
Simiyu. Vurugu za Uchaguzi Mkuu 2025 zinazodaiwa kutokea katika Wilaya ya Meatu, mkoani Simiyu, zimemuibua Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina, anayedai kuwa jimboni kwake kuna makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wanaoendesha kampeni usiku badala ya mchana.
Ubunge wa Mpina unakoma Juni 27, mwaka huu, kama ilivyo kwa wabunge wote wa Bunge la Tanzania kwa mujibu wa Katiba. Baada ya hapo, wataingia kwenye mchakato wa kura za maoni ndani ya chama hicho ili kuwatafuta wagombea watakaokiwakilisha CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Mpina amewachongea wanaofanya vurugu kwenye jimbo lake wakati wa mkutano uliofanyika Meatu, mkoani Simiyu, jana mbele ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira, anayepita kukagua utekelezaji wa Ilani ya chama hicho.
Akizungumza huku akishangiliwa na halaiki ya makada wa chama hicho, mbunge huyo wa Kisesa amesema kuwa katika jimbo lake wamejitokeza makada wengi wanaopiga kampeni kwa madai kuwa ni watia nia nyakati za usiku.
“Wanajiita watia nia, lakini CCM ina utaratibu wa muda rasmi wa kampeni. Wanafanya kampeni usiku, mimi nikasema hizo kampeni zenu na utia nia wenu fanyeni mchana na usiku ili mpate fursa nzuri zaidi. Mimi nilishazoea mapambano,” amesema Mpina.
Katika maelezo yake, amesema kuwa amehudumu kama mbunge kwa miaka 20, amekuwa mjumbe wa kamati ya siasa kwa miaka 22 na pia amewahi kuwa mwalimu. Hivyo, amesema kuwa wanafunzi wake wanapaswa kuruhusiwa kufanya kampeni muda wote, usiku na mchana.
“Waruhusuni wafanye kampeni kwa uwazi mchana na usiku ili kuondoa malalamiko yoyote. Ninachotaka kusema ni kwamba wajumbe wangu wa Halmashauri Kuu, kazi nzuri iliyofanywa na CCM inahitaji mshikamano. Pale tutakapompata kada sahihi katika nafasi zote za udiwani na ubunge, ni muhimu tuendelee kuwa na umoja,” amesema Mpina.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Kenani Kihongosi, amesema kuwa siasa za mkoa huo ni rahisi kuliko zinavyotafsiriwa nje ya mkoa. “Nikuhakikishie (Makamu Mwenyekiti Wasira) mwaka huu hatupotezi jimbo wala kata,” amesema Kihongosi.
Hata hivyo, Kihongosi amesema kuwa mwaka huu wa uchaguzi, baadhi ya watu wanajihusisha na siasa za kuchafuana kwa kurekodi mazungumzo ya wenzao kwa maslahi binafsi.
Amesema kuwa hali hiyo isipodhibitiwa, inaweza kuchafua taswira ya chama chao huku akitoa rai kwa Wasira kusaidia kukemea tabia hizo, akisisitiza kuwa siasa ni ushindani wa hoja na si fitina au majungu.
“Siasa ni jinsi unavyoishi na jamii yako. Kama uliokota kuni na kundi la watu, utaota nao moto; kama hukuokota, basi jiandae kuondoka. Hakuna njia nyingine. Ukweli lazima usemwe,” amesema Kihongosi.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohamed, amesisitiza kuwa mkoa huo uko imara licha ya maneno yanayoendelea. “Mkoa wa Simiyu unaongozwa na vijana, hatutetereki. Meatu kumekuwa na maneno mengi yanayotumika kutengeneza ajali za kisiasa.
“Tuache kutengenezeana ajali. CCM ina utaratibu wake, inaweza kuwa na wagombea 20 lakini mmoja tu atashinda. Tusitengeneze vurugu kuelekea uchaguzi.
“Kila mtu atavuna alichopanda; kama ulifanya mema kwa wananchi, utavuna mazuri, na kama hukufanya hivyo, huwezi kuvuna. Hakuna mwenye umiliki wa kata au jimbo; kila mwanachama ana haki ya kugombea,” amesema.
Wasira atoa kauli
Akijibu Wasira amewataka wanachama wa CCM kuacha makundi yanayoweza kudhoofisha ushindi wa chama hicho katika uchaguzi huu.
Amesema kuwa upinzani unapata ushindi wakati makundi ndani ya CCM yanaposhindwa kushirikiana, hali inayosababisha wanachama kumpigia kura mpinzani.
“Tukiwa na umoja, hakuna anayeweza kutushinda, lakini makundi yanadhoofisha ushindi wetu. Kwa mfano, huko Meatu, kutokana na makundi, CCM iliwahi kupoteza jimbo kwa mgombea asiye na hata makazi jimboni, mtu aliyekuwa anakaa hotelini. Migogoro ndani ya chama ilimfanya apate kura nyingi na kushinda,” amesema Wasira.
Akiwa Bariadi, Wasira amesisitiza kuwa CCM ina kanuni za maadili zinazozingatiwa na yeye ni msimamizi wa maadili hayo.
“Wanaotaka njia za mkato kwa kugawa fedha tutawabaini. Kamati ya siasa inaweza kusema fulani anakubalika, lakini tunajiuliza, zile fedha alizosambaza mmezijua? Tuna watu wetu wanapita mtaani bila sare za CCM wakikusanya taarifa. Tunataka kuhakikisha kuwa mgombea tunayempeleka kwa wananchi ni chaguo sahihi.”
Wasira ameongeza kuwa Katiba ya Tanzania, Ibara ya 8, inatamka kuwa mamlaka yote ya dola hutoka kwa wananchi, hivyo hawawezi kupuuzwa. “Lazima tupeleke mtu sahihi kwa wananchi. Tusichague mgombea ambaye watu wanajiuliza, ‘huyu wamemtoa wapi?’”
Ameonya dhidi ya kuvuruga maadili ya uchaguzi na kusema kuwa chama cha upinzani, Chadema, kimepoteza mvuto na hakina nguvu vijijini. “Hata wakiwepo watu, ni wa kupiga kelele tu na hawawezi kushinda,” amesema.
Amesema kuwa moja ya matatizo makubwa ndani ya CCM ni makundi ambayo huendelea hata baada ya uchaguzi.
“Watu wanaposhindwa, hawakubali. Wanaendelea na makundi na chuki kwa miaka mitano. Hiyo si afya. Mtu akikosa nafasi, akubali matokeo na tuendelee mbele kwa mshikamano,” amesema Wasira.