JKT Queens yaivua Simba Ubingwa WPL

JKT Queens yaivua Simba Ubingwa WPL

JKT Queens imefanikiwa kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) baada ya kuishushia kipigo cha mabao 5-0 timu ya Gets Program katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Major General Isamuhyo.

Mabao ya JKT Queens yamefungwa na Annastazia Katunzi ambaye aliandika bao la uongozi kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya tisa huku Stumai Abdallah akifunga la pili katika dakika ya 24’ kabla ya Winifrida Gerald kufunga mawili akiingia kwenye nyavu katika dakika ya 31, na 68 wakati Janeth Mutulanga akiitimisha kwa kufunga bao la tano katika dakika ya 87.

Katika mchezo wa leo, JKT walitakiwa kupata angalau ushindi wa aina yoyote ili kubeba taji hilo ambalo wamelikosa kwa mwaka mmoja tangu walipolitwaa mwaka 2023. JKT na Simba zimelingana alama zikiwa na 47 kila mmoja ila JKT Queens imeweza kutwaa taji hilo kwa tofauti ya mabao ya kufungwa na kufunga.

Kwa upande wa Simba Queens ambao ndiyo walikuwa wapinzani wa karibu wa JKT Queens, walikuwa na nafasi finyu ya kulitetea taji lao kwani walitakiwa kushinda dhidi ya Alliance Girls huku ikiombea JKT Queens ipoteze au kutoka sare dhidi ya Gets Program jambo ambalo limeonekana kuwa gumu licha ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 ugenini dhidi ya Alliance Girls.

JKT Queens sasa wamefikia idadi ya mataji manne sawa na waliokuwanayo Simba Queens. Mara ya mwisho JKT ilibeba taji hilo ilikuwa mwaka 2023 huku mengine ikiyachukua mwaka 2027 na 2018.

Mabingwa waliopita

Rekodi za mabingwa wa Ligi Kuu Wanawake zinaonyesha hivi; Mlandizi Queens (2017), JKT Queens (2017/2018), JKT Queens (2018/2019), Simba Queens (2019/2020), Simba Queens (2020/2021), Simba Queens (2021/2022), JKT Queens (2022/2023) na Simba Queens (2023/2024).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *