Je, ni ‘divisheni one’ za mchongo?

Dar es Salaam. Wanafunzi 639 kati ya 752 waliomaliza kidato cha nne wamefanikiwa kupata daraja la kwanza kwa pointi saba katika shule 10 bora zilizofanya vizuri zaidi, Mwananchi imebaini.

Hata hivyo, ingawa wanafunzi wote wa shule hizo wamepata daraja la kwanza, takwimu zinaonyesha asilimia 85 ya wanafunzi hao wamepata daraja la kwanza kwa pointi saba. Uchambuzi wa kina unaonyesha zaidi ya nusu ya wanafunzi katika shule hizo wamepata alama hizo za juu.

Mfano shule ya sekondari ya St Francis Girls (Mbeya) iliyokuwa na wanafunzi 91 wote wamepata daraja la kwanza kwa pointi 7.

Shule iliyofuata ni Canossa (Dar es Salaam) wanafunzi 80 kati ya 89 wamepata daraja la kwanza kwa pointi 7.  Tengeru Boys (Arusha) wanafunzi 115 kati ya 129, Kibaha Secondary (Pwani) zaidi ya asilimia 60, Precious Blood (Arusha) asilimia 74, Ahava (Kibondo) asilimia 74 na Feza Boys'(Dar) asilimia 66.

Nyingine ni Kemebos (Bukoba), Ahmes (Bagamoyo) na Bethel SABS Girls (Mafinga) ambazo zote ni zaidi ya nusu ya wanagunzi wamefaulu kwa kiwango hicho.

Matokeo hayo yaliyotangazwa Januari 23, 2025 na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), wanafunzi 639 kati ya 752 wa shule hizo wamepata ufaulu wa daraja la kwanza kwa pointi 7.

Jambo hili linatajwa na wadau wa elimu kwamba uwekezaji uliofanyika katika elimu ndiyo chanzo cha matokeo hayo, wengine wakihoji umahiri wa wanafunzi hao.

Mwananchi leo Ijumaa Januari 24, 2025 imezungumza na mtafiti wa masuala ya elimu, Muhanyi Nkoronko, amesema miaka ya nyuma mwanafunzi kupata ufaulu wa Daraja la Kwanza kwa pointi 7 ilikuwa ni gumzo.

Anasema hiyo ilikuwa kutokana na mazingira na uhaba wa vitendea kazi hususani vitabu, walimu na miundo mbinu tofauti na sasa ambapo gepu limepungua.

“Zamani upatikanaji wa vitabu ilikuwa ni changamoto, hivi sasa sio tatizo tena, japo walimu bado hawatoshelezi, lakini idadi yao imeongezeka, vitendeakazi vinapatikana jambo lililopelekea uboreshaji wa ufundishaji kuongezeka n ahata ufaulu huo kuwa mkubwa,” amesema.

Amesema walimu pia wamepata mbinu stahiki za kumudu masomo, huku shule nyingi za sekondari zikiwa na watu wa kutoa ushauri nasaha kwa wanafunzi, jambo linalowajenga kuwa makini.

Mdau mwingine wa elimu, Ochola Wayoga amesema kuna mengi ya kujiuliza katika ufaulu huo, akieleza kwamba huenda wingi huo wa Daraja la Kwanza la pointi 7 unachagizwa na mabadiliko ya mitiani ya wakati huu.

“Nafikiri watakuwa wamesha ‘master coverage ya syllabus ya kidato cha kwanza hadi cha nne na kwa syllabus hiyo wanafunzi hao wana uwezo zaidi ya wanachofundishwa na kile kinachotolewa kwenye mitihani.

“Zamani kupata ‘division one’ ya pointi saba kwa watu 600 ilikuwa haiwezekani, sana utasikia mmoja mmoja kutoka Tabora na kwingine, hivi sasa sio ishu, tujiulize standard za mitihani yetu sasa zikoje? Na huyu anayepata daraja hilo basi abalance na stadi za kazi,” amesema Ochola.

Lakini mdau mwingine wa elimu aliyezungumza na Mwananchi, Nicodemus Shauri ameenda mbali zaidi na kusema uwingi wa waliofaulu kwa daraja hilo unaweza kuwa na mambo matatu.

