Job Ndugai: Safari ya kisiasa ya Spika wa Bunge la 12

Dodoma.  Job Ndugai ni jina lisilopitwa katika historia ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aliwahi kushika nafasi ya Spika wa Bunge la 12, akiongoza muhimili huu wa dola kikatiba kwenye kipindi cha mpito muhimu katika siasa za Tanzania.

Umahiri wake katika kuendesha shughuli za Bunge, pamoja na msimamo wake thabiti kuhusu masuala ya uwajibikaji wa Serikali, ulimfanya kuwa mmoja wa wanasiasa waliotajwa kwenye mijadala ya kitaifa.

Baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, Ndugai alichaguliwa kuwa Spika wa Bunge la 12 kwa kura nyingi za wabunge.

Akiwa mbunge wa Kongwa, katika uchaguzi wa Spika wa Bunge la 12 uliofanyika Novemba 10, 2024 alishinda kwa kupata kura za ndiyo 344 kati ya kura 345 zilizopigwa, ukiwa ni ushindi wa asilimia 99.7.

Alishika nafasi hiyo kwa miaka miwili, akiiongoza taasisi hiyo kwa msisitizo mkubwa juu ya nidhamu, kuheshimu kanuni za Bunge na kuhakikisha Serikali inawajibika kwa wananchi kupitia wawakilishi wao bungeni.

Alipigania masilahi ya wabunge, mara kadhaa alitumia kipaza sauti akiwa ameketi kwenye kiti cha Spika akiuliza kuhusu posho za wabunge akitumia maneno: “Yale mambo yetu” huku akimtaka Katibu wa Bunge kuzingatia suala la malipo.

Siku 422 za mwanzo katika Bunge la 12 zilikuwa za mchakamchaka kwa wabunge na mawaziri.

Novemba 24, 2020 zikiwa zimepita siku 10 baada ya kuchaguliwa kuwa Spika, Ndugai aliwaapisha hadharani, nje ya ukumbi wa Bunge wabunge 19 wa viti maalumu kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), licha ya kuwapo mzozo kwamba hawakupitishwa na chama hicho kushika nyadhifa hizo.

Waliapishwa nje ya ukumbi wa Bunge kwa kuwa kipindi hicho kilikuwa cha ugonjwa wa Uviko 19.

“Nitawalinda kwa namna yoyote ile, fanyeni kazi zenu za kibunge na kuwatumikia Watanzania mimi nipo pamoja nanyi msijali, ninyi ni wabunge kama walivyo wengine,” alisema Ndugai.

Mzozo kuhusu nafasi za wabunge hao ulisababisha wavuliwe uanachama wa Chadema na kesi kufunguliwa mahakamani.

Mkwara kwa mawaziri, AG

Oktoba 30, 2021 Ndugai aliwashukia mawaziri, naibu mawaziri na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kuhusu marekebisho ya sheria.

Akizungumza kwenye mkutano wa mafunzo ya kuwajengea uwezo watendaji hao ulioandaliwa na taasisi ya uongozi alisema:

“Utaratibu wa kutunga sheria na kisha ikarudishwa haraka bungeni kwa marekebisho, ujue hapo mna matatizo na hili la mawasiliano lazima kutakuwa na shida.”

“Kuna sheria zinatungwa na Bunge, baada ya kupitishwa tu zinaletwa tena kwa ajili ya marekebisho hii siyo sawa, hapa unaonekana ni uzembe au kutokuwa na mawasiliano kati ya Mwanasheria Mkuu na mawaziri, kajipimeni wenyewe badala ya kusubiri mpimwe na watu,” alisema.

Alieleza huchukizwa na kitendo cha kukosekana mawasiliano baina ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na mawaziri, akisema asingetamani mambo hayo yajitokeze.

Kauli hiyo ilizua minong’ono miongoni mwa mawaziri wakisema ni kama wamedhalilishwa na kuna wakati walianzisha vuguvugu la chini kwa chini la kutokuwa na imani naye.

Jumamosi Mei 29, 2021 Ndugai alihoji namna sheria ya kutaifisha mifugo inayoingia kwenye hifadhi ilivyopitishwa na Bunge.

Alisema wakati wa kupitisha sheria hiyo huenda wabunge walikuwa wamelala usingizi.

“Hii sheria ni mbaya, huenda wakati inapitishwa wabunge walikuwa wamelala usingizi na kama hawakuwa wamelala basi yawezekana mimi nilikuwa safarini siku hiyo, haifai na haiwezekani kuwa na sheria ya namna hii,” alisema.

