Simiyu. Washtakiwa wawili kila mmoja amefungwa miaka mitano jela kwa wizi wa nguruwe. Waliokumbwa na adhabu hiyo katika Mahakama ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu ni Masunga Chenya(20)na Daud Elias(19) wakazi wa Mtaa wa Sola mjini Maswa.

Kabla ya hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Aziz Khamis kutoa hukumu hiyo leo Jumanne Machi 11,2025, Mwendesha mashitaka kutoka ofisi ya Taifa ya mashitaka wilaya hiyo, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Vedastus Wajanga aliieleza Mahakama kuwa vijana hao kwa pamoja waliiba nguruwe mmoja mwenye thamani ya Sh500,000 mali ya Clerdes Donacian mkazi wa mtaa wa Sola wilayani humo.
Amesema kuwa tukio hilo lilitokea Septemba 2,2024 saa 11;00 alfajiri baada ya washtakiwa wote kuingia ndani ya zizi la nguruwe linalomilikiwa na Clerdes Donacian na kuiba nguruwe huyo dume, na siku hiyohiyo walikamatwa wakiwa naye katika mtaa huo wa Sola.
Taarifa zilifika kituo cha polisi wilaya hiyo na askari polisi wafika eneo la tukio na kukuta tayari washtakiwa wapo chini ulinzi wa wananchi wakiwa pamoja na kielelezo ambacho ni nguruwe.
Walishtakiwa katika Mahakama hiyo kwa makosa mawili la kwanza ni wizi wa mifugo kinyume na kifungu cha 258 (1)(2) (a) na 268 (1)(3)cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyo fanyiwa marejeo mwaka 2022 .
Na katika kosa la pili la kupatikana na mali idhaniwayo kuwa ni ya wizi kinyume na kifungu cha 312(1)(b) na( 2) Cha sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 Kama ilivyo fanyiwa marejeo mwaka 2022.
Upande wa mashitaka ulileta jumla ya mashahidi watano na vielelezo viwili ambavyo vilitolewa mahakamani hapo ili kuthibitisha mashitaka hayo.
Baada ya washtakiwa kutiwa hatiani upande wa mashitaka uliiomba Mahakama kuwapa adhabu kali ili iwe funzo kwao na kwa jamii, kwani matuko ya wizi wa mifugo yanaongezeka ndani ya wilaya na mkoa huo.