JKT, Singida BS ni vita ya rekodi

Rekodi ya JKT Tanzania kuwa timu pekee kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu ambayo haijapoteza mechi nyumbani itaendelea kudumu? Hilo ni swali wanalojiuliza wengi wakati Wanajeshi hao wa Kujenga Taifa watakapowakaribisha Singida Black Stars.

Ni katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopangwa kuchezwa kuanzia saa 10 jioni leo Alhamisi kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo Mbweni, Dar es Salaam.

JKT Tanzania inashikilia rekodi hiyo baada ya kucheza mechi nane, imeshinda tatu na sare tano, mara ya mwisho imetoka kuizuia Yanga ikipata matokeo ya 0-0.

Licha ya kwamba JKT Tanzania ina rekodi bora ya kutopoteza nyumbani, lakini wastani wa ukusanyaji pointi unawakataa kutokana na kuwa timu ya 10 kwenye msimamo wa matokeo ya nyumbani ikiwa na pointi 14 pekee huku mechi tatu za mwisho uwanjani hapo ikitoka 0-0 zote dhidi ya Pamba Jiji, Mashujaa na Yanga.

JKT Tanzania katika pointi zao 20, sita imezipata uwanja wa ugenini ikiifunga Fountain Gate, huku ikitoka sare na Singida Black Stars, Kagera Sugar na Namungo. Mchezo wa leo, Singida Black Stars ina wakati wa kujiuliza kwani haina matokeo mazuri kwenye mechi mbili zilizopita baada ya kutoka sare ya 2-2 nyumbani na kufungwa 2-0 na KMC ugenini.

Kaimu Kocha Mkuu wa Singida Black Stars, David Ouma, ana kazi ya ziada kukiandaa kikosi chake na mbinu bora za ushindi huku akiwategemea nyota wake wa eneo la ushambuliaji wakiongozwa na Jonathan Sowah ambaye ni usajili mpya aliyeanza kwa kufunga mechi ya kwanza dhidi ya Kagera.

Mbali na Sowah, kuna Elvis Rupia, mshambuliaji mwenye mabao nane ambapo anapambana kurudi kileleni mwa chati ya wafungaji akizidiwa bao moja na Clement Mzize wa Yanga, huku akiwa sawa na nyota wawili wa Simba, Leonel Ateba na Jean Charles Ahoua.

“Mechi dhidi ya KMC na Kagera kuna vitu nimeviona kwenye timu, hayo nimeyabaini kutokana na aina ya wapinzani tuliokutana nao, tunakwenda kucheza na timu ambayo nayo ni ngumu hivyo lazima tuwe bora kukabiliana nao.

“Tumejifunza mambo mengi kutoka mechi zilizopita, kuelekea kuikabili JKT tumewaona walivyocheza na Yanga, kuna mbinu tofauti tutazitumia kusaka matokeo mazuri.

“Ukiangalia katika ligi zipo zinazowania ubingwa, pia zinazotaka kupanda nafasi kutoka kule chini, hivyo tunafahamu tunatakiwa kwenda kuchezaje ili kufikia malengo,” amesema kocha Ouma kuhusu anavyokwenda kuikabili JKT Tanzania.

Mchezo wa leo unaongezwa ugumu na matokeo ya duru la kwanza pale ambapo timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Liti mkoani Singida. Rupia aliitanguliza Singida kwa bao la dakika ya 14 lililotokana na beki na kipa wa JKT Tanzania kujichanganya kwenda kuokoa krosi ya Ibrahim Imoro na kujikuta wakimpa nafasi mfungaji kumalizia kirahisi, kabla ya beki Wilson Nangu kuisawazishia JKT Tanzania dakika ya 67 akiunganisha kwa kichwa krosi ya Shiza Kichuya.

Kocha wa JKT Tanzania, Ahmad Ally, amesema baada ya kumalizana na Yanga, anawakaribisha Singida akiamini wanakwenda kucheza mchezo mwingine mzuri na mgumu.

Kocha huyo ameongeza kwamba kwake kucheza dhidi ya timu ngumu na zenye wachezaji wengi wazoefu kuliko kikosi chake inampa wakati mzuri wa kukua katika ufundishaji wake.

“Tunakwenda kucheza mchezo mzuri baada ya kumaliza salama mchezo uliopita, tumekuwa na siku moja ya kurudisha utimamu wa mwili, leo (jana) tunamalizia programu ya mwisho kabla ya kucheza kesho (leo).

“Cha msingi ni kuwaheshimu wapinzani, kuangalia ubora wao unauzuiaje na udhaifu wao tunautumiaje. “Singida ni timu nzuri, ina wachezaji wengi wazuri wenye mwendelezo mzuri na malengo yao ya kumaliza nafasi bora zaidi kwenye msimamo, tunawaheshimu, ni mchezo muhimu unaohitaji kupata matokeo mazuri kila upande.

“Tunahitaji kuwa wamoja kuhakikisha tunafanikisha malengo yetu, bila ya umoja sidhani kama tunaweza kufanikisha malengo.

“Kukutana na timu kubwa zilizopo nne bora ni nzuri kwa sababu inanifanya kuwa bora zaidi kila wakati, ili uwe bora ni lazima ukutane na walio bora zaidi,” amesema kocha huyo.

Katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, JKT Tanzania inashika nafasi ya 10 ikiwa na pointi 20, wakati Singida inazo 34 ikishika nafasi ya nne, zote zikicheza mechi 18.