Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina imetangaza katika taarifa kwamba, kauli ya Waziri wa Fedha wa utawala wa Kizayuni kuhusu kuukalia kwa mabavu Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan yamewazaba kibao kingine wafanya mapatano.
Taarifa ya Jihadul-Islami imesema kutoa matamshi Bezalel Yoel Smotrich ya kuukalia kwa mabavu Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan sambamba na kufanyika mkutano wa wakuu wa nchi za Kiarabu na Kiislamu huko Riyadh, ni kiashiria cha vita kamili na visivyo na mwisho vya utawala wa kihalifu wa Israel dhidi ya taifa la Palestina.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa, maneno aliyotoa Bezalel Yoel Smotrich, kuhusiana na kunyakuliwa Ukingo wote wa Magharibi wa Mto Jordan sambamba na kufanyika kikao cha wakuu wa nchi za Kiarabu na Kiislamu mjini Riyadh, ni kiashiria cha vita kamili na vita visivyo na mwisho vya utawala wa kihalifu wa Israel dhidi ya watu wa Palestina.

Imeelezwa katika taarifa hiyo ya Jihadul-Islami kwamba matamshi ya Smotrich ni kofi jingine ambalo wamechapwa wale ambao kwa miongo kadhaa wameweka matumaini yao kwenye njia ya mazungumzo au kuanzisha uhusiano wa kawaida na maghasibu hao.
Waziri wa Fedha wa utawala wa Kizayuni ambaye anajulikana kuwa ni mpingaji wa kuasisiwa taifa huru la Palestina na kuunga mkono upanuzi wa vitongoji vya walowezi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan amedai Jumatatu ya jana kuwa mwaka 2025 ni mwaka wa Israel kuwa na mamlaka kamili katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan inaoukalia kwa mabavu.
Waziri huyo mwenye msimamo mkali wa kufurutu ada aliwahi kusema huko nyuma kuwa anapinga kuasisiwa taifa huru la Palestina na atafanya juu chini kupanua ujenzi wa vitongoji vya walowezi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kuimarisha usalama wa utawala wa Israel, kwa sababu idadi kubwa ya Waisraeli wanajua vyema kwamba kuanzishwa nchi huru ya Palestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kuhatarisha uwepo wa Israel.