Je, pesa yako iko salama au hatarini?

Matumizi ya pesa mtandaoni yameleta mageuzi makubwa katika kufanya miamala ya kifedha hapa nchini, ikiwapa mamilioni ya watu fursa ya kipekee ya kupata huduma za kifedha na kusaidia kubadilisha taswira ya uchumi wa nchi.

Kwa mujibu wa ripoti ya FinScope Tanzania 2023, zaidi ya asilimia 72 ya Watanzania wanatumia huduma za pesa mtandaoni na huduma hizi zimekuwa tegemeo la kila siku.

Hata hivyo, mafanikio haya makubwa yanakabiliwa na tishio kubwa linaloongezeka kila siku: utapeli unaoendeshwa na akili mnemba (AI).

Wahalifu wa mtandaoni wanajaribu kutumia teknolojia za kisasa ili kuzidi mbinu za kiusalama zilizopo, hali inayohatarisha uchumi wa kidijitali nchini. Maamuzi tunayoyafanya leo ndiyo yatakayoamua kama pesa mtandaoni itaendelea kuwawezesha wananchi au kuwa hatari kwao.

Ripoti ya Global Cybersecurity Outlook 2025 ya World Economic Forum inasema kuwa karibu nusu ya taasisi zilizofanyiwa utafiti zinataja matumizi mabaya ya AI, kama vile deepfakes na mashambulizi ya ulaghai mtandaoni kuwa ni tishio kubwa zaidi kwa usalama wao wa kimtandao.

Wahalifu wanatumia AI kuiga sauti za watoa huduma kwa wateja, benki na hata mashirika ya serikali, hali inayowafanya watumiaji kuamini na kutoa taarifa zao za siri kama neno siri na nywila.

Hali hii imechangiwa na kuongezeka kwa visa vya utapeli wa pesa mtandaoni, ambapo Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) inaripoti kuwa kesi za utapeli ziliongezeka kutoka 12,603 mwishoni mwa mwaka 2022 hadi 21,788 mwishoni mwa mwaka 2023. Takwimu hizi zinaakisi maelfu ya watu hasa wanawake, wazee, na wakazi wa vijijini wanaopoteza akiba zao kwa njia za udanganyifu.

Moja ya mambo ya kushangaza tuliyogundua wakati wa kampeni yetu ya uhamasishaji juu ya utapeli mnamo mwezi Novemba mwaka jana ni kwamba watu wengi hawafahamu umuhimu wa kulinda PIN zao.

Wengine huwakabidhi ndugu au marafiki simu zao wafanye miamala kwa niaba yao bila kuelewa hatari zinazoweza kutokea. Kama Vodacom, tunatambua kuwa usalama wa miamala ya kidijitali si tu kuhusu mifumo ya kisasa, bali pia kuwaelimisha wateja wetu.

Kupitia vipindi vya redio, mikutano ya hadhara, na ujumbe wa kuelimisha, tunahimiza wateja wetu kutunza PIN zao kwa usiri mkubwa, kwani PIN ni sawa na saini ya kifedha. Lakini, je, uhamasishaji huu pekee unatosha kuleta mapinduzi ya uelewa wa kidijitali ili kuimarisha usalama wa pesa mtandaoni kwa Watanzania?

Zaidi ya vitendo vya mtu mmoja mmoja, uhalifu wa mtandaoni sasa umechukua sura mpya kwa kuendeshwa na mitandao ya wahalifu waliobobea. Sasa kuna huduma za “Cybercrime-as-a-Service” zinazoruhusu hata wale wasio na ujuzi wa teknolojia kuzindua mashambulizi ya kimtandao kwa urahisi.

Iwapo wananchi hawatakuwa na imani na huduma hizi, madhara yake yatakuwa makubwa zaidi ya hasara binafsi: ukuaji wa uchumi utayumba, ujumuishwaji wa kifedha utarudi nyuma na maendeleo ya kidijitali yatapata pigo kubwa.

Juhudi za kukabiliana na utapeli huu zipo, lakini zinapaswa kuongezeka kwa kasi zaidi. Kampuni za Mawasiliano kwa kushirikiana na TCRA zimezindua kampeni za uhamasishaji kama #Sitapeliki, ujumbe wa tahadhari kwa njia ya SMS, vipindi vya redio, na ushirikiano na vyombo vya usalama.

Kampeni hizi zinahimiza watumiaji kutambua utapeli na kuripoti matukio yanayotiliwa shaka. Hata hivyo, kwa kasi ambayo uhalifu wa AI unakua, elimu peke yake haitoshi.

Wahalifu wanazidi kuwa wabunifu huku sheria na mifumo ya utekelezaji zikiwa hazijaweza kuwafikia kwa kasi inayotakiwa. Ni lazima Tanzania ianze kuwekeza katika miundombinu madhubuti ya usalama wa kimtandao, kuwawezesha maafisa wa kupambana na uhalifu wa mtandaoni kwa zana za kisasa na kurekebisha mifumo ya sheria ili kuhimiza adhabu kali kwa wahalifu wa pesa mtandaoni.

Ushirikiano ndiyo silaha bora zaidi katika vita hivi. Wadau wa sekta ya mawasiliano, taasisi za kifedha, mashirika ya serikali na washirika wa kimataifa lazima waimarishe ushirikiano wao katika kubadilishana taarifa za kiintelijensia, kufuatilia mitandao ya wahalifu na kuanzisha mifumo ya kugundua uhalifu kabla haujafanyika.

Matumizi ya teknolojia mpya kama uthibitishaji wa alama za vidole (biometric verification) na mifumo ya ufuatiliaji inayoendeshwa na AI inaweza kusaidia kupunguza visa vya utapeli.

Lakini uUtapeli wa pesa mtandaoni si changamoto ya kiteknolojia pekee, bali ni kipimo cha uimara wa taifa katika kukabiliana na vitisho vya kidijitali. Kwa kuimarisha sheria, kukuza ubunifu na ushirikiano wa karibu kati ya sekta binafsi na serikali, Tanzania inaweza kulinda mustakabali wake wa kidijitali.

Agapinus Tax ni Mkurugenzi wa Udhibiti wa hatari na Utii wa Sheria Vodacom Tanzania

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *