JKT Tanzania yaipeleka Simba Mkwakwani Tanga

Dar es Salaam. JKT Tanzania imepanga kucheza mechi yake ya Ligi Kuu dhidi ya Simba, Mei 5, 2025 katika Uwanja wa Mkwakwani Tanga badala ya Uwanja wake wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni Dar es Salaam.

Uamuzi wa JKT Tanzania kupeleka mechi hiyo katika Uwanja wa Mkwakwani umechukuliwa baada ya kufungwa kwa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo kwa ajili ya kufanyiwa ukarabati wa mwisho kuupa utayari wa kutumika kwa ajili ya mazoezi ya timu zitakazoshiriki Fainali za Mataifa ya Afrika wa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN) 2025 mwezi Agosti mwaka huu.

Chanzo cha uhakika kimeithibitishia Mwananchi Digital kuwa tayari JKT Tanzania imeshachagua Uwanja wa Mkwakwani baada ya kuambiwa kufanya hivyo na pua timu yao ya wanawake ya JKT Queens huenda ikacheza mechi yao ya Ligi Kuu dhidi ya Simba Queens katika Uwanja wa Manungu Complex, Turiani Morogoro.

“Uwanja kwa sasa umeanza kufanyiwa ukarabati wa mwisho kwa ajili ya CHAN hivyo mechi yetu ya nyumbani dhidi ya Simba tutacheza Tanga katika Uwanja wa Mkwakwani maana ndio upo karibu na timu yetu ya wanawake inaweza kuchezea Uwanja wa Manungu,” kilifichua chanzo hicho.

Mtendaji mkuu wa JKT Tanzania, Jemedari Said amekiri kuwa ni kweli Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo umeanza kufanyiwa ukarabati ingawa bado uamuzi wa wapi watacheza mechi zao zilizobakia nyumbani haujafanyika.

“Ni kweli serikali imetutaarifu kuwa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo unapaswa kufanyiwa huo ukarabati ambao umeshaanza wa kuweka taa na vitu vingine ambavyo vinahitajika hivyo kwa sasa maombi ya kutumia uwanja mwingine yapo kwenye ‘process’ (mchakato).

“Hii ni kwa mechi zetu mbili zilizobakia kwenye Ligi Kuu za nyumbani ambazo ni dhidi ya Simba na Fountain Gate,” amesema Jemedari.

Jemedari amesisitiza kuwa hamu yao ni kuutumia Uwanja huo kwa mechi mbili za nyumbani lakini dharura hiyo imewalazimisha kusaka uwanja mwingine.

“Hili jambo ni la dharura lakini kama serikali ikaamua tumalizie hizo mechi hapo tunatamani iwe hivyo maana sisi tunatamani kucheza katika uwanja wetu wa nyumbani. Hatufanyi eti kwa sababu kuna kanuni inayoturuhusu kucheza mechi mbili kwenye viwanja vingine bali hili ni jambo la dharura na jambo lenyewe ni la kitaifa lazima tuheshimu mamlaka,” amesisitiza Jemedari.

Uamuzi huo umekuja siku chache baada ya uongozi wa KMC kuamua kupelekea mechi yake ya Ligi Kuu dhidi ya Simba, Mei 11, 2025 katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora badala ya Uwanja wake wa nyumbani wa KMC Complex, Mwenge Dar es Salaam.

Ofisa habari wa KMC, Khalid Chukuchuku alisema kuwa sababu mbili ndizo zimewafanya waamue hivyo.

“Siku mbili baada ya kucheza na Simba, tutakuwa na mechi ya ugenini dhidi ya Tabora United katika Uwanja huohuo wa Ali Hassan Mwinyi hivyo benchi la ufundi limeshauri tukacheze hiyo mechi ili wachezaji wasichoshwe na safari.

“Lakini sababu ya pili ni kwamba kanuni zinaturuhusu kufanya hivyo na hii sio mara ya kwanza kitu kama hicho kufanyika,” amesema Chukuchuku.

Kanuni ya 9(7) ya Ligi Kuu 2024/2025, kila timu inaruhusiwa kucheza mechi zake mbili za nyumbani katika uwanja uliopo katika mkoa tofauti na kituo ilipo.

“Timu ya Ligi Kuu inaweza kuteua viwanja vingine miongoni mwa viwanja

vilivyokaguliwa na kukidhi vigezo vya kikanuni kutumika kwa michezo ya Ligi Kuu kwa michezo yake miwili tu ya nyumbani na kuwasilisha Uteuzi wake huo siku ishirini na moja (21) kabla ya mchezo husika inayokusudia kucheza kwenye uwanja wa uteuzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *