Jela miaka mitano kwa kummwagia mtoto chai ya moto

Geita. Mahakama ya Wilaya ya Geita imemuhukumu kifungo cha miaka mitano jela, pamoja na kulipa faini ya Sh1 milioni baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumjeruhi mtoto mwenye umri wa miaka saba kwa kumwagia chai ya moto.

Hukumu hiyo imetolewa Aprili 8, 2025 na Hakimu mwandamizi wa mahakama hiyo, Bruno Bongole baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo ambapo pia hukumu hiyo imemtaka mshtakiwa kumlipa mwathirika wa tukio hilo fidia ya Sh2 milioni.

Katika kesi hiyo ya mwaka 2025 mshtakiwa alitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 169A (1) na (2) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Awali, mwendesha mashitaka wa Serikali, Wakili Godfrey Odupoy akisaidiana na Consesa Desideri aliieleza Mahakama kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Agosti 03, 2024 saa tatu asubuhi katika Mtaa wa Mwembeni Kata ya Nyankumbu Manispaa ya Geita.

Alisema mshitakiwa alimmwagia chai ya moto kwenye mguu wa kushoto mtoto huyo ambaye alikuwa chini ya uangalizi wake,  na kumsababishia majeraha makubwa na maumivu makali.

Akijitetea mahakamani hapo, Rehema ameiomba mahakama kumpunguzia adhabu kwa kuwa ana mtoto mchanga.

“Mheshimiwa hakimu naomba nipunguziwe adhabu kwa kuwa nina mtoto mchanga ana miezi minne,” ameomba Rehema.

Akitoa hukumu hiyo baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka, Hakimu Bongole amesema ushahidi uliotolewa mahakamani hapo umethibitisha pasipo shaka kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo.

Hakimu Bongole amesema kwa kuzingatia kifungu cha 13 (1) cha Sheria ya mtoto Sura ya 13 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019 na ushahidi wa mashahidi watano walioutoa mahakamani hapo pamoja na utetezi wa mshtakiwa, Mahakama imejiridhisha pasipo shaka kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo.

Amesema Mahakama imetoa adhabu hiyo ili iwe fundisho kwa watu wengine wanaowafanyia watoto ukatili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *