JIONGEZE: Kabla ya Cheka Tu na Watubaki

Dar es Salaam. Kulikuwa na Pwagu na Pwaguzi. Hii ilibamba sana pale Pugu Road Radio Tanzania. Ni katika utawala wa Mzee Jangala na Mzee Jongo. Nyakati hizo walikuwa mastaa wakubwa sana.

Akaja King Majuto na Mzee Small. Hao nao walikimbiza sana na sanaa ya maonesho. Kwenye kampeni na ‘promosheni’ ya bidhaa mbalimbali. Uliza watu nyakati zao ilikuwa balaa.

Wakaibuka Max na Zembwela. Katika wakati wao hawa nao walikuwa noma sana. Nani hakujua muungano wao hawa wahuni wa mjini? Kuanzia Migo, Manzese mpaka Hedaru.

Wakaibuka Joti na Mpoki. Na hawa pia walitesa nyakati zao. Hapo kabla ya Ze Comedi. Tunaongelea Joti na Mpoki wa Mambo Hayo. Enzi za kina Aisha na Waridi, Bishanga na Rich. 

Katika zama hizo wakaibuka Bambo na Kingwendu. Wakateka soko na kuwafunika Joti na Mpoki. Dunia ya Bongo Fleva, dansi na magazeti ya udaku. Kwa pamoja viliwapa ukubwa sana.

Baadaye kidogo wakaja Mzee Pembe na Senga. Kiumri walikuwa wakubwa na sanaa walianza kitambo. Lakini ule umoja wao ulikuja baadaye sana. Na wakadumu zaidi kabla ya umauti kumkuta Mzee Pembe.

Kwa sasa ‘bato’ la wachekeshaji siyo kwa msanii mmoja mmoja. Bali sasa imekuwa kwa kambi na kambi. Dunia ya sasa ya ‘uchekeshaji’ imetekwa na Cheka Tu na Watu Baki. Wanatupa burudani. Ni wakati wao.