Jiji la DSM lajivunia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa mafanikio ndani ya miaka minne ya Rais Samia madarakani

Miaka minne imepita tangu Tai­fa letu lilipoandika historia mpya ya kuwa na Amiri Jeshi Mkuu wa kwanza Mwanamke, Rais wa Jam­huri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk Samia Suluhu Hassan, ni mengi yameandikwa na mengi yameelezwa juu ya uwezo wake mkubwa wa kiu­ongozi katika awamu hii ya Sita.

Hotuba yake ya kwanza ya tarehe 22 Aprili, 2021 kwa Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, ilitosha kutoa dira ya uongozi wake na Tan­zania aitakayo, hivyo katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Mhe. Dk Samia Suluhu Hassan teyari ame­fanya mapinduzi makubwa katika sekta ya afya, elimu, maendeleo ya jamii na sekta nyengine za uzalishaji mali ikiwa ni pamoja na masuala ya biashara.

Kwa upande wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kama ilivyo Halmashauri nyengine, jukumu lake kubwa la kwanza na la kisheria ni kuhakikisha kwamba inatoa huduma zilizo bora na endelevu kwa wanan­chi wake katika sekta za msingi, hivyo ni dhahiri sasa mafanikio yameanza kuonekana kwa kila sekta, kwani Serikali anayoiongoza Rais Samia, imefanikiwa kutimiza ahadi zilizoa­hidiwa kwa wananchi kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM (2020-2025).

“Dhamira yetu ni kuhakikisha tunatekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi na kwakweli kuhakikisha kwamba maendeleo ndani ya Hal­mashauri ya Jiji la Dar es Salaam yanaonekana na yanaonekana dha­hiri,” amesema Mkurugenzi wa Hal­mashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya

Fedha kwenye miradi ya maendeleo zaongezwa

Imekua ni miaka minne yenye matokeo chanya kwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, bajeti ya halmashauri imekua ikiongezeka kila mwaka, hiyo imechagizwa na Rais Samia kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta za afya, elimu na maeneo mengine muhimu.

“Katika kuhakikisha kwamba Ilani ya Uchaguzi inatekelezwa ipasavyo, maendeleo kwenye sekta muhimu tumeyazingatia, kwa miaka minne tumeona mabadiliko makubwa na nguvu ambayo Halmashauri imewe­ka, lakini pia Mhe. Rais Dk Samia Suluhu Hassan amewekeza” amese­ma Mkurugenzi Mabelya.

Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ilipanga kukusanya Sh 202.4 bilioni, mwaka wa fedha 2022/2023 ilipanga kukusanya Sh 208.5 bilioni, mwaka wa fedha 2023/2024 ilipanga kukusanya Sh 255 bilioni na mwaka 2024/2025 imepanga kukusanya Sh 280 bilioni.

“Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa miaka minne kumekua na ongezeko kubwa la ukusanyaji wa mapato na hivyo kupelekea utekelez­aji wa miradi mbalimbali ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwenda kwa kasi lakini kwa uhaki­ka kwamba fedha za utekelezaji wa miradi hiyo zipo” alisema Mkuru­genzi Mabelya.

Mabelya aliendelea kufafanua “Kwa mwaka huu tunaoendelea nao wa 2024/2025 hadi sasa tumefikia asilimia 83 ya makusanyo maana yake mpaka tutakapofika mwisho mwa mwaka tunatarajia tutakwenda mbali zaidi, kwa hiyo hii ni katika eneo la utekelezaji wa mpango na bajeti ya Halmashauri yetu kwa kip­indi cha hii miaka minne, inaonesha kuna ongezeko kubwa na sehemu kubwa ya ongezeko hili imekua ni kwa ajili ya kwenda kutatua kero zilizopo kwa wananchi wetu katika maeneo ya miundombinu ya utoaji wa huduma za msingi, hivyo tuna jukumu la kumshukuru Rais Samia.”

