Jeshi la Israel lashindwa kikamilifu kudhibiti mji wa al Khiam wa Lebanon

Duru za kuaminika za Lebanon zimetangaza kuwa, wanajeshi vamizi wa utawala wa Kizayuni wamekimbia kikamilifu katika mji wa al Khiam wa kusini mwa Lebanon kutokana na vipigo vikali walivyopata mtawalia kutoka kwa harakati ya Hizbullah.

Duru hizo za Lebanon zimesema kuwa, wanajeshi wa Israel wamelazimika kukimbia kutoka maeneo yote ya mashariki na kusini mwa mji wa al Khiam kutokana na vipigo vya mfululizo walivyopata kutoka kwa wanamapambano wa Hizbullah katika siku za hivi karibuni. 

Duru hizo zimesisitiza kuwa, jeshi la Israel limefeli na halikuweza kuuteka na kuukalia kwa mabavu mji wa al Khiam kiasi kwamba wanajeshi wote wamelazimika kukimbia na haonekani mwanajeshi yoyote wa Israel karibu na mji huo wa kusini mwa Lebanon. 

Kwa upande wake, mwandishi wa televisheni ya al Manar amethibitisha habari hiyo na kusema kuwa, wanajeshi vamizi wa Israel wamelazimika kuondoka kabisa karibu na mji wa al Khiam baada ya kupigwa vibaya na Hizbullah katika maeneo ya Sarda, al Umra na kwenye kilima cha al Hamamisw. Wanajeshi hao wa Israel wamekimbilia kwenye kitongoji cha walowezi wa Kizayuni cha Matleh, kaskazini mwa ardhi za Palestina zilizopachikwa jina bandia la Israel.