Jordan alivyobadili mapishi hadi Cuba

Jina la Michael Jordan, 62, lina ufalme katika Ligi ya Kikapu Marekani (NBA) na wapenzi wa mchezo huo duniani wanajivunia kushuhudia kipaji na alama aliyoiacha ndani na nje ya uwanja.

Nje ya uwanja kuna mengi unayoweza kuzungumzia kuhusu maisha binafsi ya Jordan, mojawapo ni kubadili mapishi nyumbani kwake kwa kumleta fundi mpya wa jiko mwenye asili ya Cuba, Yvette Prieto, 46, ambaye ndiye mkewe tangu 2013.

Gwiji huyo aliyekipiga Chicago Bulls kwa mafanikio akiweka rekodi nyingi NBA, hiyo ilikuwa ni ndoa yake ya pili kufuatia kutalikiana na mkewe wa zamani, Juanita Vanoy ambaye walidumu kwa miaka 17 na kujaliwa watoto watatu.

Jordan na Juanita walifunga ndoa Septemba 2, 1989 katika kanisa la A Little White Wedding Chapel huko Las Vegas, Marekani. Kabla ya bahari kuchafuka uhusiano huo uliwaleta duniani Jeffrey (1989), Marcus (1990) na Jasmine (1992).

Baada ya miaka 13 ya kuishi pamoja kama familia mnamo Januari 2002, wawili hao waliwasilisha mahakamani kesi ya talaka wakitaja tofauti zisizoweza kusuluhishwa kama sababu ya uamuzi huo lakini walitatua migogoro yao muda mfupi baadaye.

Hata hivyo, ilifika hatua suluhisho pekee likaonekana ni talaka, nayo ikatoka Desemba 2006 ukiwa ni uamuzi wa pande zote mbili na wa amani huku Juanita akivuta Dola262 milioni na kuifanya kuwa talaka ya watu maarufu iliyotoka kwa fedha nyingi. 

Miaka miwili baadaye, yaani 2008, Jordan akiwa viwanja akila zake bata akakutana na Yvette, na punde tu ukaribu wao ukazidi kuwa mkubwa hadi msimu wa Krismasi 2011 ambapo walichumbiana na mipango ya kufunga ndoa ikaanza. 

“Wamekuwa wakipanga kwa miezi na miezi kuhusu jinsi watakavyofunga ndoa. Ni wazi kuwa Jordan anataka kumpa Yvette kila kitu ambacho amewahi kutaka kutoka kwake,” chanzo kimoja kiliuambia mtandao wa The People wakati huo.

Yvette alizaliwa Machi 26, 1978 nchini Cuba ingawa familia yake ilihamia Miami, Marekani alipokuwa mdogo na kukulia karibu na bahari ya eneo hilo huku akisoma Miami Sunset kisha Chuo Kikuu cha Florida.

Kwa mujibu wa ESPN The Magazine, mwanamitindo huyo aliyefanya kazi kama mbunifu wa Alexander Wang, anapenda sana kusafiri na meli ukiwa ni utamaduni wake wa miaka mingi kitu ambacho humlazimu Jordan kufanya hivyo ingawa hapendi kusafiri juu ya maji.

Hata hivyo, mwanzoni mwa miaka ya 2000 kabla ya kukutana na Jordan, Yvette alikuwa na uhusiano na Julio Jr ambaye ni mtoto wa mwimbaji wa Hispania, Julio Iglesias na kaka wa mwanamuziki wa Pop wa Kilatini, Enrique Iglesias.

Mwaka 2003 katika mahojiano yake na Jarida la Hola! ikiwa ni muda mfupi baada ya kuachana na Yvette, Julio Jr alikiri kwamba kwa kipindi chote mwanamitindo huyo alikuwa msichana mzuri kwake, mwenye upendo na asiye na mambo mengi.

Hatimaye Aprili 27, 2013, Jordan na Yvette wakafunga ndoa katika kanisa la Bethesda-by-the-Sea huko Palm Beach, Florida na kuhudhuriwa na wageni 500 waliosafirishwa kwa basi la watalii hadi uwanja wa gofu wa Bears Club ilipofanyika shughuli hiyo.

Miongoni mwa watu maarufu waliohudhuria harusi yao ni pamoja na Spike Lee, Patrick Ewing na Tiger Woods huku waimbaji Robin Thicke na Usher wote wakitumbuiza mbele ya wageni.

Kufikia Februari 9, 2014, wawili hao wakajaliwa kupata watoto mapacha na kuwapa majina ya Victoria na Ysabel, hiyo ni baada ya hapo Novemba 2013 Yvette kuthibitisha kuwa walikuwa wanatarajia jambo hilo ingawa hawakufichua kwamba walikuwa mapacha. “Yvette na watoto wanaendelea vizuri na kusema kweli familia ina furaha tele kwa kuzaliwa kwao,” msemaji wa Jordan alinukuliwa na vyombo vya habari wakati huo.

Julai 2023 Jordan na familia yake walienda mapumzikoni Italia walipoungana na marafiki zao Magic Johnson, Samuel L. Jackson na Jaji Greg Mathis, na wake zao kisha kupata chakula cha usiku katika mgahawa maarufu duniani wa Da Paolino Ristorante huko Capri.

Ingawa Yvette alikutana na Jordan akiwa ameshastaafu kucheza kikapu, lakini bado ni mtu maarufu na anayejali chapa yake, hivyo mara zote amekuwa akizingatia usalama wake na familia kwa ujumla kila wanapoenda.

ESPN iliripoti Jordan aliajiri walinzi wa kuandamana nao katika safari za nje ya nchi na mara zote huficha utambulisho wao wakitumia majina ya msimbo ili kuhakikisha faragha na usalama wao ambapo Yvette hutumia jina la Harmony huku Jordan akijita Yahweh.

Na hadi sasa Michael Jordan ni miongoni mwa wanamichezo wenye nguvu kubwa ya ushawishi duniani, anakumbukwa kwa kuchochea mauzo makubwa ya viatu vya Nike vya Air Jordan ambavyo vilianzishwa mwaka 1984.

Akitajwa na wengi kama mchezaji bora zaidi wa NBA kwa muda wote, mwaka 2016 Jordan aliandika rekodi kama mchezaji wa kwanza kutoka katika ligi hiyo maarufu kufikia hadhi ya ubilionea na hadi sasa Forbes wanakadiria utajiri wake kuwa ni Dola3.5 bilioni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *