JKT Morogoro kugawa chakula kwenye vikosi vingine

Morogoro. Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kikosi 837 KJ Chita mkoani Morogoro wameanzisha skimu ya umwagiliaji lengo ni kuepuka kilimo cha kutegemea mvua ambazo wakati mwingine hazitabiriki.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa JKT Meja General Rajabu Mabele, leo Jumanne Machi 25,2025 alipotembelea kikosi hicho kinachofanya kilimo cha kimkakati kwa mazao ya mpunga na ufugaji wa samaki.

Amesema matumaini ya JKT ni kuzalisha chakula cha kutosha kwa ajili ya kugawa kwa vikosi vingine na kuongeza uzalishaji.

“Katika mkakati huu Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (Sua) wamekuwa wakiwaleta vijana wao katika maeneo yetu wakijifunza na kutupa sisi elimu zaidi ya namna gani ya kupata mazao zaidi,” amesema General Mabele.

Hata hivyo baadhi ya wahitimu wa mafunzo hayo akiwepo Monica Michael amesema anaona yakienda kubadilisha maisha yake kiuchumi kwani kwa sasa ana ujuzi wa ufugaji wa samaki kwa tija.

“JKT tunajifunza mambo mengi licha ya kuwa wakakamavu na nidhamu kwa kila mtu ila hapa tunapata ujuzi, hivyo jamii ilete ndugu zao kujifunza mengi ya kizalendo”. amesema Monica

Kamanda wa kikosi hicho, Kanali Ashiraf Hassan, amesema eneo hilo lenye ekari 14 linatumika kuleta faida kwa jeshi kwani ni mradi maalumu wa kilimo na ufugaji samaki unaosaidia kulisha Mkoa wa  Morogoro na maeneo mengine yenye uhitaji.

“Kikosi hicho kinajihusisha zaidi na ulimaji wa mpunga kwa kutumia skimu ya umwagiliaji inayosaidia kufanya kilimo hicho katika majira yote ya mwaka” amesema Kanal Hassan

Amesema kwa upande wa ufugaji wao ni salama kwani hawatumii vitu vyovyote vyenye viashiria vya sumu, ambavyo vinaweza kuhatarisha maisha ya watumiaji

Kanali Hassan amewataka wadau mbalimbali pamoja na vijana wanaotoka mashuleni wanaotaka kujifunza kwa vitendo kujitokeza kwa wingi ili wapate mafunzo hayo yenye tija.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *