Jela miaka 30 kwa kubaka, kumtia mimba mwanafunzi

Simiyu. Mahakama ya Wilaya ya Maswa, mkoani Simiyu, imemuhukumu Jumanne Clement (23), mkazi wa Ngudu Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza, kutumikia kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kumbaka na kumpa ujauzito mwanafunzi wa kidato cha kwanza mwenye miaka 15.

Hukumu hiyo imesomwa leo Jumatano Aprili 30, 2025 na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Enos Misana.

Hakimu Misana amesema mshtakiwa amekutwa na hatia katika makosa matatu, kosa la kwanza na la pili amemuhukumu kifungo cha miaka 30 na kosa la tatu atatumikia kifungo cha miaka mitano jela.

“Hata hivyo, adhabu hizi zinaenda pamoja, hivyo nakuhukumu kifungo cha miaka 30 gerezani,” amesema hakimu huyo.

Aidha, Hakimu Mwandamizi Misana amesema Mahakama hiyo pia inamuamuru Clement kumlipa mwathirika fidia ya Sh500,000.

Amesema Mahakama imetoa hukumu hiyo baada ya kuridhika na ushahidi wa upande wa mashitaka, ambao uliwasilisha mashahidi watano, akiwamo mwathirika mwenyewe na vielelezo vinne kuthibitisha makosa hayo.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka katika kesi ya jinai mshtakiwa alitenda makosa hayo usiku wa kuamkia Aprili 20, 2024, katika kijiji cha Jijabilishi wilayani Maswa. Baada ya tukio hilo, inaelezwa alimchukua mwanafunzi huyo na kuishi naye nyumbani kwake mjini Ngudu kwa nia ya kumuoa pasi ridhaa ya wazazi  wala binti mwenyewe.

Clement alishtakiwa kwa makosa matatu likiwamo la kubaka, kinyume na kifungu cha 130(1)(2)(e) na 131(1) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Kosa la pili ni la kumtia mimba mwanafunzi, kinyume na kifungu cha 60A(3) cha Sheria ya Elimu Sura ya 353, marejeo ya mwaka 2002, kama ilivyofanyiwa marekebisho kupitia kifungu cha 22 cha Sheria ya Marekebisho Madogo Na. 2 ya mwaka 2016.

Huku kosa la tatu likiwa ni kupoka kinyume na kifungu cha 134 na 35 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, marejeo ya mwaka 2022.

Utetezi wake

Awali mshtakiwa alikana mashitaka yote na kudai kuwa alisingiziwa bila ushahidi wa moja kwa moja. Hata hivyo, upande wa mashitaka uliomba apatiwe adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine.

Akijitetea baada ya kupewa nafasi nyingine, Clement aliiomba Mahakama impunguzie adhabu alisema ni mara yake ya kwanza kufikishwa mahakamani na ana familia inayomtegemea.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Mahakama iliridhika kuwa upande wa mashitaka umeweza kuthibitisha kesi dhidi ya mshtakiwa, na hivyo ikamtia hatiani na kutoa adhabu hiyo.

 “Kwa kuzingatia kwamba kitendo alichotekeleza mshtakiwa ni kinyume cha sheria na maadili ya Mtanzania, na kimeacha athari isiyofutika kwa mwathirika, ikiwemo kumwacha na ujauzito ambacho pia ni aina ya ukatili wa kijinsia, ni wazi kuwa kinastahili adhabu kali,” amesema hakimu kabla ya kutoa adhabu.

“Hivyo basi, Mahakama hii baada ya kumtia hatiani mshtakiwa Jumanne Clement kwa kosa aliloshtakiwa nalo, inamuhukumu kutumikia kifungo cha miaka 30 jela. Aidha, mshtakiwa anaamriwa kumlipa mwathirika fidia ya Sh500,000,” alimalizia hakimu huyo.

Awali, Mwendesha mashitaka, Vedastus Wajanga, aliieleza Mahakama kuwa hakuna kumbukumbu zozote za kihalifu za awali zinazomuhusu mshtakiwa.

Hata hivyo aliiomba Mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa mshtakiwa na onyo kwa wengine wenye nia ya kutenda makosa kama hayo.

Kesi hiyo ilifunguliwa na kuendeshwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Violeth Mushumbusi kwa kushirikiana na Mwendesha Mashtaka wa Jeshi la Polisi, Vedastus Wajanga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *