Iliwahi kumtokea Nasireddine Nabi. Iliwahi kuwatokea Djuma Shaban na Yannick Bangala. Unapigwa na kitu kizito usoni na haujui kimetokea wapi. Na sasa imetokea kwa Miguel Gamondi. Amepigwa na kitu kizito na wala hafahamu kilichompiga.
Watu wawili muhimu walioondoka huku wakitaka ni Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Fiston Kalala Mayele. Hao wengine niliowataja hapo juu waliondoka huku wakitamani kuendelea kuwepo Yanga. Na sasa imetokea kwa Gamondi.
Nadhani haamini namna ambavyo maisha yameenda kasi kwake. Hakuna shaka alitazamia kuwa katika benchi la Yanga dhidi ya Al Hilal ya Sudan lakini ghafla atakuwa mpenzi mtazamaji huku akitafuta timu mpya itakayompa ajira.
Nini kimetokea kwa Gamondi? Nadhani ni uamuzi mgumu wa Rais wa Yanga, Hersi Said. Ana falsafa za roho ngumu za kuchangamsha kikosi chake. Huwa anataka Yanga iwe na njaa ile ile kila siku. Gamondi alipungukiwa njaa. Huwa inatokea. Waliwahi kusema ‘kuwa namba moja sio jambo gumu bali kuendelea kuwa namba moja ni jambo gumu’. Gamondi alishindwa kushikilia bomba kisawasawa kama ambavyo Injinia alitaka.

Kwanza alipunguza njaa na timu ikapunguza njaa. Zile bao tano tano zikatoweka. Gamondi alikariri maisha. Niliandika hapa. Aliongeza starehe zake za nje ya uwanja na ndani ya uwanja alihisi maisha yamekuwa rahisi. Timu nzuri ipo. Wachezaji wapo. Wapinzani wengi hasa wa ndani walionekana kuwa rahisi.
Naambiwa kulikuwa na mambo mengi nyuma ya pazia. Ubaguzi kwa wachezaji. Kukariri kikosi. Kulikuwa na upungufu mwingi lakini jibu lake lilikuwa kwamba ‘timu inashinda’. Hata wakati kikosi chake kikionekana kutocheza vema bado jibu lake kubwa kwa waandishi wa habari lilikuwa kwamba ‘alikuwa hawafundishi wachezaji wake kufunga mabao mengi’.
Nadhani yote haya yalikuwa hayawapendezi mabosi wa Yanga wenye uamuzi, hasa Hersi. Ambacho Gamondi hakujua ni kwamba katika mpira wetu watu wenye uamuzi wanaweza kukuondoa huku ukiacha rekodi nzuri tu nyuma yako. Wakati mwingine hata mabosi huwa wanajua namna gani timu yao inashinda kando ya uwezo wa kocha na wachezaji wake. Gamondi hakujua hili.

Gamondi hakujua kama hata Nabi aliondoka akiiacha timu ikiwa bingwa na pia ikiwa imefika fainali za Kombe la Shirikisho Afrika. Yote haya Yanga hawakuyaangalia wakati walipoamua kuachana na Nabi. Hata kuna wachezaji waliachwa kwa staili hii. Djuma na Bangala hawakuona kama wangeweza kuachwa. Hersi akaichangamsha timu kwa kuleta wachezaji imara zaidi katika nafasi zao.
Hiki ndicho kitu ambacho kimempiga Gamondi bila ya kujijua. Ukitazama rekodi zake Yanga huoni namna gani anaweza kufukuzwa. Hata yeye mwenyewe akitazama rekodi zake anajiuliza ni namna gani Yanga wamechukua uamuzi mgumu dhidi yake. Ana robo fainali ya Ligi ya Mabingwa lakini pia mpaka sasa anashikilia mataji ya Ligi Kuu na FA. Hapa ndio wazi Gamondi hajui kilichompiga.
Gamondi alipaswa kuendelea kushikilia pale pale alipoishia msimu uliopita. Hata hivyo kiburi kikapanda juu na starehe zikapanda juu. Wachezaji wenyewe wakapoteza nidhamu na Yanga ikaanza kuwa na mechi ngumu tofauti na msimu uliopita ambapo ‘Pira Gamondi’ lilitembea hasa.