Aliizungumzia sheria hiyo akisema  tembo wakiingia kwenye mashamba ya watu mbona hawataifishwi.

Kutukuza usomi

Akiwa kwenye kiti cha Spika Septemba Mosi, 2021 Ndugai alitaja kada nne alizosema zinamkera kutokana na kutukuza usomi wao wakitaka waanze kutukuza kisomo chao kabla ya majina yao.

Alizitaja kada hizo kuwa ni za wahasibu, wahandisi, mawakili na madaktari wa kusomea ambao alisema siyo lazima kila mtu kuanza na kutukuzwa kwa kisomo chake.

Safari ya kujiuzulu

Katika uongozi wake, Ndugai alisisitiza matumizi ya fedha kwa uangalifu mkubwa na alionyesha wasiwasi kuhusu ongezeko la deni la Taifa. Kauli yake ya mwaka 2021 kuhusu Tanzania kuendelea kukopa kutoka nje ya nchi ilizua mjadala mpana, siyo tu bungeni bali pia katika jamii ya Watanzania kwa ujumla.

Kauli hiyo ilitafsiriwa kwa namna mbalimbali, huku baadhi wakiona kuwa ilikuwa ni sauti ya tahadhari kwa mustakabali wa uchumi wa nchi, ilhali wengine waliiona kama kinyume cha msimamo wa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Januari 6, 2022, Job Ndugai alitangaza kujiuzulu nafasi ya Spika wa Bunge, hatua ambayo ilishangaza wengi. Alieleza amefikia uamuzi huo kwa hiari baada ya kutafakari kwa kina. Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Spika kujiuzulu kwa hiari katika historia ya Bunge la Tanzania tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Ndugai aliitisha mkutano na vyombo vya habari akatumia sekunde 189 (dakika 3:09) kutoa kauli ya kuachia ngazi.

Alifikia uamuzi huo baada ya vuguvugu la siku 12 mfululizo baada ya kauli yake kuhusu deni la Taifa aliyoitoa Desemba 26, 2021 kwenye Mkutano wa Umoja wa Wagogo (Mikalile ye Wanyausi) alikozungumzia suala la kujitegemea kuliko kuwa tegemezi.

Katika hotuba alitoa mfano wa Bunge lilivyopitisha sheria ya tozo kwenye miamala ya simu ili kupunguza utegemezi na madeni kwani nchi ilishakopa sana kwa ajili ya miradi ya maendeleo ndipo akasema: “Kuna wakati nchi itapigwa mnada” kama hatutakuwa makini katika kujitegemea.

Mwaka mmoja baadaye Ndugai alimtaja Waziri Mkuu mstaafu John Malecela kwamba ndiye alimuanzishia safari ya kujiuzulu, kwani alimfuata nyumbani usiku wa Januari 5, 2021 na kumwomba aachie nafasi ya Spika wa Bunge.

Ndugai alisema haikuwa kawaida na hakuna siku ambayo Mzee Malecela aliwahi kuomba kuonana naye muda kama huo lakini alipokea simu na mkongwe huyo wa siasa nchini akaomba kuonana naye nyumbani kwake Kongwa.

Walipokutana alisema wakawa na maneno machache ya kumwomba akijiuzulu kiti cha Spika jambo alilolitekeleza siku iliyofuata.

Maisha baada ya uspika

Ndugai mwanasheria, mwanasayansi na mtaalamu aliyebobea katika masuala ya uhifadhi ameendelea kuwa mbunge wa Kongwa akishiriki siasa ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Mchango wake katika kujenga hoja za kibunge na ushauri kwa viongozi wenzake uliendelea kujitokeza.

Amekuwa mbunge wa Kongwa tangu 2000 aliporithi kiti cha Gideon Senyagwa ambaye hakugombea. Amewahi kuwa Naibu Spika na Mwenyekiti wa Bunge. Kwamba atagombea tena ubunge, ni suala la muda kuamua.

Ndugai atasalia kuwa kiongozi aliyebeba majukumu ya Bunge kwa uzito mkubwa. Uongozi wake ulitoa somo kuhusu uwajibikaji wa viongozi, nafasi ya Bunge kama muhimili wa dola na haja ya kuwa na mjadala wa wazi kuhusu hatima ya uchumi na siasa za Tanzania. Historia itamkumbuka kama kiongozi aliyethubutu kusema kile alichoamini, hata kama hakikupokelewa na wengi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *