Jinsi Kauli ya ‘kulambishwa asali’ inavyowatesa wanasiasa

Dar es Salaam. ‘Kulambishwa asali’ ni msemo unaobamba siku hizi mitaani na hata kwenye mitandao ya kijamii, lakini msemo huo unawalenga zaidi wanasiasa, hususan viongozi au waliokuwa viongozi ndani ya vyama vya siasa.

Wengi hutafsiri msemo huo kama kupokea kitu kwa siri, kama vile fedha, ahadi ya cheo, au zawadi yenye thamani, ili kunyamazishwa na kuacha kuzungumzia masuala nyeti.

Ingawa msemo huu mara nyingi huonekana kama fursa, baadhi ya watu wameeleza wazi maumivu yao kutokana na matumizi yake. Mfano ni Freeman Mbowe, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chadema, ambaye kwa nyakati tofauti alieleza hisia zake kuhusu kauli hiyo.

Mbowe alidai kuwa kauli hizo zililenga kudhoofisha morali yake, huku akisisitiza kuwa katika utumishi wake wa miaka 30 ndani ya Chadema, hakuna kashfa iliyomuathiri kama tuhuma kwamba “amelambishwa asali.” Msemo huu ulianza kutumika kama fimbo dhidi yake baada ya kuonekana kuwa na ushirikiano wa karibu na Serikali, jambo lililoibua hisia tofauti miongoni mwa wanachama wa chama chake.

Msemo huo pia umetajwa kumhusu Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi, ambaye baadhi ya watu wanamtuhumu eti huenda naye kalambishwa asali, kisa ni kule kuwa karibu na Serikali.

Hivi karibuni alipokuwa akihutubia sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Sheria duniani, alikanusha madai hayo kwa kusisitiza kuwa ushirikiano wa TLS na Serikali hauwezi kutafsiriwa kama ‘kulamba asali.’

“Tunaposhirikiana na Serikali hatulambi asali, kwa sababu tunapata changamoto ya watu kuhisi hivyo. TLS ni bodi ya kisheria, itaonya kwa haki, itapongeza kwa haki na kushiriki katika kujenga taifa kwa maslahi ya Watanzania,” alisema Mwabukusi.

Mtazamo wa wachambuzi
Hata hivyo, wachambuzi wanahoji kuwa mabadiliko ya kauli na misimamo, kushindwa kushikilia misingi ya utetezi wao, pamoja na kubadilika kutoka lugha kali hadi laini, ni mambo yanayoibua hisia miongoni mwa jamii kuwa mtu ‘amelambishwa asali.’

Mchambuzi wa masuala ya kijamii, Dk Faraja Kristomus ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), anasema kauli ambazo watu hutumia wanapokuwa kwenye harakati za kupigania haki, mara nyingi huwasaliti wanapoanza kushirikiana na serikali.

“Wanapokuwa kwenye harakati, hutumia sauti zenye misimamo mikali wakiahidi hawawezi kubadilika wala kununuliwa. Wananchi ni wepesi wa kufuatilia kuona kama misimamo hiyo inabaki ileile kabla na baada ya wao kushika nafasi fulani,” anasema.

Dk Kristomus anasema jamii huangalia namna wanavyosimamia misimamo yao baada ya kuchaguliwa au kupata nafasi ya ushawishi, mara nyingi lugha wanayotumia katika kampeni huwajengea imani kwa wananchi. “Wananchi waliwachagua kutokana na harakati zao na wanatarajia waendelee na misimamo hiyo hata baada ya kupata nafasi. Wakiona mabadiliko, huanza kusema kuwa mtu amelambishwa asali,” anasema mchambuzi huyo.

Dk Kristomus anabainisha kuwa mara nyingine mabadiliko hayo hutokana na wao wenyewe kuchagua ni masuala yapi ya kuyasimamia na jinsi ya kuzungumza wanapokuwa na viongozi wa Serikali.

“Ni kama vile wanapoteza ukali wao wanapokaribiana na Serikali. Wananchi hawaoni tena ule msimamo waliokuwa nao kabla, na kauli zao zinapokuwa laini wanaposhirikiana na viongozi wa Serikali, watu huanza kuhisi kuwa wameshawishiwa kulegeza misimamo yao,” anasema.

Anatoa mfano wa Boniface Mwabukusi, aliyewahi kuwa mwanaharakati, akisema kuwa wakati huo watu walivutiwa naye na wakamchagua kuongoza TLS kwa sababu ya msimamo wake mkali. Hata hivyo, baada ya kuchukua nafasi hiyo, jamii ilitarajia kuona akiendelea kukemea mambo kwa nguvu ileile. Aidha, anasema athari za mabadiliko haya ni kuwavunja moyo wananchi waliokuwa na matumaini kwa viongozi wao, hali inayofanya watu waamini kuwa Serikali ni taasisi kubwa isiyoweza kuguswa.

Mkurugenzi wa Kituo cha Utetezi wa Mtandao wa Haki za Binadamu nchini (THRDC), Onesmo Olengurumwa, anasema baadhi ya watetezi wa haki wanapokaribiana na Serikali hukosa mwelekeo na kusahau majukumu yao ya msingi.

“Kuna wengine wanapopata nafasi ya kukaa meza moja na viongozi wa Serikali, wanatoka hapo wakiwa wamesahau kabisa wajibu wao wa kukemea na kupinga mambo yasiyo sahihi. Hii ni changamoto kubwa,” anasema.

