Jeshi la Israel laua Wapalestina 14 Ghaza baada ya kuua Walebanon 14 pia Bekaa

Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel limeendelea kufanya jinai za mauaji ya kinyama katika Ukanda wa Ghaza kwa kuwaua shahidi Wapalestina 14 asubuhi ya leo waliokuwa wamepata hifadhi katika linalodaiwa na utawala huo kuwa ni “eneo salama” huko al-Mawasi.

Mahmoud Basal, msemaji wa ulinzi wa raia wa Ghaza, amevieleza vyombo vya habari kuwa mashambulizi yaliyofanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni leo asubuhi yameua watu wasiopungua 14 na kujeruhi makumi kadhaa.

Mbali na mashambulio ya Ghaza, jeshi la Israel limeendeleza pia mashambulizi yake katika kila kona ya Lebanon na kuua shahidi watu watatu mashariki mwa Bekaa, saa chache baada ya kuwaua watu wengine 14 katika shambulio lililofanya kwenye mji huo wa kaskazini, mbali na mpaka wa nchi hiyo na Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Hayo yanajiri huku waziri mpya wa ulinzi wa utawala haramu wa Israel Katz akitangaza kuwa utawala huo hauko tayari kusimamisha vita na harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Lebanon, Hizbullah.

Mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na utawala ghasibu wa Israel huko Ghaza yameshaua shahidi Wapalestina wasiopungua 43,603 na kujeruhi 102,929 tangu Oktoba 7, 2023.

Nchini Lebanon, hadi sasa watu wapatao 3,243 wameuawa shahidi na 14,134 wamejeruhiwa katika mashambulizi ya jeshi la Kizayuni tangu vilipoanza vita dhidi ya Uaknda wa Ghaza…/