“Mitihani ikiwa ni mirahisi lazima watu watafaulu sana, ingawa pia kuna uwezekano shule imefundisha sana na kupelekea mtokeo hayo au wanafunzi wamekuwa na uelewa mzuri, japo inahitaji utafiti wa kina kwenye hilo, huenda kukawa na sababu nyingine hatuwezi kujua hadi utafiti,” amesema.

Amesema mitihani inapotungwa migumu ndipo ufaulu unapungua na zamani ilikuwa ni hivyo, ndiyo sababu ilikuwa ni nadra kukuta ufaulu wa Daraja la Kwanza ya pointi 7 zikiwa nyingi.

“Ilikuwa ni wawili watatu au zaidi ya hapo kidogo, hivi sasa ni wengi, hivyo kuna mambo mengi nyuma yake, ambayo yanahitaji utafiti,” amesema.

Ufaulu huo nyuma ya pazia, shule zafunguka

Mbali na ufaulu huo wa daraja la kwanza kwa pointi 7, wanafunzi 104 wa shule hizo wamepata ufaulu wa daraja la kwanza kwa pointi 8-9 na wengine 100 wamepata ufaulu wa daraja hilo kwa pointi 10-17 huku kukiwa hakuna aliyepata daraja la pili na kuendelea.

Wakizungumzia ufaulu huo, baadhi ya wakuu wa shule hizo wamesema unajengwa kwenye nidhamu, ushirikiano, taalumainayotolewa katika mazingira rafiki yenye miundo mbinu yote ya kielimu sanjari na kuwajenga wanafunzi kisaikolojia kabla ya kwenda kwenye mtihani.

Mkuu wa shule ya Tengeru Boys, Gaudence Mtui akizungumza leo amesema kila mwaka wanajiwekea malengo ya shule, wazazi, walimu na wanafunzi.

‘Tunaishi kwenye malengo hayo, anayejaribu kutoka nje ya malengo huwa anakumbushwa na kurudishwam kundini, huo ndio msingi wa ufaulu wetu,” amesema.

Amesema wanazingatia maadili, taaluma na nidhamu ya kazi, hakuna kupoteza kipindi na ikitokea mwalimu amefanya hivyo atatafuta njia ya kufidia.

‘Huwezi kufaulisha wakati huna nidhamu, tunalizingatia sana hilo na wanafunzi tunawajenga kuwa na hofu ya Mungu huk tukihakikisha hadi kufikia Agosti tunakuwa tumemaliza mad azote ili kupata muda wa kufanya marudio,” amesema.

Mkuu wa shule ya Ahava, Jeremiah Nyamukama anasema siri kubwa katika matokeo hayo ni kumtanguliza Mungu.

“Kwa kufanya hivi, zile tabia mbaya mbaya zinazosababisha utovu wa nidhamu hazionekani na kusihi kwa nidhamu huku wakishirikiana kitaalmua kati ya mzazi, mwalimu na mwanafunzi.

‘Ukiachana na taaluma, huwa tuawajengea watoto kujiamini na wiki mbili kabla ya mitihani yao tunawapa semina elekezi na kuwajengea uwezo kupitia wahamasishaji,” amesema.

Wakuu wa shule hizo pia kwa nyakati tofauti wameeleza namna wanavyo waandaa wanafunzi kisaikolojia muda wa mitihani unapokaribia sambamba na kuwajenga kuwa washindi tangu siku ya kwanza wanapojiunga na kidato cha kwanza kwenye shule zao.

Je, wanafanya mchujo kila mwaka?

Mkuu wa Tengeru Boys alipoulizwa endapo wana utaratibu wa kuwarudisha madarasa ya chini wanafunzi ambao hawajafikia wastani uliowekwa na shule alisema, hawana.

“Hapa kwetu tukishapokea mwanafunzi ni wa kwetu, hatuna mchujo wa kuwarudisha madarasa ya chini, isipokuwa wale wanaojiunga na kidato cha kwanza tunaanza nao mwezi wa tisa (Septemba) mara tu wanapohitimu darasa la saba.

“Tutakuwa nao tukiwafundisha pre form one, kwa kuwapima kuona kama tunaweza kwenda nao, watakaofanya vizuri ndiyo tunaendelea nao form one (kidato cha kwanza), alisema.

Mkuu wa Ahava pia hakutofautiana na mtangulizi wake naye akieleza kutokuwa na utaratibu wa kuwachuja wale wanaoshindwa kufikia wastani wa shule kila mwaka.