
Dar es Salaam. Baada ya Nenda Kamwambie kufanya vizuri. Diamond akanunua pikipiki aina ya Vespa. Pikipiki hizi maarufu sana Unguja na Pemba. Akawa anapigia misele yake.
Mambo yalipoenda vizuri aliachana na usafiri huo wa Vespa. Akanunua gari kuu kuu aina ya Toyota Celica. Gari hii aliuziwa na mtangazaji wa televisheni, Ben Kinyaiya.
Ndo gari iliyotumika katika video ya Mbagala. Kuna shot ikimuonesha kaka yake Rommy Jones. Akishusha mguu toka ndani ya gari hiyo akiwa amevaa viatu vyekundu.
Shoo ya kwanza Diamond kulipwa akiwa chini ya Aljazeerah, ilikuwa Morogoro. Kampuni ya Aljazeera chini ya Papa Misifa ililipwa shilingi laki tano tu. Mwanzo mgumu.
Ikafuata shoo ya Mbagala. Walipewa pande na Dj Nelly. Shoo ilikuwa ya majonzi sana. Kwani ukumbini hawakuzidi watu kumi pamoja na wale wa bure. Usione vyaelea.
Ilikuwa shoo ya hasara kweli. Lakini pamoja na yote hayo, baada ya shoo Diamond alibaki akicheka na kusema: “Dah imetupiga kweli!” Hakuonekana kukata tamaa. ‘Hasla’!
Mtafute Diamond wa leo. Hapo Mbagala hakuna eneo la yeye kufanya shoo maana itakuwa maafa. Mondi wa leo ni wa shoo za viwanja vikubwa. Maisha ni safari.