Aidha, Mkurugenzi Mabelya ame­sema “Sisi Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam tumejipanga vyema kuhakikisha tunakua na miradi mikubwa ya kimkakati ambayo ina­fadhiliwa na mapato ya ndani ya Hal­mashauri ya Jiji la Dar es Salaam kama nilivyosema uwezo wa kuku­sanya ni mkubwa na hivyo tumejikita na kujielekeza katika kuhakikisha tunakua na miradi ya kielelezo au miradi ya kimkakati ndani ya Hal­mashauri ya Jiji la Dar es Salaam.”

Mapinduzi katika sekta ya afya

Tangu alipoingia madarakani, Rais Samia ameonesha miujiza mikubwa katika sekta ya afya kwa kuzinga­tia kuwa afya ni zaidi ya rasilima­li muhimu kwenye maisha ya kila mmoja wetu na ustawi wa Taifa, hivyo Rais Samia ameendelea kufan­ya jitihada mbalimbali ili kupambana na adui maradhi.

“Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kila unapojaribu kuongelea bado hujapata mfano wake wa kumuonge­lea, kwa kipindi cha miaka minne hii Jiji la Dar es Salaam imekua ni faraja na furaha kubwa sana, Idara ya Afya imepokea kiasi cha fedha Sh 101.4 bil­ioni kutoka Mapato ya ndani ya Hal­mashauri, Serikali Kuu na Wafadhili kwa ajili ya ujenzi wa vituo vipya vya afya, zahanati na hospitali pamoja na ununuzi wa dawa na vifaa tiba” ame­sema Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Dk Zaitun Hamza.

Kupitia mapato yake ya ndani, Idara ya Afya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kipindi cha miaka minne imepata kiasi cha Sh 35.4 bil­ioni ikiwa ni pamoja fedha za ujenzi wa Hospitali tatu za kila jimbo.

Aidha, kwa fedha za Serikali Kuu, Idara ya Afya imetekeleza miradi mbalimbali, ambapo kiasi cha Sh 5.2 bilioni kimegharamia ujenzi wa vituo vya afya vinne ambavyo ni Segerea, Mchikichini, Guluka Kwalala na Kipunguni ‘B’ lakini pia ujenzi wa wodi tatu, majengo manne ya upa­suaji, wodi ya upasuaji wanawake na wanaume na jengo la kuhifadhia maiti, ujenzi mwengine ni wa jengo la dharura, ujenzi wa vyumba vya kujifungulia akina Mama Gongolam­boto, Bangulo, Zahanati ya Nzasa na Luhanga

“Mhe. Rais yeye ametimiza wajibu wake, kile kipande ambacho Mwe­nyezi Mungu amemkatia katika hii Dunia ambapo ni Tanzania kuhakiki­sha analeta faraja na matumaini kwa watanzania kuwapelekea huduma za afya karibu na wananchi wake waweze kupata muda mchache wa kupata huduma na waweze kuende­lea na shughuli zao za Maendeleo,” ameeleza Dk Zaituni Hamza.

Lakini pia Idara ya Afya imetumia kiasi cha Sh 17.5 bilioni kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa vituo vya afya ambavyo ni Mzinga, Mchikichini, Kiwalani, Kinyerezi, Zingiziwa na Majohe, ujenzi wa jengo la macho na meno Kivule, jengo la bima na kuon­geza ghorofa moja kituo cha mnazi mmoja.

Haijaishia hapo, huwezi kujenga tu bila ya kuweka dawa na vifaa tiba, katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa Rais Samia, ameweza kutoa fedha zaidi ya Sh 42.9 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba “haijawahi kutokea, ndani ya hii miaka minne, fedha zimekua ziki­shushwa ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, kwa hiyo ni kitu kikubwa sana cha kujivunia kwa maana kwamba hakujenga tu, lakini dawa na vifaa tiba vimeletwa,” Dk Zaituni Hamza.

“Kama mlivyoona katika program ya mama ya ‘M-Mama’ sasa tunak­wenda kuboresha mfumo mzima wa ‘referral system’ kwa ajili ya kumuo­koa mama na mtoto wake, kwa maana kwamba kupata ujauzito siyo sababu ya mama kwenda kufariki, kwa hiyo kuna mafanikio makubwa sana” amefafanua Dk Zaituni Hamza.

