TIMU za kikapu ya KIUT na DB Oratory zimezitikisa timu kongwe zinazoshiriki Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL) baada ya kuzifumua katika mechi zilizokutana wiki hii.
Ubabe wa timu kongwe za JKT na UDSM Outsiders pamoja na Srelio na Savio ulijikuta ukielea kufuatia vipigo visivyotarajiwa kutoka kwa timu hizo ambazo zinachukuliwa kuwa changa katika mashindano hayo.
KIUT iliyopanda BDL miaka ya karibuni iliifumua JKT kwa pointi 84-74 na baadaye ikaifunga UDSM Outsiders kwa pointi 64-53 – timu ambazo zimekuwapo katika michuano hiyo kwa miaka mingi.
Wakati KIUT ikizitembezea vichapo timu hizo kubwa na zenye mashabiki wengi, DR Oratory iliifunga Srelio kwa pointi 76-72 kisha ikaichapa Savio kwa pointi 75-60.
Kocha wa KIUT, Denis Funganoti alisema ushindi wanaopata katika ligi hiyo unatokana na mipango waliyojiwekea ya kufanya vizuri mwaka huuna kwamba, walijiandaa mapema vizuri kipindi cha mapumziko.
“Tulikuwa tunabezwa sana kutokana na uchanga wa timu ya KIUT. Nachosema tutapambana na timu yoyote tutakayocheza nayo,” alisema Funganoti huku mmoja wa mastaa wa timu hiyo, Adam Michael akisema ushindi huo unachangia pia na maboresho waliyokuwa wanafanya katika michezo ya mwanzo.
“Kwa kweli zoezi la kurekebisha makosa lilifanikiwa. Tulibadilika na timu zote kwa sasa zimeanza kutuhofia,” alisema Michael.
Hata hivyo, akizungumza baadaye baada ya Srelio kuifunga Mgulani JKT kwa pointi 107-64, kocha wa timu hiyo, Miyasi Nyamoko alisema watapambana kuhakikisha kwamba wanacheza hatua ya nane bora ya mashindano hayo msimu huu.
“Timu ilikuwa inabezwa na kila mtu. Nachosema kwa sasa tutakuja kushangaza na watu watakuja kutufahamu ligi itakapomalizika,” alitamba Nyamoko.
Katika mchezo huo Srelio iliongoza robo zote nne kwa pointi 30-9, 27-20, 28-16 na 22-4 ambapo mchezaji Junior Louissi wa timu hiyo alifunga pointi 30 akifuatiwa na Mussa Mwakalobo aliyetupia 15 ilhali pia Louisisi ambaye ni raia wa Gabon aliongoza kwa kudaka mipira ya rebound mara 13.
Kwa upande wa Mgulani JKT, Yassin Shabani alifunga pointi 40 kati ya pointi hizo alifunga eneo la mtupo mmoja ‘three pointi’ 21 akifuatiwa Dotto Zephanie aliyefunga 10.
WAKALI WA ASISTI
Wakati ushindani kwa timu za wanawake ukizidi kushika kasi katika Ligi ya Mpira wa Kikapu wa Wanawake Mkoa wa Dar es Salaam (WBDL), upande wa asisti Noela Uwendameno wa Jeshi Stars anaongoza kwa kutoa asisti 34.
Mwaka jana, Noela aliyechezea Vijana Queens mwaka huu ameonyesha kiwango bora akiwa na timu mpya, huku Juliana Sambwe wa Tausi Royals anayecheza kama namba 1 (Pointi Guard) akishika nafasi ya pili kwa kutoa asisti 31 akifuatiwa na Jesca Lenga (DB Troncatt 28), Tumaini Ndossi (Tausi Royals 22) na Elina Sinamenga (Twalipo Queens 22).
Kwa upande wa kupora mipira (steal) Sambwe anaongoza kwa kunyakua mara 14 akifuatiwa na Salma Sandali (Vijana Queens 9), Elina Sinamengo (Twalipo Queens 8), Mahewa Matema (Tausi Royals 8) na Noela Uwendameno (Vijana Queens 8).
Steal ni neno linalotumika baada ya mchezaji kunyakua mpira kutoka kwa mpinzani wake bila kumfanyia madhambi.
Kwenye ribound anayeongoza ni Taudencia Katumbi kutoka DB Lioness aliyedaka mara 74 akifuatiwa na Jackline Mgaiwa (City Queens 57), Marshallet Shimbweche (Reel Dream 53), Anamary Cyplian (Jeshi Stars 48) na Nadjima Manji wa Ukonga Queens mara 45.
NGISAISE ANATUPIA TU WBDL
Mchezaji Jesca Ngisaise wa JKT Stars anaongoza kwa kufunga pointi 62 katika mchezo mmoja wa WBDL pale JKT ilipoifunga Mgulani Stars kwa pointi 121-23.
Mbali ufungaji wa pointi hizo pia alifunga 60 katika dhidi ya UDSM Queens ambapo JKT ilishinda kwa pointi 109-26, vilevile alitupia pointi 23 dhidi ya DB Troncatti katika ushindi wa pointi 61-51 akifuatiwa na Taudencia Katumbi wa DB Lioness aliyefunga 55.
Pointi hizo alifunga dhidi ya Kurasini Divas katika mchezo ambao Lioness ilishinda kwa pointi 112-24, huku akifunga pointi 48 dhidi ya Mgulani Stars ambapo walishinda kwa pointi 98-38 na pia alifunga pointi 35 dhidi ya Kigamboni Queens pale Lioness iliposhinda 81-39.