
Kiungo wa Arsenal, Jorginho ameripotiwa kufikia makubaliano ya kujiunga na Flamengo kwa uhamisho wa bure mwishoni mwa msimu huu.
Mtaliano huyo yupo kwenye miezi ya mwisho ya mkataba wake kwenye kikosi cha Arsenal na dili lake litafika ukomo Juni na sasa amekubali kurudi kwenye nchi alikozaliwa kwa uhamisho wa bure kabisa kwenye uhamisho wa dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Kutokana na kubakiza miezi sita kwenye mkataba wake wa sasa, hivyo Jorginho ana ruhusa ya kusaini dili la awali na klabu nyingine ya ng’ambo.
Klabu ya Brazil, Flamengo imeripotiwa kupambana kunasa saini ya kiungo huyo mwezi uliopita, lakini haikutaka kulipa pesa yoyote ya uhamisho na hivyo inasubiri imchukue bure kama mchezaji huru mwishoni mwa msimu.
Taarifa za kutoka Brazil zilizoripotiwa na BolaVIP zimebainisha kila kitu kimefikiwa na Flamengo imekubali kulipa mshahara anaotaka Jorginho.
Beki wa zamani wa Chelsea, Filipe Luis, ambaye kwa sasa ni kocha mkuu wa Flamengo, alizungumza na mchezaji huyo wa Arsenal mwezi uliopita na kufanikiwa kumshawishi kwenda kujiunga na mamba hiyo. Huko Brazil, Jorginho amekuwa akiwindwa kwelikweli na mwezi uliopita, iliripotiwa Palmeiras ilizungumza naye pia ikimtaka akacheze kwenye kikosi chao.
Jorginho, ambaye aliwahi kukipiga Chelsea ni mmoja kati ya mastaa saba ambao wataonyeshwa mlango wa kutokea huko Arsenal mwisho wa msimu. Kinachoelezwa, kocha Mikel Arteta ataondoa watu kwenye kikosi chake ili kupata pesa za kusajili kwenye dirisha lijalo.
Kiungo Jorginho analipwa Pauni 110,000 kwa wiki, hivyo Arsenal itafanikiwa kuokoa pesa nyingi itakapoachana na mchezaji huyo mwisho wa msimu, ambaye ilimsajili miaka miwili iliyopita akitokea Chelsea kwa ada ya Pauni 12 milioni. Ameichezea Arsenal mara 73 kwenye Ligi Kuu England.
MISHAHARA MIKUBWA YA MASTAA ARSENAL
-Sterling, Pauni 325,000 kwa wiki
-Havertz, Pauni 280,000 kwa wiki
-Jesus, Pauni 265,000 kwa wiki
-Rice, Pauni 240,000 kwa wiki
-Odegaard, Pauni 240,000 kwa wiki
-Partey, Pauni 200,000 kwa wiki
-Saka, Pauni 195,000 kwa wiki
-Saliba, Pauni 190,000 kwa wiki
-Martinelli, Pauni 180,000 kwa wiki
-White, Pauni 150,000 kwa wiki
-Zinchenko, Pauni 150,000 kwa wiki
-Calafiori, Pauni 120,000 kwa wiki
-Tierney, Pauni 120,000 kwa wiki
-Jorginho, Pauni 110,000 kwa wiki