Jela miaka 30 kwa kumbaka mtoto wa miaka 17

Geita. Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita, imemuhukumu Ramadhan Katoro kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 17.

Mshtakiwa alitenda kosa hilo kinyume na Kifungu cha 131(1) cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Hukumu hiyo ilitolewa Aprili 29, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Bruno Bongole.

Awali, Mwendesha Mashtaka wa Serikali,  Godfrey Odupoy kwa kushirikiana na Consesa Desideri, waliieleza Mahakama kuwa kati ya Desemba 12, 2024 na Februari 10, 2025, katika maeneo ya Bomani na Mseto, Wilaya ya Geita, mshtakiwa alikuwa akiishi na kufanya tendo la ndoa mara kwa mara na mwathirika, ambaye ni mtoto wa miaka 17.

Wakili Odupoy ameeleza kuwa uchunguzi wa tukio hilo ulibaini kuwa mwathirika alikuwa akiishi na mshtakiwa kama mume na mke.

Akitoa ushahidi wake mahakamani, mtoto huyo alikiri kuwa aliondoka nyumbani kwao Desemba 12, 2024 na kwenda kuishi kwa mshtakiwa, aliyekuwa mpenzi wake, na walikuwa wakiishi kama wanandoa huku wakifanya mapenzi mara kwa mara. Alisema hakuwa na mpenzi mwingine.

Shahidi wa tatu, ambaye ni daktari aliyefanya uchunguzi, alisema hakukuwa na dalili za kuingiliwa kwa nguvu, lakini matokeo yalionyesha mwathirika alikuwa akifanya tendo la ndoa mara kwa mara.

Katika utetezi wake, Katoro alikiri kuishi nyumba moja na mwathirika, lakini alikana kosa la kumbaka.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Bongole amesema kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto, Sura ya 13, mtoto ni mtu yeyote aliye chini ya umri wa miaka 18, na hivyo hata kama kulikuwa na ridhaa, tendo hilo ni kosa kisheria.

Amesema Mahakama imeridhika pasipo shaka na ushahidi uliotolewa na mashahidi watano wa upande wa Jamhuri na wawili wa utetezi kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo, na hivyo Mahakama imemtia hatiani na kumuhukumu kifungo cha miaka 30 jela.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *