

Chanzo cha picha, Alamy
Duma ni maarufu kwa kuwa mnyama wa nchi kavu mwenye kasi zaidi – lakini utafiti unapendekeza kuna mengi kwa jinsi wanavyokimbia zaidi tu ya kasi.
Fikiria wewe ni swara, unayekimbia katika eneo la savana huko Afrika kujaribu kumtoroka duma – mnyama wa nchi kavu mwenye kasi zaidi duniani, ambaye anaweza kufikia kasi ya kukimbia ya zaidi ya kilomita 100 kwa saa (62 mph).
Inaweza kuonekana kama juhudi ambazo haziwezi kuzaa matunda, lakini katika maisha halisi, swara wakati mwingine hufanikiwa kutoroka duma.
Je, unadhani ni mkakati gani wa kukimbia unaweza kukupa nafasi nzuri ya kumshinda duma?
A. Kukimbia kwa haraka na kwa kufuata mstari moja kwa moja
B. Kukimbia kwa haraka na zigizagi
C. Kukimbia polepole na kwa kufuata mstari moja kwa moja
D. Kukimbia polepole na zigizagi
Utafiti kuhusu duma na mawindo yao sio tu unaonyesha jibu la chemsha bongo hii – lakini pia unatoa maarifa mapana zaidi kwa nini hasa duma wana kasi ya haraka mno, na kile tunachoweza kujifunza kutoka kwao ili kusaidia wanariadha wetu.
Alan Wilson, profesa wa masuala ya kibayolojia huko Royal Veterinary College, Chuo Kikuu cha London, Uingereza, na timu yake wameangazia kwa kina jinsi duma anavyokimbia.
Wametumia kifaa maalum kufuatilia na kupima kasi na mienendo yake.
Pia wamechukua picha za mnyama huyo wakati ndege ikiwa kwenye anga, na kuchunguza misuli ya duma waliokufa. Ugunduzi mmoja muhimu sana, kulingana na Wilson, ni kwamba utendaji wao katika kukimbia ni zaidi ya kasi.
“Unamtazama duma na kufikiria, ‘kuna mnyama ambaye ameibuka kuwa mkimbiaji bora mwenye kasi mno duniani’,” anasema. “Lakini sivyo, ni mbinu anazotumia, na miondoko yake inayotokea kwa haraka sana.”

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika utafiti wa mwaka 2013 uliochapishwa katika jarida la Nature, Wilson na timu yake waliwawekea vifaa vya kuwafuatilia duma watatu wa kike na wa kiume wawili nchini Botswana ili kukusanya data kuhusu mbio walizokimbia 367 kwa zaidi ya miezi 17.
Data hiyo ilithibitisha kwamba duma wana kasi ya ajabu: kasi ya juu kabisa iliyorekodiwa ilikuwa kilomita 93 kwa saa (58 mph, au 25.9 m/s). Kwa kulinganisha, kasi ya juu iliyofikiwa na binadamu ni 12.32 m/s, ambayo ilifikiwa na Usain Bolt katika Mashindano ya Dunia ya Berlin ya 2009 katika riadha.
Hakuna shaka, basi, kama duma wangeshiriki katika Michezo ya Paris mwaka huu, wangeshinda dhahabu.
Kwa hakika, uwindaji mwingi uliofuatiliwa ulihusisha tu kasi ya wastani – lakini ulionyesha ujanja mwingi, kama vile kuongeza kasi, kupunguza mwendo, na kugeuka kwa haraka sana.
Duma, ambao mara nyingi walikuwa wakiwinda swara, waliongeza na kupunguza kasi mara mbili ya uwezo wa farasi aina ya polo, na waliongeza kasi zaidi kuliko mbwa wa kuwinda mwanzoni mwa mbio, kulingana na utafiti huo.
Umbo lao linachangia pakubwa katika hili, kwa mfano, misuli yao ya nyuma yenye nguvu ikiwasaidia kuongeza kasi.
“Duma wana misuli,” Wilson anasema. “Watu hutazama duma katika mbuga ya wanyama na huona aina ya safu ya pande mbili, lakini duma mwitu haonekani hivyo. Duma mwitu ana misuli zaidi kidogo. Imejitokeza zaidi kuliko ya mbwa wa kuwinda. Wana miguu mikubwa, mabega makubwa, misuli mingi yenye nguvu – hiyo ni sehemu muhimu ya kuwa mnyama mwenye kasi zaidi.”
Misuli hii yenye nguvu inasaidiwa na vipengele vingine muhimu vya mwili, vinavyowawezesha kusonga mbele kutoka chini haraka sana, pamoja na kugeuka, anaongeza.
“Wana makucha yasiyoweza kurejeshwa ndani.” Anazungumzia kwa kifupi jinsi hayo yote huletwa pamoja wakati duma anapowinda:
“Misuli hufanya kazi haraka na kwa nguvu, hivyo, anaweza kuongeza na kupunga kasi, miguu ina nguvu na anaweza kutumia nguvu kubwa na kuelekea kwingine, mwili wake unabadilika-badilika kwa urahisi… unaweza kujipinda na unaweza kuegemea upande mmoja”. Hata mkia husaidia: duma huuzungusha kutoka upande mmoja hadi mwingine kufanya mwili wake uwe juu juu, akitumia mkia kama kifaa cha kukabiliana na uzito wake wakati anageuka kwa haraka sana.

