Jela miaka 20 kwa kukutwa na vipande vya meno ya tembo

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemhukumu, Pascal Daima (43) kutumikia kifungo cha miaka 20 jela, baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na vipande viwili vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh34 milioni.

Daima, mkazi wa Kongowe mkoani Pwani anayekabiliwa na shtaka moja la kusafirisha vipande viwili vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh34 milioni, bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori, tukio analodaiwa kulitenda Agosti 11, 2021, Mtaa wa Tandale, Mkunduge Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Hukumu hiyo imetolewa leo, Aprili 30, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu Gwantwa Mwankuga, baada ya mshitakiwa kutiwa hatiani kama alivyoshtakiwa.

“Mshtakiwa umetiwa hatiani kama ulivyoshtakiwa, hivyo Mahakama inakuhukumu kifungo cha miaka 20 jela kwa kosa la kukutwa na vipande viwili vya meno ya tembo,” amesema hakimu.

Hakimu Mwankuga amesema upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha mashtaka pasina kuacha shaka, hivyo mahakama imemtia hatiani kama alivyoshtakiwa.

Hata hivyo, Mahakama ilimpa nafasi mshtakiwa huyo ambapo aliomba apunguziwe adhabu kwa sababu ana familia inayomtegemea.

“Mheshimiwa hakimu naomba mahakama inipunguzie  adhabu kwa sababu nina familia inayonitegemea,” ameomba mshtakiwa.

Awali, Wakili wa Serikali, Erick Kamala amedai kuwa kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kutokewa hukumu na upande wa mashtaka wapo tayari kusikiliza.

Pia, aliomba mahakama itoa adhabu kwa mujibu wa sheria.

Hakimu Mwankuga baada ya kusikiliza shufaa za pande zote, alitupilia mbali ombi la mshtakiwa na kumhukumu kifungo cha miaka 20 gerezani.

Katika moja ya mashahidi wa upande wa mashtaka waliowahi kutoa ushahidi katika kesi hiyo ni Ofisa Wanyamapori Augustino Kawala (37), kutoka Kikosi cha Kupambana na Ujangili Kanda ya Mashariki na Pwani, alidai kuwa yeye ndio aliyefanya tathimini ya meno hayo.

Kawala, mwenye uzoefu wa miaka 10 katika kikosi hicho, alidai kuwa Agosti 9, 2021 aliitwa na kiongozi wa kazi aende kituo cha Polisi Oysterbay kufanya utambuzi na tathimini ya vitu vilivyokamatwa ambayo vinazaniwa ni nyara za Serikali.

“Nilipofika kituo cha Polisi Oysterbay, nilionana na mtunza vielelezo aitwaye Koplo Juma na kumweleza kila kilichotumwa na bosi wangu,” amedai Kawala na kuongeza

” Nilipewa boksi rangi ya kaki ambalo kwa nje lina nembo ya K- Vant ambalo ndani yake kulikuwa na mfuko wa salfeti ambapo ndani yake kulikuwa na vipande viwili vya meno ya tembo vyenye junla ya kilo 15.18,” amedai shahidi.

Ameendelea kueleza kuwa baada ya kufanyia utambuzi aligundua kuwa yale ni meno ya tembo.

” Utambuzi huu ulikuwa ni kuangalia maombile kwa macho na kila nyara ina maumbile ya kipekee” amedai.

Ameendele kufafanua kuwa meno ya tembo yakikatwa katika vipande zaidi ya viwili huwa kuna kuwa na mistari midogo kwa ndani na huo ndio upekee uliopo katika meno ya tembo.

Ameendelea kudai kuwa baada ya utambuzi huo aligundua tembo aliyeuwani ni mmoja na thamani ya tembo mmoja ni dola za kimarekani 15,000,  ambapo kwa siku hiyo, dola moja ilikuwa ni Sh2,287.85, sawa na Sh34, 317,722.

” Nilipima uzito kwa kila kipande na meno ya tembo, ambapo kipande kimoja kilikuwa na uzito wa kilo 7.320 na kingine kilikuwa na uzito wa kilo 7.875 na kupata jumla ya kilo 15.18,” amedai shahidi.

Baada ya hapo aliandaa fomu ya tathimini ya Wanyamapori na kuijaza na kisha kumkabidhi mtunza vielelezo.

Kesi ya msingi:

Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo, Agosti 6, 2021 katika eneo la Tandale Mhuluge , lililopo wilaya ya Kinondoni, ambapo siku hiyo alikutwa akisafirisha vipande viwili vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh34 milioni mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mshtakiwa anadaiwa kusafirisha vipande hivyo, bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *