Jeshi la Kizayuni kutokuwa na uwezo wa kuendelea na vita vya Ukanda wa Gaza

Kuendelea vita vya Ukanda wa Gaza, kumeanika wazi zaidi udhaifu wa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel katika medani ya vita.

Baada ya kuanza Oparesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa,  watawala wa Kizayuni wa Israel na jeshi la utawala huo wamekuwa wakihalalisha vitendo vyao vya jinai za kinyama dhidi ya raia wasio na ulinzi wa Palestina ili kufidia kushindwa na udhaifu wao  katika vita vya Gaza. Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni amedai kuwa vita vya Gaza vitaendelea hadi Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) itakapoangamizwa.

Kupenda vita Wazayuni kumekuwa na taathira mbaya za kiuchumi na kiusalama katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina, jambo ambalo hata viongozi wa utawala huo wenyewe wanalikiri. 

Utayari wa vikosi vya Muqawama na mashambulizi yao makubwa yamelishangaza sana jeshi la Israel na hivyo kudhihirisha wazi udhaifu wake katika nyanja tofauti. Katika hali hiyo vita vimebadilika kuwa jinamizi la kutisha kwa jeshi hilo la Kizayuni na mara nyingi vikosi vya jeshi hilo vinakataa kuendelea na vita katika vita vya Ukanda wa Gaza.

Wapiganaji wa Hamas, Gaza

Magonjwa ya akili na hofu ya vita, mizozo kati ya askari wa kawaida na makamanda wa jeshi na kutokuwa tayari vikosi vya akiba kushiriki kwenye medani ya vita huko Gaza ni baadhi tu ya matokeo ya vita vya utawala wa Kizayuni. Jeshi la Kizayuni, licha ya kupata uungaji mkono wa pande zote wa silaha na kifedha kutoka Marekani katika miezi ya hivi karibuni, lakini halijaweza kuzuia mafanikio ya makundi ya Muqawama wa Palestina, na mbali na hayo, maandamano katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina (Israel) dhidi ya Netanyahu yanazidi kupamba moto.

Upande mwingine wa vita vya Gaza, unadhihirisha uwezo mkubwa wa vikosi vya Muqawama katika kutekeleza oparesheni kubwa dhidi ya Israel na kulenga vituo vya kijeshi na kijasusi vya utawala huo, jambo ambalo limefichua uongo wa Wazayuni na ngano zao za eti kutoshindwa utawala huo katika medani ya vita.
Jeshi la Kizayuni linakabiliana na matokeo hasi ya vita vya Ukanda wa Gaza kadiri kwamba vikosi vya jeshi la utawala huo vinakabiliwa na mgogoro mkubwa vitani. Udhaifu wa askari jeshi sambamba na mafanikio ya oparesheni za makundi ya Muqawama katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Israel umedhihirisha pakubwa kudhoofika kkwa Wazayuni. Katika hali hiyo, vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni navyo vimelazimika kukiri kuhusu udhaifu wa jeshi hilo na kutoweza kwake kukabiliana na maadui zake katika medani ya vita.

Wanajeshi wa Israel

Noam Amir, ripota wa kanali 14 ya televisheni ya utawala wa Kizayuni amekiri katika ripoti yake kwamba,  idadi ya ndege ambazo jeshi la anga la utawala huo lilizitumia  siku ya Jumanne, Oktoba 22, kwa ajili ya kutafuta na kufuatilia ndege isiyo na rubani iliyorushwa kutoka Lebanon, haina kifani na kuwa hilo linaonyesha wazi kutokuwa tayari kwa jeshi hilo kuendelea na vita. Redio ya utawala wa Kizayuni pia imekinukuu chanzo cha kijeshi cha utawala huo ghasibu kikisema kuwa, mabaki ya ndege hiyo isiyo na rubani iliyorushwa kutoka Lebanon bado hayajapatikana hadi sasa. Kanali ya 12 ya televisheni utawala wa Kizayuni pia imeripoti kuwa askari 15 wa utawala huo kutoka kikosi cha askari wa miavuli ambao walishiriki katika vita vya Ukanda wa Gaza wameitwa kurejea vitani, lakini wamekataa.

Taathira za vita vya Gaza zimedhihirisha zaidi udhaifu mkubwa wa jeshi la utawala wa Kizayuni katika nyanja mbalimbali. Askari wengi wa Kizayuni hawataki kuendelea na vita, nao makamanda wao wamekiri mara kadhaa kuhusu udhaifu wa vikosi vyao katika uwanja wa vita. Kuendelea vita vya Gaza kumedhihirisha upande mwingine wa mgogoro ambao unalisumbua jeshi la Israel ambao umewaathiri wajeshi wake na kushindwa kujinasua katika hali hiyo.