Olengurumwa anasisitiza, kuwa karibu na serikali hakumaanishi kushindwa kukosoa au kupigania haki za binadamu.
Anasema ni muhimu kwa watetezi kujifunza namna ya kutekeleza majukumu yao huku wakiendelea kuwa na uhusiano mzuri na serikali. “Inawezekana kufanya vyote kwa wakati mmoja. Kuna nyakati inahitajika kukaa pamoja na serikali kwa mazungumzo, lakini hiyo haimaanishi uadui.

Tunapaswa kuiwajibisha serikali kwa hoja na wakati huo huo kushirikiana kwa maendeleo ya haki za binadamu,” anaeleza.

Akitoa mfano wa Boniface Mwabukusi, anasema kabla ya kuwa Rais wa TLS, alikuwa huru kuzungumza kwa uhuru bila kufuata taratibu za taasisi. Hata hivyo, baada ya kuingia katika taasisi rasmi, anakabiliwa na misingi, miiko na taratibu zinazomlazimu kushirikiana na Serikali kwa namna fulani.

“Alivyokuwa nje ya taasisi, hakuwa na mipaka. Sasa yupo kwenye taasisi yenye mfumo rasmi wa utendaji unaohusiana moja kwa moja na serikali, hivyo lazima afuate utaratibu wa taasisi hiyo,” anasema.
 

Kwa upande mwingine, kuhusu Freeman Mbowe, anasema haikuwa rahisi kwake kubadilika ghafla kwa sababu kama mwanasiasa alikuwa na mtazamo wa siasa za mrengo wa kati. “Si rahisi kumlazimisha mwanasiasa wa mrengo wa kati kuwa na siasa kali.

Watu wanapaswa kuelewa hilo. Kila mtazamo wa kisiasa una faida na changamoto zake,” anasema.
Olengurumwa anaongeza kuwa ni muhimu kwa vyama vya siasa kuwa na watu wa mitazamo tofauti ili kudumisha usawa.

“Kuwa na chama chenye mtazamo mmoja pekee si jambo jema. Vyama vinapokuwa na mitazamo tofauti, vinasaidia kuleta mizania. Na kuhusu utetezi, si lazima iwe vita au uadui, kwa sababu hata anayekosolewa ndiye unayepaswa kuzungumza naye ili kupatikane suluhisho,” anaeleza.
Anasisitiza kuwa hata mabadiliko makubwa kama Katiba Mpya lazima yapitie serikalini, hivyo utetezi bora ni ule unaochanganya ukosoaji, ushauri, na mazungumzo bila kuharibu mahusiano muhimu.

Mhadhiri Mwandamizi wa Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda, anaeleza kuwa jamii imepoteza imani na mifumo ya utawala kwa sababu serikali mara nyingi hutumia kila mbinu kujitetea dhidi ya tuhuma mbalimbali.

“Wale wanaojitokeza kuzungumzia changamoto wanapata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa jamii. Hata hivyo, mtu anayekosoa akionekana kuwa karibu na Serikali, watu huanza kuwa na mashaka,” anasema.

Mbunda anaongeza kuwa wanaharakati huru ni wachache na mara nyingi sauti zao hupokelewa vizuri na wananchi, lakini mifumo ya utawala hujitahidi kuwakaribisha na kuwashawishi.
“Mifumo inapokosa kuaminika, inakuwa tatizo kwa sababu wananchi wanapoteza imani kwa viongozi wao. Wanaharakati wanapaswa kuwa wepesi kufafanua hali halisi kwa jamii ili iondokane na mashaka yasiyo ya lazima,” anahitimisha.

Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya siasa, Bubelwa Kaiza anasema wananchi mara nyingi huwa na matarajio makubwa kutoka kwa viongozi na wanaharakati. Wanaposhindwa kutimiza matarajio hayo, jamii huanza kupoteza imani nao.
“Wananchi wanapomchagua mtu kama mwakilishi wao, wanatarajia atasimamia masuala waliyoamini atapigania,” anasema Kaiza.

Kwa mujibu wa Loisulie Paul, dunia inabadilika na harakati za kidiplomasia zinakuwa na nafasi kubwa katika kufanikisha mabadiliko, lakini changamoto ni kwamba nchi nyingi za Afrika, ikiwemo Tanzania, bado hazijazoea mabadiliko hayo.

“Historia inaonesha mtu kuwa na msimamo mkali pekee si rahisi kufanikisha mabadiliko. Mara nyingi serikali hutumia mbinu mbalimbali kujilinda na kujitetea. Mfumo wa 4R (Reconciliation, Resilience, Reforms, and Rebuilding) ni mzuri katika kufanikisha malengo,” anasema.

Anasema wanaharakati wanapaswa kuelewa kuwa msimamo mkali unahitaji uvumilivu mkubwa, lakini wengi hujikuta njiapanda kwa sababu wanapaswa pia kufikiria familia zao na hatari zinazoweza kuwapata.

“Mabadiliko ya kweli yanahitaji ushiriki wa kubadilisha sheria na sera kandamizi kwa njia za kidiplomasia. Kama tunahitaji msimamo mkali, basi tunapaswa kuwa tayari kupoteza wanaharakati wengi njiani, jambo linaloweza kuchelewesha mafanikio,” anasema.

Mkurugenzi wa THRDC, Olengurumwa anasisitiza kuwa watu waliopo kwenye taasisi za utetezi wana majukumu makubwa yanayohusisha kushauri, kusaidia na kushirikiana na serikali ili kufanikisha mabadiliko.

“Huwezi kubadili sheria bila kushirikiana na waziri mwenye dhamana. Kuwa karibu na serikali wakati mwingine haikwepeki kwa sababu taasisi zetu zinasimamiwa na serikali. Ili kupata matokeo chanya, tunapaswa kuwa na ushirikiano wa karibu, lakini bila kupoteza misingi ya utetezi wa haki za binadamu,” anasema.