
Kamanda wa ngazi ya juu zaidi wa kijeshi nchini Iran amesema kuwa Majeshi ya Iran yameandaa jibu kali kwa shambulio la mwezi uliopita la utawala wa Israel dhidi ya Iran, akisisitiza kwamba kulipiza kisasi kutakuwa “tofauti” na “zaidi ya inavyodhaniwa” na utawala huo ghasibu.
Akizungumza siku ya Jumanne, Mkuu wa Majeshi ya Iran Meja Jenerali Mohammad Baqeri amesema kuwa Iran tayari imefanya oparesheni mbili dhidi ya Israel katika masuala ya mbinu na silaha na kwamba vile vile, jibu lake la baadaye kwa mashambulizi ya hivi karibuni ya Israel litakuwa zaidi ya wanavyodhania watawala wa Israel.”
Ameongeza kuwa: “Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kamwe haitavumilia uchokozi dhidi ya ardhi yake na haitacha uvamizi upite bila kujibiwa, na kwa hivyo bila shaka itatoa jibu linalofaa.“
Tarehe 26 Oktoba, ndege za kivita za Israel zilitumia anga inayodhibitiwa na Marekani nchini Iraq kuvurumisha makombora kwenye vituo vya kijeshi katika mikoa ya Tehran, Khuzestan na Ilam nchini Iran ikiwa ni ukiukaji wa wazi wa mamlaka ya kitaifa ya Iran, na kuua maafisa wanne wa Jeshi na raia mmoja.
Iran ilisema kuwa shambulio hilo la kigaidi lilizuiliwa kwa mafanikio kwa kutumia mfumo wa ulinzi wa anga uliotengenezwa ndani ya nchi na kwamba lilisababisha uharibifu mdogo tu kwenye maeneo ya rada. Maafisa wa Iran wamesisitiza kuhusu haki ya taifa hili ya kutoa majibu kwa utawala huo wa ghasibu na wa kibaguzi.
Meja Jenerali Baqeri ameonya kwamba Israel “italipa gharama kubwa” kwa kuvamia ardhi ya Iran.