
KIWANGO kinachoonyeshwa na straika wa Simba Queens, Jentrix Shikangwa huenda akavunja rekodi yake ya msimu 2022/23 wa kufunga mabao 17.
Hadi sasa ndiye kinara wa mabao akiweka nyavuni mabao 16 huku Stumai Abdallah wa JKT Queens akiwa nayo 11.
Ndiye mshambuliaji aliyefunga hat-trick nyingi kwenye michezo 11 akifunga tatu huku Stumai akiweka mbili.
Ni kama kuna vita kati ya wawili hao wanaokipiga timu zenye ushindani kwenye Ligi ya Wanawake kutokana na mwenendo wao.
Sasa swali lipo kwa Shikangwa je, ataweza kuvunja rekodi yake ya msimu juzi ya kufunga mabao 17 baada ya msimu huu tayari kuweka kambani 16 likibaki bao moja kufikisha idadi hiyo akiwa na mechi nane mkononi.
Huu unaweza kuwa msimu bora zaidi wa Mkenya huyo tangu ajiunge na Simba msimu juzi ambaye msimu wake wa kwanza aliibuka kinara na kuondoka na tuzo ya kiatu.
Pia unaweza kuwa msimu wa nne mfululizo wa Simba kama Shikangwa atamaliza kinara kwa kutoa wafungaji baada ya msimu 2021/22 Asha Djafar kufunga mabao 26 uliofuata akauchukua straika huyo na mwaka jana Aisha Mnunka akabeba akifunga mabao 20.
Urejeo wa Mnunka pia umeongeza ushindani kwa nyota huyo kuendelea kufanya vizuri kutokana na wote wawili wanawania namba kwenye kikosi hicho.