JKT Tanzania, Mbeya City zakata tiketi ya robo fainali Shirikisho

MAAFANDE w JKT Tanzania ikiwa uwanja wa nyumbani wa Meja Jenerali Isamuhyo, imeinyoosha Mbeya Kwanza kwa mabao 3-0 na kukata tiketi ya hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho.

JKT ilitumia dakika 20 za kwanza kupata mabao hayo na kuitupa nje Mbeya Kwanza inayoshiriki Ligi ya Championship katika mchezo huo uliopigwa jioni hii jijini Dar es Salaam.

Ibrahim Ngecha aliitanguliza JKT inayoshiriki Ligi Kuu baada ya kujifunga katika harakati za kuokoa hatari dakika ya 10 kabla ya Edward Songo kufunga mengine mawili dakika ya 14 na 17 na kuwakatisha tamaa wageni walionyesha soka la upinzani, lakini walizidi maarifa na nyota wa JKT.

Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko ya wachezaji na kuongeza kasi ya mchezo, lakini ni wageni walioonekana kuimarika zaidi na kuwabana wenyeji kiasi dakika 45 za pili zilimalizika bila kuongezwa idadi ya mabao na kuaga michuano hiyo kwa mabao 3-0.

Hadi kufika hatua hiyo, JKT ilianza kuing’oa Igunga United kwa mabao 5-1 hatua ya 64 Bora kisha katika 32 Bora ikapata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Biashara United, wakati Mbeya Kwanza ilianza mechi za 64 Bora kwa kuifunga Mabao FC kwa mabao 2-1 kisha kuizima Mambali Ushirikino kwa 3-0.

Katika mechi nyingine iliyopigwa jijini Mbeya, wenyeji Mbeya City waliiduwaza Mtibwa Sugar kwa kuwachapa kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Sokoine na kutangulia robo fainali.

Riffat Khamis aliitanguliza Mbeya City dakika ya 35 kwa mkwaju wa penalti kisha nahodha Elius Ambokile akaongeza jingine pia kwa penalti sekunde chache kabla ya mapumziko kabla ya Omar Marungu kufunga bao la kufutia machozi la Mtibwa dakika ya 75.

Mtibwa wamewahi kulitwaa kombe hilo la Shirikisho linalotoka tiketi ya CAF mwaka 2018 kwea sasa ndio vinara wa Ligi ya Championship ikipambana kutaka kurudi Ligi Kuu iliyoshuka msimu uliopita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *