.
Mtifuano Momba, Mbozi, Ileje
Wakati makada wa CCM Tunduma wakiona nafasi ya Silinde iko Momba, Jimbo la Momba linalowakilishwa na Condester Sichalwe, linakabiliwa na ushindani kutoka kwa Ombeni Nanyaro, kada wa chama hicho anayetajwa na wanachama.
Jimbo la Mbozi linaloongozwa na mbunge, George Mwenisongole, linakabiliwa na ushindani kutoka kwa mbunge wa zamani, Godfrey Zambi, aliyewahi pia kuwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya.
Katika siasa za eneo hilo, Zambi, aliyewahi kuwa mbunge wa Mbozi Mashariki, bado anakubalika katika eneo hilo, huku akitajwa kuwa na nafasi kubwa kwenye uchaguzi ujao endapo atateuliwa kuwakilisha wananchi katika jimbo hilo.
“Hapa Mbozi, Zambi anakuja juu sana, hata kwenye mikutano ukifuatilia, wananchi wanamshangilia sana kuliko hata mbunge wao. Kama ni ubunge, ana nafasi kubwa katika jimbo hili,” anasema Emmanuel Mwashiuya, mkazi wa Mbozi.
Zambi, aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Kilimo, hata kwenye mkutano wa ndani wa chama hicho, aliofanya Mbozi, mgeni rasmi akiwa Makamu Mwenyekiti wa CCM, Tanzania Bara, Stephen Wasira, alipata nafasi ya kuzungumza na kushangiliwa.
Mbunge wa Ileje, Godfrey Kasekenya ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ujenzi, anakabiliwa na upinzani kutoka kwa kada wa CCM aliyeongoza kwenye kura za maoni mwaka 2020, Wilman Ndile aliyepata kura 172, Kasekenya akiambulia kura 106, hata hivyo aliteuliwa na kamati kuu kupeperusha bendera ya CCM.
Kivumbi Mbeya Mjini
Kivumbi cha kusaka nafasi ya kuwania ubunge kupitia CCM Mkoa wa Mbeya, nako kimeendelea kuchukua sura mpya baada ya mwenyekiti wa chama hicho mkoani hapo, Patrick Mwalulenge naye kudaiwa kutia mguu kugombea katika jimbo la Mbeya mjini au lingine linalotarajiwa kugawanywa (Uyole).
Inaelezwa turufu ya Mwalulenge kugombea nafasi hiyo itatokana na uamuzi wa Mbunge wa Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson kugombea katika jimbo gani kati ya Mbeya Mjini au Uyole. Kama atakwenda kugombea jimbo jipya litakalopatikana baada ya kugawanywa, basi atagombea Mbeya Mjini.
Hata hivyo, mvutano unaonekana kuwa mkubwa kati yake na baadhi ya vigogo wa CCM Mkoa wa Mbeya, ambao nao kila mmoja anatajwa kuonyesha nia ya kugombea, akiwemo Mwaselela na wengine.
Mchambuzi afafanua
Mchambuzi wa siasa za kutoka nyanda za juu kusini, Mwaihojo Mwambipile anasema wanasiasa wa mikoa ya Mbeya na Songwe hawana siasa za maono ya maendeleo, bali wana siasa za kuwapumbaza wananchi ili waendelee kuwaabudu.
“Kama wangekuwa na siasa za maendeleo na masilahi ya wananchi wangekuwa wanajipima uwezo wao kabla ya kuingia kwenye kunyang’anyiro,” anasema.
Anasema watu wengi wanaojitosa kupigania madaraka wanalenga kupigania maslahi yao binafsi, hawana jipya kwa wananchi.
“Changamoto hiyo inatokana na jamii yenyewe haina maono, kama ingekuwa na malengo, wangeweza kutafuta mwenye nia ya dhati katika kutafsiri maono yao, sasa kila mtu anagombea kutafuta maslahi yake,” anasema Mwambipile.
Mwambipile, ambaye ni Chifu wa Busokelo, anasema tatizo la viongozi hao ni kwamba muda mwingi wanashindwa kueleza serikali imefanya jambo gani kwa wananchi, badala yake wanasema mama kafanya.
