
Geita. Upande wa mashtaka katika kesi inayowakabili washtakiwa wanne wanaodaiwa kumuua Joyce Ludeheka kwa kumkata na kitu chenye ncha kali kisha kukata sehemu yake ya siri na kuikausha, umeieleza mahakama namna kaburi lilivyofukuliwa na kuchukua sampuli kwa ajili ya vipimo vya vinasaba.
Kesi hiyo iliyopo Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Geita, mashahidi wanne wametoa ushahidi kwa kueleza namna sampuli zilivyochukuliwa hadi kusafirishwa kwenda ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi.
Kesi hiyo ya mauaji namba 29820 ya mwaka 2024 inasikilizwa na hakimu mwenye mamlaka ya nyongeza Fredrick Lukuna.
Watuhumiwa kwenye kesi hiyo ni Mateso Joseph, Thereza Luhedeka, Dogani Budeba na Lucas Elias wakazi wa Mbogwe mkoani Geita ambao wanadaiwa kutenda tukio hilo Oktoba 11, 2025 katika Kijiji cha Ikobe wilayani Mbogwe mkoani Geita.
Washtakiwa hao wanadaiwa kumuua Joyce Ludeheka ambaye ni mdogo wa Thereza Ludeheka waliokuwa na mgogoro wa ardhi.
Kwa mujibu wa mashtaka, sehemu ya siri inayodaiwa kukatwa kwa marehemu ilikutwa nyumbani kwa mshtakiwa wanne Lukas Elias.
Shahidi wa 10 katika kesi hiyo ambaye ni Mkuu wa Upelelezi Kituo cha Polisi Masumbwe, Frank Fredrick ameileza mahakama namna walivyokwenda kufukua kaburi la Joyce Ludeheka na kuchukua sampuli kwa ajili ya uchunguzi.
Fredrick ameiambia mahakama kuwa wakiwa wameambatana na daktari, askari kwa kushirikiana na wananchi walifukua kaburi na kuutoa mwili wa Joyce kisha daktari akachukua sampulu kutoka kwenye mwili huo.
Shahidi huyo ameleza kuwa daktari alichukua sehemu za nywele, kipande cha nyama kutoka kwenye unyayo wa mguu na kipande cha nyama kutoka kwenye sehemu ya uke wa marehemu.
“Sampuli hizo tulizichukua kwa lengo la kwenda kufanya uchunguzi ili kujua uke uliokutwa kwa mmoja wa washtakiwa ni wa Joyce au la na baada ya kuchukua tulisaini fomu ya makabidhiano mimi na daktari aliyechukua sampuli,” amesema Fredrick.
Shahidi wa 11 ambaye ni daktari, John Masule naye ameieleza mahakama namna alivyochukua sampuli kwenye mwili wa marehemu na kuwakabidhi polisi kwa ajili ya kupeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi wa vina saba.
Pia, shahidi wa 13 ambaye ni mhudumu katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Kituo cha Afya Masumbwe naye ameieleza mahakama nama alivyopokea sampuli ambazo ni nywele, kipande cha nyama kutoka kwenye unyayo wa mguu pamoja na kipande cha nyama kutoka kwenye sehemu za siri wa mwili wa binadamu na kuhifadhi kwenye chumba cha kuhifadhi maiti.
Kwa upande wake Lucy Kessy ambaye ni shahidi wa 14, akiwa kwenye ofisi ya maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Kanda ya Ziwa ameieleza mahakama namna alivyopelekewa sampuli A na B kutoka Wilaya ya Mbogwe na askari aliyemtaja kwa jina moja la Alex.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi kesho upande wa mashtaka utakapoendelea na ushahidi wake