Je, kuweka akiba ni utajiri au umasikini?

Watoa ushauri wengi huwa wanawaaminisha watu kuwa mafanikio huja kwa kufanya kazi kwa bidii. Baada ya kufanya kazi kwa bidii na kupata kipato, wanawashauri watu kuweka akiba kipato hicho.

Japokuwa hakuna ubaya katika kuweka akiba, changamoto huja kwa kuwa washauri hawa hawawafundishi watu hawa nini kifuate baada ya kuweka akiba. Muweka akiba analipa kodi kubwa sana ukilinganisha na mwekezaji.

Serikali inamkata kodi mtu huyu kuanzia anapofanya kazi kwa bidii kupata kipato, katika kuweka akiba na katika kutumia akiba hiyo. Ili uwe na akiba ya Sh1 milioni unatakiwa upate mshahara wa angalau wa Sh1.18 milioni ambapo Serikali itachukua kodi ya mapato (PAYE) ya Sh180,000 na kukuacha na Sh1 milioni.

Unakwenda kuweka akiba hiyo Sh1,000,000 ambapo benki wanakupa faida ya asilimia 5 kwa kukaa na pesa yako kwa mwaka mzima. Kwa kipindi hicho pesa itakuwa imeshuka thamani (kwa sababu ya mfumko wa bei) angalau kwa asilimia 3.1.

Kushuka kwa thamani huku kunapelekea bakaa ya faida yako kuwa asilimia 1.9 badala ya asilimia 5 uliyopewa na benki. Pia Serikali inakata kodi tena ya asilimia 10 kwenye riba uliyopata. Twende kwenye uhalisia, ukiweka akiba ya Sh 1 milioni kwa mwaka mzima, utapata faida ya Sh50,000. Serikali itachukua Sh5,000 ambayo ni asilimia 5 na kukuachia 45,000.

Baada ya kodi utaondoka na Sh1.04 milioni ambayo thamani yake halisi itakuwa ni Sh1.01 milioni, ukiondoa kushuka thamani kwa pesa (inflation) ambako ni asilimia 3.1. Umeweka akiba Sh1 milioni kwa mwaka mzima, unapewa pesa inayolingana na Sh1.01 milioni.

Ukirudi kuangalia mwanzo wa huu mchakato ni kuwa umetumia kipato cha Sh1.18 milioni kwenye uwekaji huu wa akiba. Mwisho wa mchakato umepata Sh1.01 milioni ambayo ni ndogo kuliko pesa uliyoweka akiba.

Bakaa ya mchakato huu wa kuweka akiba ni hasara. Kama unahitaji kufanya kazi kwa bidii ili kupata utajiri, unatakiwa kufikiria zaidi ya kuweka akiba. Pesa hiyo uliyoweka akiba benki, unaweza kuamua kuwekeza katika biashara ndogondogo za kichuuzi ambazo zinaweza kuifanya iongezeke.

Ikiwa una changamoto ya kuwekeza kwenye biashara ndogo ndogo, unaweza kuamua kuwekeza kwenye maeneo ambayo yatafanya faida yake iwe ni kubwa kuliko kushuka thamani kwa pesa (inflation).

Maeneo unayoweza kuyafikiria ni katika kununua vipande, hisa, bondi au hati fungani. Mafanikio huja baada ya kufanikiwa kutambua tofauti na matokeo ya kuweka akiba ama kuwekeza.