JKT Queens yatangulia fainali ngao jamii wanawake kitemi

Nusu fainali ya kwanza ya ngao ya jamii kwa wanawake imetamatika leo Oktoba 2 huku JKT Queens ikitangulia fainali baada ya kuichakaza Ceasiaa Queens mabao 7-0 Uwanja wa KMC Complex.

JKT Queens ilianza kupata bao dakika ya 20 ya mchezo likifungwa na Winifrida Gerald, Yasinta Mitoga dakika ya 44, Anastazia Katunzi 45 na hat-trick ya Stumai Abdallah aliyefunga 45, 46 na 65 na 87 Janet Matulanga yaliyozamisha matumaini ya Ceasiaa Queens kusonga hatua ya fainali.

Ni mara ya pili kwa JKT kama isemavyo kauli mbiu yao ya Kichapo cha Kizalendo kugawa dozi ya mabao mengi kwani msimu uliopita ilikutana na Fountain Gate Princess ambayo msimu huu imemaliza nafasi ya tano ikapata ushindi wa mabao 5-0.

Matokeo hayo yanawafanya Wanajeshi hao wa kike kutangulia fainali ambayo inatarajiwa kuchezwa Oktoba 05 uwanjani hapo.

Hii ni mara ya pili kwa Shirikisho la Soka nchini (TFF) kuleta michuano hiyo kwa wanawake tangu ilipochezwa msimu uliopita na Simba Queens ikichukua ubingwa kwa kuitoa JKT kwa mikwaju ya penati 5-4 dakika 90 zikitamatika kwa sare ya 1-1.