“Wameondoa kuutambulisha utaasisi na kumsifia mtu, uchawa sasa, saa hizi kuna tatizo la ajira katika jamii, badala ya kuja na mikakati hiyo na kwa kutengeneza ajira walau zenye staha, nao wanajikita kuzungumzia kumpamba mtu,” anasema.
Anasema jamii ya Kitanzania, hasa vijana wana nafasi ya kubadili mlengo wa siasa za sasa, mfano zamani wakati yeye anakua ajira haikuwa tatizo, ingawa umaskini ulikuwa unaimbwa zaidi.
“Tanzania kwa sasa tatizo la ajira ni kubwa, na hii Mbeya pamoja na Songwe vijana wengi wanaogombea hawajui matatizo yetu na hii inakuwa ngumu kuipatia jamii kile wanachohitaji,” anasema.
Anasema waliowengi wanatafuta nafasi za ubunge kwenda kuvuna na kuondoka zao na kuendelea na maisha mengine na kuwaacha wananchi njiapanda. “Wanazungumza sera ya viwanda, ukiangalia hapa Mbeya na Songwe viwanda vyenyewe viko wapi? Vijana ni wengi hawana kazi, tungekuwa na viongozi wenye kubeba ajenda za jamii mambo yangebadilika,” anasema.
Wasira aonya minyukano
Wasira amefanya ziara yake katika mikoa ya Songwe na Mbeya ambapo kuhusu kuwania nafasi za ubunge na udiwani, anasema Tanzania ina vijana wengi na kazi ya CCM ni kujenga viongozi bora, kazi waliyoifanya tangu kupata uhuru, hivyo wajitokeze wakanolewe ili wawe tayari kuwatumikia wananchi.
Wasira anasema muda ukifika kamati za siasa ngazi ya kata ziwatafute watu wenye uwezo wa kuwania nafasi ya udiwani sambamba na kamati za siasa wilaya ziwatafute wenye uwezo wa kuwania nafasi za ubunge, ili waweze kupata viongozi wanaokubalika. Wasira anasema hakuna mwenye haki miliki na nafasi ya ubunge, wakati ukifika duka linakuwa wazi kila mtu kugombea na kwa wale wanaohitaji madaraka ya kujimilikisha waanzishe duka lao.
“CCM ni duka la wote, na wenye kuuza wanabadilika, leo yule kesho mwingine, lakini tuna shida ndani ya hiki chama, tunaacha kazi ya kujenga chama chetu, tuna matatizo ya wakulima wa chai pale wanasema hawalipwi fedha zao kule Rungwe,” anasema na kuongeza:
“Watu wanaanza kujadili mwenyekiti anakaa wapi siku hizi, hatuwezi kuunda chama kikubwa namna hii halafu tunaanza kushughulika na matatizo ya aina hiyo. Tunataka vikao vyetu vya chama vizungumze matatizo ya wananchi, narudia, vikao vyetu vizungumze matatizo ya wananchi,” anasema Wasira.
Kwa mujibu wa Wasira, kuna matatizo mengi ya wamachinga, bodaboda, hivyo ni muhimu kuzungumza matatizo ya watu hao ili wananchi wajue wakiwa na kero wakimbilie ndani ya chama hicho. “Mambo ya ubinafsi yanahusiana na nini ndani ya chama chetu? Uchaguzi ukiisha kwa sababu fulani kashinda, unanuna miaka mitano yote na tambueni madaktari wanasema ukinuna kwa muda mrefu utakufa bure, lazima ukubali matokeo,” anasema.
Wasira anasema baadhi wanakuja na hoja kwamba wanaungwa mkono na wanachama wengi, akidai kauli hiyo si sahihi, kwani wanachama wote wanamilikiwa na Chama hicho: “Unasemaje wa kwako kwani uliwaumba? Wakwako? Una matatizo kweli, tuache hayo,” anasema Wasira.
Anasema wengine wakishindwa kwenye kinyang’anyiro wanaanza kudai warudishiwe fedha zao; “Kwani hizo fedha ulinikopesha, shauri yako uliacha kununua mboga ukaenda kununua kura,” anasema.