Kwenye eneo la uboreshaji wa miundombinu ya kutolea huduma, Rais Samia ameimarisha miundom­binu ya kutolea huduma za dharura kwenye Hospitali ya EMD iliyopo Ukonga Magereza “Mhe. Rais amet­uletea vifaa kwa ajili ya huduma za dharura kwenye hospitali ya EMD ambayo ipo Ukonga Magereza, kwa hiyo ukiangalia kwenye kuboresha huduma Mhe. Rais amejitahidi sana kwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam,” amesema Dk Zaituni.

Halkadhalika, Serikali pia imewekeza kwa kiwango kikubwa katika eneo la huduma za uchunguzi ambapo imeshajenga jengo la x-ray kituo cha afya cha Pugu “Uwekezaji huu umewezesha upatikanaji wa huduma za uchunguzi karibu zaidi na wananchi ambapo hapo awali huduma za uchunguzi. zilikuwa zinapatikana katika Hospitali kama vile Amana na Mnazi Mmoja, hivyo kuwalazimu wagonjwa kutumia gharama kubwa kufuata huduma,” amesema Dk Zaituni.

Mapinduzi katika sekta ya elimu

Ndani ya miaka minne ya Uon­gozi wa Rais Samia, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeshuhudia maboresho makubwa katika sekta ya elimu kulingana na azma yake ya kuhakikisha elimu inakuwa ni kicho­cheo kikubwa cha maendeleo kwa kutoa wahitimu wenye ujuzi na stadi.

Elimu ya awali na msingi

Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kupitia Div­isheni ya Elimu ya Awali na Msingi, imeweza kupokea fedha za ujenzi wa vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo, nyumba za walimu, ujenzi wa ofisi za walimu, ujenzi wa shule mpya pamoja na utengenezaji wa madawati na vifaa vya kujifunzia na kufundishia kutoka Serikali Kuu, wafadhili wa elimu na mapato ya ndani ya Halmashauri.

“Tumepokea zaidi ya Sh 20.5 bil­ioni katika kipindi cha miaka minne, fedha hizi zimetoka Serikali Kuu, wafadhili pamoja na mapato ya ndani, kwa hiyo tunamshukuru sana Mhe. Rais kwa kutuwezesha kupata fedha zote hizi ambazo zimetuweze­sha kujenga vyumba vya madarasa 437 ambavyo wanafunzi wemeweza kuingia na kupata huduma ya kuso­ma kirahisi” Mwl. Magreth Macha, Afisa Elimu Awali na Msingi, Jiji la Dar es Salaam.

“Halkadhalika kwa kipindi hiki cha miaka minne tumeweza kupata fedha ya ruzuku ya uendeshaji kiasi cha Sh 7.8 bilioni kwa ajili ya posho ya madaraka, chakula cha wanafun­zi wenye mahitaji maalumu, fedha ya uendeshaji utawala, ununuzi wa vifaa, mitihani na shughuli za miche­zo” amesema Mwalimu Macha.

“Lakini pia Halmashauri yetu ya Jiji la Dar es Salaam kupi­tia mapato yake ya ndani tumewe­za kutengeneza madawati 31,539 ambayo yana thamani ya Sh 3.9 bil­ioni ambayo tumeyasambaza katika shule zetu zote zile ambazo zina upungufu wa madawati” aliongeza Mwl. Macha

Aidha, katika kipindi hiki cha mia­ka minne Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeweza kujenga shule mpya 12 zenye jumla ya Sh 3.3 bil­ioni kwa hiyo kwa kipindi hiki cha miaka minne Halmashauri imekua na mafanikio makubwa sana, shule hizi zimejengwa kupitia mapato ya ndani, lakini na fedha kutoka Serikali Kuu, fedha zilizotoka Serikali Kuu ni kwa ajili ya miradi mitatu ya BOOST, LENS na EP4R.

