
Namna ambavyo shabiki mmoja na wenzake wamejibana katika Coaster la kutoka Simiyu kuja Dar es Salaam kutazama pambano linaloitwa Dabi ya Kariakoo. Wametumia kilomita nyingi kukwepa ajali. Wanafika Dar es Salaam wanaambiwa pambano halipo.
Namna ambavyo mtu alikuwa anataka kwenda Marekani wikiendi hii iliyopita, lakini anasogeza mbele tiketi yake hadi wikiendi ijayo kwa ajili ya kutazama pambano la Simba na Yanga. Mida ya mchana anathibitishiwa na barua ya wazi ya Bodi ya Ligi pambano halitakuwepo.
Kuna wazungu watalii walitaka kushuhudia pambano hilo. Wakataka kujua inakuaje Manchester City ya Kariakoo ikicheza na Manchester United ya Kariakoo. Walishanunua tiketi, lakini mchana wakaambiwa pambano halipo.
Kwa mara nyingine tena uhuni umefanyika juzi katika pambano la Simba na Yanga. Limefutwa katika njia za ajabu tu. Waliofuta pambano ni wahuni wawili watatu ambao wamezungumza kwa simu wakiwa wamevaa suti na tai.
Hawakujali hisia za mashabiki wa soka nchini. Hawakujali biashara inayofanywa na kampuni ya Azam katika kuuza ving’amuzi vyao. Hawakujali biashara kubwa ya kubashiri inayofanywa na kampuni za ‘betting’ duniani kote.
Hawakujali kuna maelfu ya Watanzania walikuwa wameacha shughuli zao ili kujaribu kufika Temeke kuangalia pambano hilo. Hawakujali kuna huyu mtu ametoka Simiyu au Ngara kuja kushuhudia pambano hili la soka.
Unadhani haya yanakuwa maamuzi ya watu wengi? Hapana. Maamuzi ya watu wawili watatu tu ambao wamelewa na madaraka. Wamelewa na ukweli kupitia nguvu za Simba na Yanga wanaweza kufanya lolote wanalotaka hata kuahirisha pambano hili la soka.
Ujinga ni upi? Simba kuzuiwa kuingia uwanjani kufanya mazoezi siku moja kabla ya pambano lao na mtani. Wao ndio walikuwa wageni. Kanuni ilikuwa inawaruhusu hivyo. Haijawahi kutokea katika soka letu kwa mkubwa mmoja kwenda kuutembelea uwanja siku moja kabla ya mechi.
Zamani wakati huo timu zilikuwa zinawasili katika jiji la Dar es Salaam siku ya mechi. Yanga wangeweza kutokea Bagamoyo, Simba wangeweza kutokea Zanzibar. Siku hizi mambo hayo hayapo na timu uweka makazi yake hapa hapa Dar es Salaam.
Lilikuwa jambo jipya kwetu kuona Simba wanakwenda kufanya mazoezi usiku wa siku moja kabla ya pambano dhidi ya watani. Hata hivyo, kanuni ilikuwa inawabeba. Baada ya Simba kukataliwa na mabaunsa kuingia uwanjani usiku huo huo walitoa taarifa wasingecheza mechi.
Hapo ujue kuna simu mbili tatu za wavaa suti na tai zilipita. Tukirudi katika uhalisia wa kanuni nyingine ni kwamba jambo hilo halizuii mechi kufanyika ila mwenyeji alipaswa kuadhibiwa vya kutosha. Hata hivyo, adhabu ambayo ilitolewa kwa mashabiki waliosafiri kilomita nyingi kuja Dar es Salaam ni mechi isingekuwepo.
Baadaye Bodi ya Ligi ilitoa taarifa mechi ingekuwepo. Baadaye tena ikatoa taarifa mechi haitakuwepo. Hapo hapo Yanga wakaja na taarifa mechi itakuwepo. Na kweli wakapeleka timu uwanjani bila ya Ahmed Arajiga kuwepo uwanjani.
Huu ukawa mwendelezo wa uhuni mwingine baada ya ule ambao Yanga pia waliwahi kufanya kuiondoa timu uwanjani ikiwa tayari wachezaji wanapasha misuli yao moto. Kisa? Mechi ilikuwa imesogezwa mbele kwa saa nyingine mbili.
Nini kinafuata? Bodi ya Ligi itaendelea kuwa katika mikono ya Simba na Yanga. Tayari Yanga wametangaza hawatacheza pambano lolote dhidi ya Simba katika ligi ya msimu huu. Ni mwenendo wa kutunishiana misuli tu.
Tarehe itatangazwa na Yanga watasema hawatapeleka timu uwanjani. Siku itafika na tutakutana na wachezaji wa Yanga mitaani wakiwa wamevaa jeans zao. Kabla ya mwamuzi wa pambano hilo hajapuliza filimbi itatoka barua nyingine ya kuahirisha pambano hilo.
Hakuna ambaye atakuwa na nguvu ya kuipa Simba pointi tatu kwa sababu hakukuwa na mtu mwenye nguvu ya kuipa Yanga pointi tatu katika pambano la juzi. Hapa ndipo tulipofika. Wakubwa wana nguvu kubwa na bahati mbaya zaidi ni kwamba kuna wakubwa wengine wenye madaraka makubwa nchini nao ni mashabiki wakubwa wa timu hizi na wana uwezo wa kuingilia maamuzi.
Unaweza kuwalaumu watu wa Bodi ya Ligi. Unaweza kuwalaumu TFF. Lakini kumbe kuna wakati wanapata presha kubwa kutoka kwa wakubwa wasiojulikana.
Haya yote yanafanyika huku tukiwa hatuna huruma na mashabiki wa soka wanaojinyima kwa ajili ya kuhakikisha mpira wetu unasonga mbele.
Kwa mfano, taarifa ya bodi ya ligi ya kuahirisha pambano hili imeandikwa bila hata ya kuwaomba radhi mashabiki waliokuwa wametumia muda wao mwingi kwa hali na mali kujaribu kufika uwanja wa taifa kushuhudia pambano hilo.
Taarifa ya Simba kutocheza pambano pia haikubeba uzito kwa mashabiki waliojitokeza au waliokuwa mbioni kuja Temeke. Tunachukulia mambo haya kwa urahisi lakini siku moja yatakuja kutugharimu mbele ya safari.
Pambano kubwa kama hili lilipaswa kuahirishwa kwa sababu ya majanga ya asili. Iwe mafuriko, msiba mzito, na machache mengineyo.
Mechi haikupaswa kuahirishwa kwa sababu tu za kikanuni za hapa na pale.
Hizi kanuni zikivunjwa huwa zina faini zake.
Mapenzi ya watu wetu katika mpira ndiyo yametufikisha hapa tulipo. Wakenya wanatuonea wivu. Siku hizi tunafuzu kwenda Afcon vizuri tu. Timu zetu kubwa Simba na Yanga zinafanya vizuri katika mechi za kimataifa. Msingi mkubwa ni mapenzi yetu kwa mpira.
Wadhamini wameweka pesa nyingi kwa sababu ya mapenzi yetu katika mpira.
Leo tumejawa na kiburi cha kuahirisha mechi ya Simba na Yanga kihuni tu. Tunahalalisha uhuni wa wahuni wanaovaa suti na tai bila ya kujali tunaanzisha mwanzo wa kupoteza mvuto wa mpira wetu.