Inachoonekana ni kwamba kilichomuondoa Yanga wala sio kichapo cha Tabora United. Ile ilikuwa hitimisho tu la fikra za Hersi pamoja na vijana wenzake wa kamati ya utendaji. Tayari walishaandaa panga kwa muda mrefu na walikuwa wanatafuta sababu tu. Bahati mbaya kwa Gamondi ni kwamba vijana wenyewe huwa hawana haya katika kuamua mambo yao.
Na sasa ni zamu ni ya Sead Ramovic. Kocha mpya ambaye Yanga walimtambulisha ndani ya saa mbili tu baada ya kuachana na Gamondi. Ni Mjerumani ambaye jina lake inaonekana wazi lina asili ya Ulaya Mashariki. Alikuwa kocha wa TS Galaxy ya Afrika Kusini. Ana kazi ngumu ambayo mwanadamu lazima aifanye.

Kama akifanikiwa ndani ya Yanga basi Hersi atakuwa amefanya kazi yake kwa ukamilifu. Kwanza ni kwa sababu ametokea katika timu ambayo haijafanya vizuri Afrika Kusini msimu huu. Haijashinda mpaka sasa hivi. Yanga wamemchukua Ramovic kwa sababu ya mambo aliyofanya misimu iliyopita.
Mwenyewe analalamika kwamba mabosi wa timu hiyo walikuwa wanauza zaidi wachezaji na kushindwa kuwekeza katika timu. Yanga itakuwa imemchukua Ramovic kwa kuangalia namna Galaxy walivyokuwa wanatandika soka safi hapo awali huku wakipata matokeo mazuri dhidi Mamelodi Sundowns, Kaizer Chiefs na Orlando Pirates.
Vyovyote ilivyo Yanga wanatazamia Ramovic aanzie pale ambapo Gamondi aliishia kwa msimu uliopita. Soka safi. Pasi nyingi, ubora mkubwa wakati timu inapokuwa na mpira lakini mbinyo kwa wapinzani wakati timu haina mpira. Pumzi kubwa uwanjani na kucheza kibabe dhidi ya timu yoyote ndani na nje ya Tanzania. Ramovic ana deni hili hasa kwa kuzingatia namna Nabi alivyoisuka timu halafu akampasia Gamondi. Sasa hivi ni zamu yake.
Ramovic ana deni. Hawezi kudai ameipokea Yanga mbovu. Adai kwamba ameipokea timu yenye wachezaji wa kawaida. Ameipokea timu ambayo hata katika ardhi ya Afrika Kusini ilikwenda ikatamba. Msimu uliopita walidhulumiwa bao la Aziz Ki pale Pretoria, halafu mwanzoni mwa msimu huu waliiteketeza Kaizer Chiefs katika mechi za maandalizi ya msimu pale Bloemfotein. 4-0.
Wanachosubiri Yanga kwa sasa ni ubingwa mwingine. Ubingwa wa nne mfululizo wa Ligi Kuu na ubingwa wa FA. Lakini hapo hapo Yanga wanaamini kwamba wanapaswa kwenda katika nusu fainali yao ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika baada ya misimu miwili iliyopita kufika fainali yao ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kitu kizuri kwa wachezaji ni kwamba kila mmoja anaanza upya. Ndivyo inavyokuwa kokote duniani. Kocha mpya akiingia basi karibu kila mchezaji anaanza upya kumshawishi kocha kwamba anastahili kuanza katika kikosi cha kwanza. Kuna namna ambavyo maringo ya Gamondi yalisababisha awatenge baadhi ya wachezaji.
Ghafla Gamondi akawa hampangi wala kumfikiria Kibwana Shomari. Ikafikia hatua akamrudisha Dennis Nkane kuwa beki wa kulia wakati Yao Kouassi alipokuwa anakosekana uwanjani. Huenda Kibwana akaitumia fursa hii kujaribu kumshawishi kocha mpya kwamba yeye ndiye msaidizi namba moja wa Yao Kouassi.
Aziz Ki alikuwa anapoteza mipira ovyo uwanjani huku Clatous Chama akiwa ameshika tama katika benchi. Pacome Zouzoua hakuwa yule tena wa msimu uliopita lakini yeye na Aziz ni lazima wangeanza katika mechi yoyote ngumu. Gamondi alikuwa amewakariri. Itakuwa vema pia kwa Jean Baleke ambaye Gamondi hakumpenda. Huenda vita ikaanza upya kati ya Clement Mzize, Prince Dube na Baleke.
Ramovic anakaribishwa katika mpira wetu. Kitu cha msingi kwake akumbushwe tu namna ambavyo Nabi na Gamondi waliondoka kiajabuajabu chini ya Injinia Hersi na kamati yake ya utendaji. Presha ni kubwa kuwa kocha wa Yanga au watani wao Simba. Msimu mmoja tu unaweza kumtosha na watu wakavunja mkataba.