Kupitia mradi wa kuboresha elimu ya awali na msingi (BOOST) Serikali imejenga shule mpya nne ambazo ni Shule ya Msingi Mshikamano, Kifuru Mpya, Mnyamani na Mzizima, kwaa­jili ya kuboresha mazingira ya kujif­unzia na miundombinu

“Lakini pia tunazo shule nyengine ambazo tumejenga, nazo ni Zogoali, Nguvu mpya, Mizengo Pinda, Guluka kwalala, Taliani, Kipera na Mwem­be ambazo zimejengwa kwa fedha za mapato ya ndani na zimesaidia wanafunzi kwenda shule kwa urahisi na hizi ni huduma ambazo tumez­isogeza kwa wananchi ili wananchi waweze kupata huduma kwa urahisi, watoto wao wasitembee mbali” ame­sema Mwalimu Macha.

Kwa upande wa ukarabati wa vyumba vya madarasa, Halmashauri kupitia mapato yake ya ndani ime­peleka fedha za kutosha kwenye shule mbalimbali “tumepeleka Sh 540 milioni za mapato ya nda­ni, tumeweza kukarabati shule 36 ambapo tumepunguza changamoto ambazo zipo kwenye mashule, lakini bado tunaendelea kupeleka fedha,” amemalizia Mwalimu Macha.

Sambamba na hayo lakini pia kwa kipindi cha miaka minne, Hal­mashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeweza kujenga majengo saba ya utawala yenye thamani ya Sh 297.6 milioni matundu ya vyoo 1,063 yenye thamani ya Sh 2.01 bilioni ujenzi wa mabweni mawili kwa ajili ya wana­funzi wenye mahitaji maalumu, tha­mani yake ni Sh 177.6 milioni na shule tatu zinazoendelea kujengwa zenye thamani ya Sh 509.6 milioni shule hizi ni Chakenge, Mvuleni na Shule ya Bangulo Anex.

Elimu ya Sekondari

Katika kipindi cha miaka minne, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imepokea jumla ya Sh 35.5 bilioni katika Idara ya Elimu Sekondari, ambazo Sh 11.3 bilioni zimetoka Serikali Kuu na kujenga vyumba vya maadarasa 255 katika awamu ya kwanza maarufu kama fedha ya UVIKO 19 na vyumba vya madarasa 310 kwa awamu ya pili kwa maana Pochi ya Mama

“Pamoja na hayo, tumekuwa na mradi wa kuboresha elimu ya sekondari (SEQUIP) ambapo Seri­kali imetoa fedha kwa Halmashauri ili kuwezesha upatikanaji wa elimu, ikiwa ni pamoja na mazingira salama ya wasichana kupata elimu, kupitia mradi huo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeweza kujenga Shule ya Sekondari Liwiti, Gunatra na sasa ujenzi wa Shule Mpya ya Ghorofa Kitunda Relini” amesema Mwalimu Mussa Ally, Afisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

Kwa upande wa mapato ya nda­ni ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, jumla ya fedha Sh 15.5 bilioni zimeweza kutumika kujenga miun­dombinu ya madarasa, vyoo, kum­alizia maabara, kujenga majengo hasa madarasa ya ghorofa “kwa sasa tunaendelea na ujenzi wa maghorofa nane katika shule za sekondari za Mnazi Mmoja, Minazi Mirefu, Kip­unguni, Kimanga, Shule mpya ya Amani, Ilala Kasulu, Msimbazi na Liwiti, ambapo ghorofa moja lina uwezo wa kubeba madarasa 20 na matundu ya vyoo 45,” amesema Mwalimu Mussa Ally.

Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Ndugu Elihuruma Mabelya (wa pili kushoto) akimsikiliza Mganga Mkuu wa jiji, Dk Zaituni Hamza alipotembelea Hospitali ya Kivule ikiwa ni katika ziara zake za ukaguzi wa miradi kila Jumamosi. Wengine pichani ni wataalamu wa Halmashauri.

