Utawala wa Kizayuni ulioanzisha vita dhidi ya Lebanon kama ulivyotangaza kwamba ni kwa lengo kuwarejesha walowezi katika nyumba zao, hivi sasa unakabiliwa na ongezeko la walowezi wanaokimbia makazi yao, askari waliochoshwa na vita na majeruhi wengi.
Baada ya kutolewa amri ya Hizbullah ya kuhama katika vitongoji 25 vya walowezi wa kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu, kumeanza wimbi jipya la kuhama makazi Wazayuni katika eneo hilo.
Ili kuunda kizuizi dhidi ya mashambulizi ya jeshi la Kizayuni katika maeneo yanayolengwa na raia huko Lebanon, ambayo hadi sasa yamesababisha vifo na majeruhi zaidi ya watu elfu 15 na kuhama zaidi ya watu milioni moja, Hizbullah iliongeza wigo wa mashambulizi yake ya makombora. Sasa walowezi milioni moja zaidi wamo katika rada ya mashambulizi haya.
Kwa kutoa amri mbalimbali, Hizbullah imewaonya Wazayuni kwamba vitongoji vyao vimekuwa eneo la askari adui wanaoshambulia Lebanon, na kwa sababu hiyo, vitongoji hivi vimekuwa shabaha halali za kijeshi kwa vitengo vya anga na vya makombora vya Muqawama wa Kiislamu wa Lebanon.
Baada ya kutolewa kwa taarifa hizi, ambazo ziliambatana na hatua za kiutendaji kama vile kulenga kikosi cha Golani na nyumba ya Netanyahu, wimbi la walowezi waliokimbia kutoka makazi ya kaskazini ya maeneo yanayokaliwa kwa mabavu liliongezeka, ambapo vyombo vya habari na vituo vya televisheni vya utawala vamizi pia vinathibitisha suala hili.

Hii ina maana kwamba, vita vilivyoanzishwa na Netanyahu dhidi ya Lebanon, hususan katika suala la kuwarejesha wakimbizi wa makazi ya walowezi wa kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kuwapokonya silaha Harakati ya Hizbollah, havijafikia malengo yake, na walowezi waliosalia al-Jalil nao sasa wanakimbia.
Mmoja wa makamanda wa zamani wa Jeshi la Anga la Israel anakiri kwa kusema kuwa: Hizbullah ingali inadumisha nguvu yake kuu na ina uwezo wa makombora ambao unaweza kutishia sio tu kaskazini mwa Israel bali eneo zima.
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon ikitumia kamera iliyoweka katika ndege zisizo na rubani au katika makombora yake imeweza kurekodi nyayo na athari zake katika vyombo vya habari vya kijeshi hasa pale inapolenga vikosi vya utawala wa Kizayuni, ktendo ambacho wanaharakati wa mitandao na vyombo vya habari wanakitafsiri kama “kombora la Hizbollah lenye kamera”.

Kuendelea mashambulizi ya Hizbullah, kuvurumishwa mara kwa mara makombora na ndege zisizo na rubani kuelekea kaskazini na katikati mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel), na kukabiliana na harakati ya ardhini ya jeshi la Kizayuni kusini mwa Lebanon, kumewafanya wanasiasa, wataalamu na wafasiri zaidi wa Kizayuni kuonya uzito wa hali ya sasa na mustakabali mbaya wa vita kati ya utawala huo na Hizbullah.
Kwa upande mwingine, jeshi la Kizayuni kivitendo limekwama katika eneo la mbele la kusini mwa Lebanon na hakuna siku ambayo halipati hasara.
Kutokana na vita vya Gaza, jeshi la Kizayuni limechoka na limedhoofika na limezungukwa na wapiganaji wa Hizbullah ambao wamejifunza mbinu za kujihami kwa muda mrefu.
Herzi Halevi, Mkuu wa Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel amesema: Tumepata hasara kubwa na chungu.
Vyombo vya habari vya Kiebrania viliripoti kuwa jeshi la Israel lilitangaza kujeruhiwa kwa wanajeshi 594 tangu kuanza kwa operesheni ya ardhini kusini mwa Lebanon.
Hivi majuzi, Yair Lapid, kiongozi wa upinzani wa utawala wa Kizayuni alisema tangu kuanza kwa vita hivyo, askari 11,000 wamejeruhiwa na askari 890 kati yao wameuawa. Jeshi la Israel nalo limetangaza kuwa, wanajeshi wake 5,150 wamejeruhiwa tangu kuanza uvamizii dhidi ya Gaza huku hali ya 764 kati yao ikiwa mbaya.

Kadhalika Shirika la Redio na Televisheni la Kizayuni likinukuu takwimu za Wizara ya Afya ya utawala huo ghasibu limetangaza kuwa, Waisraeli 300,000 wanapata matibabu ya kiakili kutokana na athari za vita hivyo.
Nukta ya kuzingatia katika ripoti za vyanzo vya Israel ambavyo vinajizuia kutangaza idadi ya vifo vya wanajeshi wake ni hii kwamba, kukiri huku lenyewe hili linaashiria kuwa majeruhi ni wengi kuliko idadi inayotajwa.
Kwa hiyo, wafuatiliaji wa mambo wanaamini kwamba, kwa kuzingatia kushindwa kwa jeshi la Kizayuni kufikia malengo yake yaliyotajwa, Hizbullah sasa imeukamata pabaya utawala wa Kizayuni na kuufanya unase katika kinamasi cha vita ambavyo hakuna njia ya kutoka.