
Ofisi ya Vyombo vya Habari vya Serikali ya Ukanda wa Ghaza imetangaza kuwa, wanajeshi makatili wa Israel wameua shahidi zaidi ya raia 2,000 kaskazini mwa ukanda huo baada ya utawala huo ghasibu kuanzisha kampeni ya kuangamiza kabisa kila kitu cha eneo hilo tangu siku 38 zilizopita.
Ismail al-Thawabta, Mkuu wa Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Serikali ya Ghaza amesema hayo na kuongeza kuwa, wengi wa wanaouawa katika hujuma inayoendelea ya Israel ni watoto, wanawake na vizee.
Aidha amelaani vikali jinai nyingine za Israel akisisitiza kuwa, Wazayuni wanaendesha kampeni ya kuwaangamiza Wapalestina wengi huko Ghaza kadiri wanavyoweza, hasa kaskazini mwa ukanda huo. Ametoa mwito kwa jamii ya kimataifa kuingilia kati mara moja na kusimamisha vita na mauaji ya halaiki yanayofanywa na utawala wa kigaidi wa Israel dhidi ya Wapalestina.
Thawabta pia amezilaumu Marekani, Uingereza na nchi kadhaa za Ulaya kutokana na kuhusika kwao moja kwa moja na jinai zinazoendelea kufanywa utawala wa kigaidi wa Israel huko Ghaza akizilaani pia kwa kushiriki katika jinai ya kuwaua kwa njaa wakazi wa Ghaza.
Mwezi uliopita wa Oktoba, utawala wa Kizayuni ulianzisha kampeni ya kuangamiza kabisa kila kitu ikiwa ni pamoja na wakazi wote wa kaskazini mwa Ghaza huku maelfu ya watu wakilazimika kuhama eneo hilo wakiwemo madaktari.
Hakuna chakula chochote kilichoingia kaskazini mwa Gaza tangu wakati huo huku utawala wa Kizayuni ukiendelea kuwashambulia kinyama wananchi wa Palestina ili kuwalazimisha kuhama.