
Jeshi la Sudan limelaumu kundi la wapiganaji wa Rapid Support Forces (RSF) Alhamisi kwa kuwaua raia watano katika mashambulizi ya ndege zisizokuwa na rubani kwenye eneo la El-Obeid, mji mkuu wa Jimbo la Kordofan Kaskazini.
Katika taarifa, jeshi limesema RSF ililenga Soko Kuu, sehemu ya viwanda, na kusababisha mauaji ya watu watano na kuwajeruhi wengine.
RSF haijazungumza chochote kuhusu tukio hilo.
Jeshi limeshtumu “tabia hiyo ya kihalifu,” likisema ni sehemu “ya muendelezo wa ukiukwaji unaoendelezwa na wapiganaji hao dhidi ya raia na miundombinu ya raia.”
Liliongeza kuwa hatua hizo za RSF “ni muendelezo wa uhalifu na upingaji wa wazi wa sheria ya kimataifa kuhusu haki za binadamu.”
Wapiganaji wa RSF na jeshi wamekuwa wakikabiliana wakitaka kuchukua madaraka ya nchi tangu Aprili 2023, jambo lililosababisha mauaji ya maelfu ya watu na kufanya Sudan kuwa na hali mbaya zaidi kwa raia duniani.