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika utafiti baadaye, uliochapishwa mnamo mwaka 2018, Wilson na timu yake walifuatilia mienendo ya wale wanaowinda, kwa kuweka kifaa maalum kwenye duma na swara, na, kwa simba na pundamilia.
Waligundua kuwa duma na swara walikuwa na mbio zaidi kuliko simba na pundamilia katika suala la kasi, mwenendo na kugeuka, kulingana na data kutoka kwa duma watano, swara saba, simba tisa na pundamilia saba, waliofuatiliwa zaidi ya mara mia wakati wanakimbia.
Hata hivyo, kwa kila mnyama mwindaji, alikuwa na mbio zaidi kuliko anayewindwa. Hasa, wanyama wanaowinda walikuwa na misuli yenye nguvu zaidi na uwezo mkubwa wa kuongeza na kupunguza kasi kuliko wanyama wanaowinda.
Wilson anasema kwamba kama ilivyoa ada, swara na mawindo wengine wanakabiliwa na takriban 50% ya uwezekano wa kufa na wanyama wanaowinda, na 50% ya kufa kwa sababu zingine.
Ufafanuzi mpana wa duma ni muhimu linapokuja suala la ujuzi kwa binadamu, anaongeza Wilson, ambaye ni mwanariadha: “Nadhani ukizungumzia kuhusu mchezo wa binadamu – ni ujumuishaji wa mazoezi mchanganyiko ambayo yatakuwezesha kuwa na kasi nzuri ya kukimbia”.
Kwa wale wanaotaka kuanza kujitosa kwenye riadha, anapendekeza kuchukulia riadha kama ustadi unaoweza kujifunza, na kuongeza nguvu kwa mazoezi ya hali ya juu kama vile kukimbia umbali mfupi, kisha kutembea, kukimbia tena, na kuongeza umbali zaidi kadiri muda unavyokwenda.
“Kadiri muda unavyokwenda, mwili utabadilika kutokana na mazoezi makali” katika suala la kukuza uimara wa mifupa, misuli na viungo, anasema Wilson, na kuna uwezekano mdogo wa kusababisha majeraha.

Chanzo cha picha, Getty Images
Na vipi kuhusu mkakati bora kwa wale swara wanaofuatiliwa na duma katika chemsha bongo mwanzoni mwa makala haya?
“Zigi zagi ni nzuri,” Wilson anasema. “Usichotaka kufanya ni kuwa katika hali ambayo duma atakulenga moja kwa moja,” ambayo inaweza kutokea ikiwa utageuka mapema sana. Badala yake, chaguo bora zaidi ni kutumia kasi ya duma dhidi yake, na kugeuka duma akiwa karibu, kwa mwendo wa kukwepa.
“Wakati mwindaji anapokupata, na ukapunguza kasi na kugeuka ghafla, na mwindaji akapita mbele yako, ni vigumu sana kurejea kukulenga tenai. Na ukweli ni kwamba, karibu theluthi moja ya swara hufanikiwa kutoroka – licha ya ukimbiaji bora wa duma.
D ndio jibu sahihi: polepole na zigi zagi. Ambayo ni sawa kwa sisi ambao hatutawahi kufikia kasi ya duma, au ya mwanariadha wa mbio za Olimpiki, lakini tunafurahia na kuvutiwa na miendendo yao tukiwa maeneo salama.