Jet Li amkabidhi mkewe utajiri wake wote

China. Mwigizaji Li Lianjie ‘Jet Li’ amewaacha mashabiki wake midomo wazi baada ya kufunguka kuwa amemkabidhi mkewe Nina Li Chi utajiri na fedha zake zote.

Mwigizaji huyo mwenye utajiri unaokadiriwa dola milioni 260, kupitia mahojiano yake ya hivi karibuni ameweka wazi kuwa uamuzi huo haukutokana na matatizo yake ya kiafya ambapo anasumbuliwa na ugonjwa wa hyperthyroidism na matatizo ya mgongo bali ni kwa sababu ana imani kubwa kwa mkewe.

“Upendo wake wa kwanza, anastahili zaidi.  Ama hakika, kwa miaka mingi, Nina amekuwa kitu kikubwa kuliko tu kuwa mpenzi wangu yeye ni mshauri, nguzo yangu ya nguvu. Alikuwa daima upande wangu, Li wakati nilipokuwa chini kabisa, alinisimamia. Anasimamia kila kitu ili niweze kuzingatia kazi yangu na afya yangu. Lolote lile, namwamini. Yeye ndiye sababu naweza kuwa ninavyokuwa leo,” amesema Jet Li.

Nina ambaye ni mke wa Li alivishwa taji la Miss Asia mwaka 1986, wawili hao walikutana na kuanzisha uhusiano mwaka 1988, aidha moja ya sababu inayomvutia Li kutoka kwa mkewe ni kumtii kuacha shughuli zake za urembo na kujikita zaidi kulea familia.

                        

Uaminifu huo wa Li kwa mkewe uliibua mijadala mbalimbali katika mtandao wa X (zamani Twitter) mashabiki wakiwapongeza wawili hao kwa kuaminiani wakiandika: “Hii si kuhusu pesa, somo la upendo ni kuhusu kuthamini mtu ambaye amekuwa upande wako kupitia kila kitu.”

Mkali huyo wa filamu za ngumi ambaye amewahi kuonekana kwenye Mulan, League of Gods, The Founding of a Republic, War na nyinginezo anadai hata akitaka kununua kitu chochote basi atamuomba mkewe pesa.

Wawili hao walifunga ndoa mwaka 1999 na wamebahatika kupata watoto wawili.