
Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na mmoja wa viongozi mashuhuri wa upinzani nchini Tanzania amekamatwa na jeshi la Polisi.
Mbowe na viongozi wengine kadhaa wa upinzani wamezuiliwa na polisi Kusini Magharibi mwa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti zilizotolewa na Polisi hapo jana, wanasiasa hao wamezuiliwa ili kuhojiwa kwa madai ya kukiuka kanuni za kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chadema, John Mrema amekanusha maelezo ya polisi la kulaani alichokiita ujanja wa kuhujumu kampeni za chama hicho.
Chadema ililalamika wiki hii kwamba wagombea wake wengi walienguliwa “kiuonevu” kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27.
Mwezi Septemba, Mbowe na makamu wake Tundu Lissu, pamoja na viongozi wengine wa upinzani waliwekwa kizuizini kwa muda baada ya askari wa kutuliza ghasia kuzuia maandamano makubwa yaliyokuwa yamepangwa kufanyika jijini Dar es Salaam.