Jinsi ya kushinda hamu ya kuvuta sigara, shisha baada ya kuacha

Dar es Salaam. Miongoni mwa watu wanaopata wakati mgumu kuacha uraibu ni pamoja na wavutaji wa sigara na shisha.

Wavutaji maarufu wa sigara duniani wamewahi kukiri kuwa, wasingethubutu kujiingiza katika tabia ya uvutaji kama wangekuwa na uwezo wa kurudisha muda wao nyuma.

Uvutaji wa sigara na shisha unachochea mazingira hatarishi ya magonjwa ya moyo, saratani ya mapafu, kifua kikuu, saratani ya damu na pia kupoteza nguvu za jinsia hususani kwa wanaume.

Tafiti zinaonesha kuwa zaidi ya nusu ya wavutaji wa sigara wanakufa mapema kwa magonjwa hayo.

Kwa mujibu wa mtandao wa Dailymail wa Uingereza, wakati mambo yanakuwa magumu na hamu inakuwa kali, ni muhimu kukumbuka sababu zilizomfanya aanze safari hiyo.

Hakuna uraibu ambao ni rahisi kuacha. Wavutaji wengi hupata hamu ya kuvuta shisha au sigara baada ya kuacha, na baadhi yao hata hurudi tena, hasa wasipokuwa na mfumo mzuri wa msaada. Lakini, kwa kujitolea na mazingira yanayosaidia, kuna njia za kushinda hali hii kama ifuatavyo;

Epuka vichocheo

Kuna mambo fulani yanayoweza kuchochea hamu ya sigara, kwa hivyo ni muhimu kuyaepuka. Ikiwa umezoea kuvuta shisha kwenye nyumba za starehe punguza kuhudhuria huko. Au sigara baada ya chakula cha jioni, jaribu kula chumba tofauti. Ikiwa unavuta sigara unapokunywa kahawa, badilisha na chai.

Wakati mwingine, kichocheo ni kampuni unayoshirikiana nayo. Je, unahisi hamu ya sigara ukiwa peke yako na huna shughuli? Tembea au jihusishe na familia, majirani na marafiki wasiovuta sigara.

Pia, ni muhimu kuepuka maeneo ambapo watu wanavuta sigara. Epuka maeneo kama baa unazopenda kwa muda au kushirikiana na marafiki tofauti.

Simamisha fikira

Unapopata hamu ya kuvuta sigara, usikubali mara moja. Jiambie unaweza kusubiri dakika tano au hata 10. Kisha jitafutie shughuli nyingine. Tembea, pigia rafiki simu au soma kitabu. Lengo ni kuondoa mawazo yako kutoka kwa sigara, hata kwa muda mfupi.

Baadhi ya mbinu za kiakili kama vile mawazo yanayoongozwa ikiwamo kudhibiti msongo wa mawazo. Mbinu hizi zinaweza kusaidia akili yako kusafiri na kupunguza hamu hiyo.

Tafuta kitu cha kutafuna

Hamu ya kuvuta sigara wakati mwingine hutokana na kuchoka, kwa hivyo ni vyema kuwa na kitu kingine cha kutafuna, kama vile bazoka au pipi vinaweza kusaidia kupunguza hamu ya sigara au shisha.

Pia, unaweza kutafuna vitu kama karoti au kuandaa saladi yenye mboga mbalimbali.

Tafuta mfumo wa usaidizi

Zungumza na marafiki na familia yako kuhusu uamuzi wako wa kuacha kuvuta sigara au shisha na uwaombe msaada wao.

Msaada kutoka kwa marafiki na familia ni muhimu hasa katika kusaidia kujenga mazingira yasiyochochea hamu ya sigara nyumbani. Baadhi ya marafiki au ndugu zako wanaovuta sigara pia wanaweza kuhamasika na kujiunga nawe katika safari hii.

Zaidi ya hayo, kuna jumuiya nyingi za mtandaoni na majukwaa zinazoweza kutoa msaada na ushauri kutoka kwa watu waliopitia hali kama yako.

Kumbuka sababu zilizokufanya uache

Wakati mambo yanakuwa magumu na hamu inakuwa kali, ni muhimu kukumbuka kwa nini ulianza safari hii.

Andika sababu zako za kuacha kwenye kipande cha karatasi au simu yako na uzisome unapopata hamu ya shisha au sigara. Hii itakukumbusha malengo yako na kukupa motisha ya kuendelea kuacha. Kuhesabu siku ambazo umekaa bila kuvuta sigara au shisha pia ni motisha kubwa.

Imeandikwa Herieth Makwetta na Mashirika