
Matumizi ya hundi, ambayo kihistoria yamekuwa njia maarufu ya kufanya malipo katika mfumo wa kibenki na fedha, yanaonekana kupungua kwa haraka. Taarifa za takwimu kutoka Ripoti ya Mwaka ya Mwenendo wa Mifumo ya Malipo nchini kwa mwaka 2023 zinaonyesha kuporomoka kwa kasi katika matumizi ya hundi kwa malipo mbalimbali. Hali hii inaweza kuibua swali: Je, huu ni mwanzo wa mwisho wa matumizi ya hundi katika malipo?
Matumizi ya hundi katika miamala yenye thamani kubwa yanaendelea kupungua kwa kasi. Kwa mfano, idadi ya hundi za shilingi zilizotumika iliporomoka kutoka 546,620 mwaka 2022 hadi 485,972 mwaka 2023, ikiwa ni kupungua kwa asilimia 11 katika mwaka mmoja. Aidha, thamani ya miamala kwa hundi hizo ilishuka kwa asilimia 4, ikitoka Sh1.98 trilioni hadi Sh1.89 trilioni.
Hali hii inaonekana pia katika miamala ya hundi za Dola za Kimarekani (USD), ambapo thamani ya malipo yaliyofanyika kwa hundi imepungua kwa asilimia 19, kutoka dola milioni 238.96 hadi dola milioni 192.41 katika mwaka mmoja.
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, matumizi ya hundi yamekuwa yakishuka. Mwaka 2019, zaidi ya hundi 554,000 zilitumika, lakini idadi hii iliongezeka kwa muda mfupi mwaka 2020 na kisha kuanza kuporomoka hadi kufikia 485,972 mwaka 2023. Mwelekeo huu unaonyesha mabadiliko makubwa katika jinsi watu wanavyofanya malipo, ambapo wengi sasa wanachagua njia mbadala.
Kwa mfano, majukwaa ya malipo ya kidijitali kama vile pesa mkononi, huduma za malipo kielektroniki, na benki za mtandao yanakuwa chaguo la wengi. Tofauti na hundi, ambazo zinaweza kuchukua siku kadhaa kuthibitishwa na kupitishwa, majukwaa haya yanatoa urahisi na uharaka wa kuhamisha fedha papo hapo. Kwa nini mtu apate taabu wakati kuna njia rahisi na za haraka zaidi?
Sambamba na hilo, kuanzishwa kwa Mfumo wa Malipo wa Haraka (TIPS) au TANQR kumekuwa kama daraja linalounganisha mifumo tofauti ya malipo. Mfumo huu unawawezesha watumiaji wa huduma za kibenki na pesa mkononi kuhamasisha malipo kwa haraka, huku ukiongeza idadi ya miamala na kuimarisha urahisi wa kutuma na kupokea fedha kutoka kwa mifumo mbalimbali. Hii imewafanya watu kuona kuwa ni rahisi na salama kufanya malipo kwa mtindo huu, ukilinganisha na kutumia hundi.
Vilevile, mambo mengine kama vile kuepuka udanganyifu katika matumizi ya hundi yanaweza kuwa yamechangia katika mwelekeo huu. Majukwaa ya malipo ya kidijitali yana mifumo ya kulinda taarifa za akaunti na uthibitisho wa kibayometriki, ambayo inawasaidia watumiaji kufuatilia miamala yao ya malipo muda wowote, wakijua hatua iliyofikiwa. Mambo haya yamewafanya watu wengi kuchagua kutumia njia mbadala za malipo, iwe ni kwa ajili ya miamala midogo au mikubwa, na hivyo kuacha pembeni matumizi ya hundi.
Hata hivyo, bado ni mapema kusema kuwa matumizi ya hundi yatakwisha kesho, au mwaka ujao. Wapo baadhi ya makundi ya watumiaji, kama vile taasisi za Serikali na makampuni, ambayo bado yanatumia hundi katika kufanya miamala ya malipo na kuweka rekodi za matumizi ya fedha.
Kwa sasa tunachoweza kusema ni kuwa umuhimu wa hundi kama njia iliyowahi kutawala katika mfumo wa malipo unaendelea kupungua. Mwelekeo tunaoutegemea ni kwamba ukuaji wa malipo ya kidijitali utaifanya miamala ya hundi kuwa nadra zaidi. Vilevile, Kadri biashara na watumiaji wanavyohamia kwenye njia mbadala za malipo kwa sababu ya kupata uharaka, usalama, na ufanisi katika kufanya malipo, ni wazi kuwa siku za mwisho kwa uhai wa matumizi ya hundi zimeanza kuhesabika.