Joseph Kabila: Mgogoro Mashariki mwa DRC unatokana na utawala mbovu wa serikali ya Tshisekedi

Wakati wa mahojiano na Gazeti la Afrika Kusini la Sunday Times siku ya Jumapili hii, Februari 23, Joseph Kabila, rais wa zamani wa DRC, amebaini kwamba mgogoro unaoendelea nchini humo unahusishwa zaidi na utawala mbovu wa mrithi wake Félix Tshisekedi. Mgogoro huu, ambao ulianza mwaka 2021 kulingana na Joseph Kabila, ni wa usalama na wa kibinadamu, lakini hasa wa kisiasa, kijamii, kimaadili na sera.

Imechapishwa:

Dakika 2

Matangazo ya kibiashara

“Katika ngazi ya kitaifa, sababu kuu ya mgogoro huu ni nia ya wazi ya uongozi wa sasa kuvunja Mkataba wa Jamhuri. Mkataba huu, uliotokana na mazungumzo baina ya Kongo huko Sun City, ulipepekea kupatikana kwa Katiba iliyopitishwa na kura ya maoni kiraia mwaka 2006,” anabainisa Joseph Kabila.

Kulingana rais huyo wa zamanai wa DRC, kuvunjwa kwa Mkataba huu wa Jamhuri kulidhihirishwa kwanza na “ukiukwaji wa makusudi na wa mara kwa mara wa Katiba na sheria za nchi. Kisha, uchaguzi wa Disemba 2023 ulivuruga mfumo wa kisheria na viwango husika vya kimataifa, na hivyo kuzidisha mfumo wa kiongozi kutokua halali, kupunguza kwa njia bandia uzito wa upinzani wa kisiasa na hivyo kumfanyarais kuwa kiongozi mkuu wa serikali.”

Demokrasia yapiga hatua nyuma

Mrithi wake, Félix Tshisekedi, alitangaza hadharani nia yake ya kurekebisha Katiba; “ambayo inaleta mkwamo mkubwa wa kidemokrasia.”

Joseph Kabila pia ameshutumu kunyamazishwa kwa upinzani wa kisiasa:

“Vitisho, watu kukamatwa kiholela, mauaji kikatili, pamoja na wanasiasa kulazimishwa kwenda uhamishoni, waandishi wa habari na watu waliokuwa wakitoa maoni yao, wakiwemo viongozi wa kidini, vimekuwa walengwa wakuu wa utawala wa Tshisekedi.”

Joseph Kabila anasema madai ya raia wa Kongo dhidi ya serikali yao lazima yasikilizwe. Kuendelea kwa utawala mbovu wa sasa kunaweza tu kusababisha mawimbi mapya ya machafuko ya kisiasa, ukosefu wa usalama, ukosefu wa utulivu wa kitaasisi, migogoro ya silaha na hata vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Paul Kagame na M23?

Alitaka suluhu la kina la mzozo huo, “na sio tu kutuma wanajeshi na zana za kijeshi. Hiyo itakuwa sawa na kupoteza rasilimali za thamani kusaidia udikteta, badala ya kusaidia DRC kuelekea demokrasia, amani na utulivu, na kuwa rasilimali kwa eneo la kusini mwa Afrika na kwa bara zima.”

Ili kurejesha amani na utulivu mashariki mwa nchi, ni muhimu kutatua suala la makundi ya kitaifa na ya kigeni yenye silaha yaliyopo katika ardhi ya Kongo. Hata hivyo, Rais huyo wa zamani ameongeza, “kinyume na kile mamlaka ya Kinshasa inachotaka tuamini, mzozo huo haukomei kwa vitendo vya kizembe vya M23 – vilivyowasilishwa kimakosa kama kundi la wanaotaka madaraka na vibaraka wa taifa la kigeni bila matakwa halali – wala kwa kutoelewana kati ya DRC na Rwanda.”