Jinsi Bunge lilivyopitisha bajeti Wizara ya Maji

Dodoma. Bunge limepitisha bajeti ya Wizara ya Maji kwa mwaka 2025/26 likitumia takribani dakika 10.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso jana Mei 8, 2025 aliliomba Bunge kuidhinisha Sh1.01 trilioni kwa ajili ya wizara hiyo, kati ya hizo Sh943.11 bilioni ni kwa ajili ya miradi maendeleo.

Katika mwaka 2024/25 Bunge liliidhinisha Sh627.78 bilioni kwa ajili ya Wizara ya Maji, Sh558.11 bilioni zikienda katika miradi ya maendeleo.

Kabla ya kupitishwa bajeti hiyo leo Mei 9, 2025, Mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga alitangaza mchangiaji atakayefuata kuchangia hoja baada ya Mbunge wa Kyerwa, Innocent Bilakwate ni mbunge wa viti maalumu, Zaytun Swai.

Hata hivyo, baada ya Bilakwate kumaliza kuchangia aliingia Naibu Spika wa Bunge, Musa Zungu aliyemtaka Naibu Waziri wa Maji, Kundo Mathew kuchangia hoja hiyo kwa dakika tatu.

Kundo alimshukuru Zungu kwa kumpatia fursa hiyo ili aweze kuongea mawili au matatu.

“Wabunge wameongea, Bunge limeongea maana yake Watanzania wameongea na kikubwa zaidi wamepongeza kazi kubwa iliyofanyika,” amesema.

Kundu alianza kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan na wananchi wa Bariadi jimboni kwake na Waziri Aweso, kabla ya kuhitimisha Zungu alimkata kauli, hivyo akaketi.

Baadaye Aweso alihitimisha hoja akiwshukuru wabunge waliochangia akieleza wachangiaji watapewa majibu kwa njia ya maandishi ili kuhakikisha wanaweka kumbukumbu.

“Ila kubwa niungane na wabunge kwa dhati ya moyo kumpongeza na kumshukuru Rais Samia, niseme ndio suluhu ya matatizo ya Watanzania hasa katika kumtua mama ndoo kichwani,” amesema.

Akiendelea kuzungumza, Zungu alimtaka waziri kutoa hoja kwa wabunge na alifanya hivyo.

Bunge liliketi kama kamati ya Bunge zima kupitia kifungu kwa kifungu cha hoja hiyo.

Zungu alisema hakuwa amepata majina ya wabunge wenye hoja katika fungu hilo ambalo lina mshahara wa waziri, hivyo alihoji Bunge kama linakubaliana na kupitishwa kwa kifungu hicho.

Mafungu mengine yalipitishwa na wabunge na kuhitimisha mchakato huo ndani ya dakika 10.

Baada ya bajeti kupitishwa, Zungu amempongeza Aweso na timu yake kwa kufanyia kazi na kupokea maelekezo ya Rais Samia.

“Nakumbuka tulipokuwa Same (Mkoa wa Kilimanjaro) Rais (Samia) alikusaluti, wewe na timu yako hongereni sana kwa kweli mnajitahidi na mmeleta mabadiliko makubwa, lakini niwaombe mwendelee kutazama maeneo ya mjini Dar es Salaam pale kuna shida ya maji,” amesema.

Baada ya bajeti hiyo kupitishwa kwa mtindo wachap chap’, ilifahamika kuwa Waziri Aweso amefiwa na mdogo wake Babu Ali, aliyeongozana na wanafamilia wengine kumsindikiza Dodoma kuwasilisha bajeti bungeni.

Ndani ya Ukumbi wa Bunge, Spika Dk Tulia Ackson Aprili 8, 2025 aliwatambulisha wanafamilia wa ASweso, kila mtu kwa jina lake na Ali alisimama akionekana mwenye furaha kama ilivyokuwa kwa ndugu wengine.

Baada ya tukio hilo, kila mmoja alikwenda kujipumzisha akiwemo Ali aliyefikia katika moja ya hoteli jijini Dodoma.

Akizungumza kwa niaba ya familia, msemaji katika msiba huo, Rashid Shangazi amesema hakuna aliyejua na anayejua hadi sasa nini chanzo cha kifo cha ndugu yao.

Shangazi ambaye ni Katibu wa Wabunge wa CCM, amesema leo Ijumaa Mei 9, 2025 ndipo walipogundua amefariki dunia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *