Jeshi la Sudan layateka tena makao makuu ya jimbo la Sinnar la katikati mwa nchi

Serikali ya Sudan ilitangaza jana Jumamosi kuwa jeshi la nchi hiyo SAF limeuteka tena mji wa Singa ambao ni makao makuu ya mkoa wa Sinnar wa katikati mwa nchi hiyo ambao ulikuwa unadhibitiwa na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF).

Katika taarifa yake rasmi, Khalid Aleisir, Waziri wa Habari na Utamaduni wa Sudan amesema: “Leo (Jumamosi), mji wa Singa umerejea mikononi mwa serikali… Wakati wa haki na uwajibikaji utafika, na wale wote wanaohusika na uhalifu huu watawajibishwa kwa matendo yao.”  

Pia amesema: “Imani thabiti waliyo nayo wananchi wa Sudan kwa vikosi vyao vya kijeshi, kijasusi na vikosi vingine vya kawaida itaendelea kuwepo kwani vikosi vyetu vya ulinzi vitabaki kuwa na nguvu na havitoyumba bila ya kujali vitisho vya ndani na nje.” 

RSF ilikuwa imeudhibiti mji wa Singa kwa miezi kadhaa. Tangu mwanzoni mwa mwezi Oktoba, jeshi la Sudan SAF limekuwa likipigana na RSF ili kuuteka tena mji huo. 

Hii ni kusema kuwa jeshi la Sudan limefanikiwa pia kutwaa tena miji muhimu katika jimbo hilo la Sinnar kutoka kutoka mikononi mwa RSF ikiwa ni pamoja na miji ya Al-Dinder na Al-Suki na eneo la kimkakati la Jebel Moya ambalo liko kwenye njia panda inayounganisha majimbo ya Gezira, White Nile na Sinnar.

Uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi wanaoongoza makundi mawili ya SAF na RSF unaendelea kuinakamisha Sudan tangu katikati ya mwezi Aprili 2023. Maelfu ya watu wameshauawa hadi hivi sasa na mamilioni ya wengine wamekuwa wakimbizi.