Jeshi la Uganda liliwashambulia wanahabari wakati wa uchaguzi mdogo: RSF

Shirika la wanahabari wasio na mipaka RSF katika taarifa yake limethibitisha kwamba wanahabari 18 nchini Uganda walishambuliwa na jeshi wakati wakiangazia uchaguzi mdogo.

Imechapishwa:

Dakika 1

Matangazo ya kibiashara

Kulingana na RSF, wanahabari hao walipigwa vibaya wakati wakifuatilia uchaguzi mdogo katika eneo la Kawempe kaskazini jijini Kampala tarehe 13 ya mwezi Machi na maofisa wa jeshi pamoja na maofisa wa kitengo cha kupambana na ugaidi.

“Walitulazimu kutoa kufunika uso kwa mavazi yetu, wakatuambia tulale chini ambapo walituchapa kwa fimbo pamoja na kutugonga na bunduki zao”, alisema mpiga picha wa gazeti la ndani la Abubaker Lubowa.

Baadhi ya wanahabari pia waliripoti kwamba vifaa vyao vya kazi vilichukuliwa na kuharibiwa wakati wenzao pia wakieleza kuzuiliwa kwa saa kadhaa kwenye gari la jeshi.

Mkuu wa shirika la RSF katika mataifa ya nchi za kusini mwa jangwa la Sahara Sadibou Marong ametaka uchunguzi kufanyika kikamilifu.

Yoweri Museveni wa Uganda amekuwa akituhumiwa kwa kuongoza kwa mkono wa chuma.
Yoweri Museveni wa Uganda amekuwa akituhumiwa kwa kuongoza kwa mkono wa chuma. © Captures d’écran CTV Uganda

Wanajeshi wanatuhumiwa kwa kuwalenga kimakusudi wanahabari ambao walijitambulisha rasimi kama wapasha habari.

Hatua hii ya kushambuliwa kwa wanahabari imekuja kuelekea uchaguzi mkuu wa urais wa mwaka wa 2026 nchini Uganda, tukio linaloibua wasiwasi. Uganda inashikilia nafasi ya 128 dunaini katika orodha ya nchi ambazo haziheshimu uhuru wa wanahabari.

Mgombea wa ubunge kwa tiketi ya chama cha rais Yoweri Museveni alipoteza katika uchaguzi huo mdogo kwenye eneo bunge la Kawempe kaskazini dhidi ya yule wa chama cha Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine.

Museveni na jeshi lake wamesema wataanzisha uchunguzi kuhusu kilichotokea wakati wa uchaguzi huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *