
Maafande wa JKT Tanzania wakiwa uwanja wa nyumbani wa Meja Jenerali Isamuhyo, imeinyoosha Mbeya Kwanza kwa mabao 3-0 na kukata tiketi ya hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho (FA).
JKT ilitumia dakika 20 za kwanza kupata mabao hayo na kuitupa nje Mbeya Kwanza inayoshiriki Ligi ya Championship katika mchezo huo uliopigwa jioni hii jijini Dar es Salaam.
Ibrahim Ngecha alikuwa wa kwanza kuitanguliza JKT inayoshiriki Ligi Kuu kwa bao la dakika ya 10 kabla ya Edward Songo kufunga mengine mawili dakika ya 14 na 17 na kuwakatisha tamaa wageni ambao walionyesha soka la upinzani, lakini walizidiwa maarifa.
Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko ya wachezaji na kuongeza kasi ya mchezo, lakini ni wageni walioonekana kuimarika zaidi na kuwabana wenyeji kiasi dakika 45 za pili zikimalizika bila kuongezwa bao na kuaga michuano hiyo kwa mabao 3-0.
Hadi kufika hatua hiyo, JKT ilianza kuing’oa Igunga United kwa mabao 5-1 hatua ya 64 Bora kisha katika 32 Bora ikapata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Biashara United, wakati Mbeya Kwanza ilianza mechi za 64 Bora kwa kuifunga Mabao FC 2-1 kisha kuizima Mambali Ushirikino kwa 3-0.
Katika mechi nyingine iliyopigwa jijini Mbeya, wenyeji Mbeya City waliiduwaza Mtibwa Sugar kwa kuwachapa kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Sokoine na kutangulia robo fainali.
Riffat Khamis aliitanguliza Mbeya City dakika ya 35 kwa mkwaju wa penalti kisha nahodha Eliud Ambokile akaongeza jingine pia kwa penalti sekunde chache kabla ya mapumziko kabla ya Omar Marungu kufunga bao la kufutia machozi la Mtibwa dakika ya 75.
Mtibwa wamewahi kulitwaa kombe hilo linalotoa tiketi ya CAF mwaka 2018, kwa sasa ndio vinara wa Ligi ya Championship ikipambana kurudi Ligi Kuu iliyoshuka msimu uliopita.
Nayo Singida Black Stars imefuzu robo fainali ikiiondosha KMC kwa bao 1-0 KMC katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Tanzanite Kwaraa mkoani Manyara.
Singida Black Stars imefuzu robo fainali kufuatia bao la kujifunga kipindi cha kwanza kupitia nyota wa KMC, Abdallah Said ‘Lanso’.