Katika kutekeleza Ilani ya CCM sura ya 3 ibara ya 80 (a-q) kwenye kuongeza fursa, ubora na manufaa kwa wakaazi, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imehakikisha kwamba maeneo yote ambayo hayakua na shule, yanakua na shule, mfano Kata ya Liwiti utakuta kuna shule kub­wa ya kisasa ambapo mpaka miun­dombinu itakapokamilika tutakuwa tumetumia jumla ya fedha Sh 3.5 bilioni kwa sasa jengo limegharimu Sh 1.8 bilioni lenye madarasa 20, matundu ya vyoo 45 pamoja na seh­emu ya lift limekamilika, kadhalika majengo yatakayofuata ni ambayo yatabeba maabara na miundombinu mingine kama vile ukumbi na jengo la utawala,” ameongeza Mwalimu Mussa Ally.

Aidha, kwa upande wa elimu bila malipo, Serikali ya awamu ya Sita imeendelea kutoka fedha kwa ajili ya kugharamia upatikanaji wa elimu kwa wanafunzi “Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kipindi cha miaka minne tumepokea fedha kiasi cha Sh 12.2 bilioni fedha zinazokuja kwa ajili ya kulipa elimu bila malipo kwa maana ya kusaidia watoto shu­leni,” amesema Mwalimu Mussa.

“Kwa upande wa vitabu, tume­kuwa tukipokea kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania na mapato ya Hal­mashauri ya Jiji la Dar es Salaam ili kuhakikisha wanafunzi wanapata vitabu vya kiada na ziada, jumla ya fedha Sh 216.2 milioni zimetumika kununua vitabu vya kiada,” amesema Mwalimu Mussa.

Ili kuhakikisha kila mtoto anasoma akiwa ameketi, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, na hili ni agizo la Serikali chini ya usimamizi wa Dkt. Samia, Rais wa Jamhuri ya Muunga­no wa Tanzania kuhakikisha kwam­ba watoto wote wanasoma wakiwa wameketi, Halmashauri imeweza kutengeneza viti na meza “kwa idara ya elimu sekondari pekee kwa mwaka 2023/2024 tumetengeneza viti na meza 17,500 na mgawanyo sawia umefanyika kwenye shule zetu ili watoto waweze kuketi. Madawati hayo yamegharimu jumla ya fedha Sh 1.4 bilioni amemalizia kwa kuse­ma Mwalimu Mussa.

Uwezeshaji wa wananchi kiuchu­mi kupitia mikopo isiyo na riba

Katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa Rais Samia, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imewajengea mazingira mazuri wananchi kupata mikopo nafuu isiyo na riba ambayo imeleta tija katika ukuaji wa uchumi kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu

“Kupitia mfuko wa asilimia 10 ya mapato ya ndani, kwa kipindi cha miaka minne (4) Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeweza kutoa kiasi cha Sh 23.5 bilioni kwa vikundi 1,465 vyeny e wanufaika 9,399 ambapo vikundi vya wanawake ni 865 vyenye wanufaika 6,075 vijana ni 428 wanu­faika 2,875 na wenye ulemavu ni 172 wanufaika 452,” amesema Francisca Makoye, Mkuu wa Idara ya Maende­leo ya Jamii, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salam.

Itakumbukwa kua Aprili, 2023 Serikali ilitoa agizo la kusimamisha utoaji wa mikopo ili kujipa muda wa kufanya maboresho ya kanuni na mwongozo wa utoaji na usimam­izi wa mikopo hii. Katika utaratibu ulioboreshwa, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ni miongoni mwa Hal­mashauri 10 za mfano katika kutoa mikopo kwa kutumia mfumo jumui­shi

“Mpaka sasa kiasi cha Shilingi Bilioni 15.3 kimetengwa na Hal­mashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwaajili ya kukopeshwa vikundi vya wanawake, vijana na walemavu mara baada ya mfumo jumuishi ambapo Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam itatoa mikopo hii kwa kushirikiana na Benki ya CRDB na Benki ya NMB. Hadi Februari, 2025 jumla ya vikundi 945 vimepokelewa katika mfumo wa WEZESHA na vipo hatua mbalim­bali za mchakato wa kupata mkopo,” amesema Makoye.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *